Wednesday, January 11, 2017

Kauli za wanasiasa Kenya zawakosesha amani wananchi

Mbunge wa Garissa Mjini, Aden Duale akihojiwa

Mbunge wa Garissa Mjini, Aden Duale akihojiwa na wanahabari jijini Nairobi, Kenya. Picha na Maktaba 

By Dorothy Jebet

Nchini Kenya wanasiasa wapo katika kipindi ambacho huweza kutamka matamshi yoyote wanayoona yatawasaidia kupata kura kwenye Uchaguzi Mkuu utakaofanyika Agosti mwaka huu.

Baadhi yao wamekuwa madarakani tangu mwaka 2013 na ‘wamelewa’ kutokana na sumu ya uongozi. Hawatambui wanalosema wala wanalomaanisha.

Kama ilivyo desturi ya wanasiasa wetu, chuki, ukabila na ukiritimba ndizo mbolea na maji yanayonyunyizia tamaa zao za uongozi ili zipate rutuba.

Wanasiasa wanajipiga vifua kuonyesha ubabe wao lakini hawatafakari matokeo ya matamshi yao. Ndimi zao zitachoma nchi mwaka huu ikiwa tahadhari haitachukuliwa.

Macho yote na hasira sasa vinamwelekea mbunge wa Garissa Mjini, Aden Duale kwa matamshi yake ya chuki na uchochezi aliyoyatoa kwenye video iliyosambazwa katika mitandao ya kijamii.

Katika video hiyo, Duale ambaye pia ni mmoja wa viongozi katika Bunge la Kitaifa, anasikika akitoa matamshi hayo kwenye mkutano na vijana kutoka eneo lake la ubunge.

Mbunge huyo anazungumza kwa Kiswahili akiwaomba vijana wa jamii ya Kisomali kuunda vikundi vya watu watano ili wapewe ‘kibarua’ cha kufanya msimu huu wa kampeni na uchaguzi.

Mbunge huyo mwenye asili ya Kisomali, aliwaambia vijana kwenye video hiyo wasikubali jamii ya Wakamba kupiga kura katika Kaunti ya Garissa.

“Mimi nitawatetea vilivyo na kuwalipia faini kortini ikiwa mtanaswa na mkono wa shera,” anasema Duale.

Anawaambia vijana ambao walikuwa wakipiga makofi kila baada ya kumaliza sentensi moja ya maneno hayo ya uchochezi.

Kaunti ya Garissa ina idadi kubwa ya watu jamii ya Wakamba wanaofanya kazi au biashara ndogo ndogo. Kaunti ya Kitui ambayo ni nyumbani kwa Wakamba inapakana na Garissa kwa hivyo, si ajabu kupata jamii hii wakitafuta riziki Garissa.

Hii siyo mara ya kwanza kwa mbunge huyo kunaswa akichochea watu wa jamii yake dhidi ya jamii ya Wakamba. Miaka miwili iliyopita alihusishwa na shambulio la al-Shabaab waliokuwa wamevamia eneo la Eastleigh jijini Nairobi na kuua watu kadhaa.

Alipotembelea eneo hilo jioni hiyo, Duale aliwasihi wavamizi wasiwasumbue Wasomali, bali waende maeneo kama vile Machakos (ni Ukambani) “kufanya kazi yao huko.”

Ulimi hauna mfupa lakini unaweza kuchoma nchi na kusababisha umwagikaji wa damu. Akihutubia vyombo vya habari wiki iliyopita, aliyekuwa Naibu wa Spika wa Bunge la Taifa, Farah Maalim alisema tayari vijana waliokuwa wamepewa ‘kazi’ ya kuwafukuza Wakamba kutoka Garissa, wameanza kazi hiyo na wamewavamia Wakamba wawili.

Maalim pia anatoka Kaunti ya Garissa na anapozungumza kuhusu masuala ya eneo hilo, bila shaka, anajua analosema.

Matamshi hayo ya chuki ya Duale ambaye anapenda kuwadhihaki viongozi wengine bila kujali athari za maneno yake, yaliwaghadhabisha viongozi wengi.

Viongozi wamekaa kimya

Inasikitisha kwamba, viongozi wa makanisa hawajamshutumu kiongozi huyo kwa matamshi hayo ya uchochezi. Kama kawaida, wao pia wanaegemea kwa pande za upinzani au Jubilee.

