Kazi ya Mkapa yaonyesha mwanga nchini Burundi

Msuluhishi wa mgogoro wa Burundi, Benjamin Mkapa (kushoto) akisalimiana na Katibu mkuu wa chama tawala cha Burundi, CNDD-FDD, Evariste Ndayishimiye baada ya kikao cha kutafuta suluhu jijini Arusha wiki iliyopita. Katikati ni Mjumbe wa Umoja wa Mataifa nchini humo, Jamal Benomar. Picha na Filbert Rweyemamu

Muktasari:

Mazungumzo hayo yanafanyika baada ya nchi hiyo kukumbwa na machafuko yaliyosababisha vifo vya mamia ya wananchi waliokuwa wakiandamana kwenye mitaa ya Jiji la Bujumbura, kupinga Rais wa nchi hiyo, Pierre Nkurunziza