Viongozi wa Muungano wa Jubilee hawajasema lolote kuhusu matamshi ya Duale. Inaonekana ni kwa sababu Duale ni kiongozi wa muungano wao bungeni na hawataki kumkosoa kwa sababu pengine wote wanaunga mkono matamshi yao.

Viongozi wa Ukambani ndiyo wamejitokeza kumkashifu Duale kwa matamshi hayo wakisema, Serikali ya Jubilee isipomchukulia hatua, wao wenyewe watawasiliana na Mahakama ya Kimataifa ya Uhalifu (ICC) wakitaka kiongozi huyo achukuliwe hatua za kisheria kabla umwagikaji damu haujaanza.

Tume ya Uwiano na Utengamano (NCIC) inayoongozwa na mwanasiasa mkongwe, Francis Ole Kaparo imesema itamchukulia hatua Duale ikiwa uchunguzi unaofanywa kuhusu video hiyo itaonyesha kwamba kweli, mwanasiasa huyo alisema maneno hayo maovu na machafu.

Wakenya hata hivyo wanajua kwamba, NCIC haiwezi kumchukulia hatua Duale kwa sababu ni mwanasiasa wa Jubilee. Kaparo pia ni mwanasiasa wa Jubilee na hawezi kufanya mambo yanaweza kuharibu muungano wao.

Ni bayana kwamba, kama maneno yao yangekuwa yametamkwa na kiongozi yeyote wa upinzani, hatua za dharura zingefanywa na mara moja angekuwa amenaswa na kufikishwa mahakamnai na kufunguliwa mashtaka bila kupoteza wakati.

Sheria inatumika vibaya mno nchini. Kama wewe ni wa upinzani, mkono wa sheria unakufikia haraka na ukiwa wa muungano tawala, maneno yako huchukua muda mrefu kuchunguzwa na baadaye yanapuuziwa mbali.

Nina hakika Duale hawezi kuchukuliwa hatua yoyote na mawakala wa Serikali. Mwanasiasa huyo kama kawaida yake alisema hakuchochea yeyote. Huu ni uongo kwa sababu watu waliokuwa kwenye mkutano huo wamedhibitisha kwamba alichochea vijana kuwavamia jamii ya Wakamba.

Wiki mbili zilizopita, mbunge huyu aliwahutubia wanahabari katika majengo ya Bunge na kusema kwamba atawashurutisha wabunge wamjadili na kumwadhibu Jaji wa Mahakama Kuu, George Odunga akisema alikiuka sheria kwa kusikiza kesi iliyowasilishwa mahakamani na wanasiasa wa muungano wa upinzani, Cord.

Cord ilikuwa imeenda kortini baada ya wabunge wa Jubilee wakiongozwa na Duale, kupitisha kwa lazima na bila kuzingatia kanuni za Bunge, mswada wa kupiga na kuhesabu kura bila kutumia mashine za kisasa zinazotambua sura ya mpiga kura.

LSK

Mbunge huyo alikighadhabisha Chama cha Wanasheria (LSK). Rais wa LSK, Isaac Okero alisema Duale alishambulia uhuru wa mahakama na kutumia vibaya mamlaka yake bungeni. Jaji Odunga ni Mluo kutoka kabila la kiongozi wa Upinzani, Raila Odinga. Kwa kuwa upinzani ulifikisha maombi yao mbele ya mahakama yake, Duale anaamini walifanya hivyo kwa sababu ya ukabila.

Hii ni dhana potofu kwa kuwa majaji wanawatumikia Wakenya wote bila kujali kabila wala tabaka na kwa hivyo, matamshi ya Duale hayafai kabisa haswa kwa kiongozi mwenye wadhifa kama wake.

Bunge la Kitaifa litaanza shuguli zake za mwaka huu Januari 24. Wakenya wanasuburi kuona ikiwa Duale atathubutu kuanzisha mjadala bungeni kuhusu Jaji Odunga.

Duale anawachukia Wakamba na Wajaluo kwa sababu ni makabila yenye upinzani kwa muda mrefu.

Ikiwa Wakamba ambao wanaishi Kaunti ya Garissa watapiga kura kwa wingi, Duale hatapata kura za kutosha kumwezesha aingie bungeni kuwakilisha Garissa Mjini.

Mwandishi ni mchambuzi wa masuala ya siasa na jamii. Anashi Nairobi nchini Kenya. Anapatikana kwa baruapepe: jebetdorothyy@gmail.com

-->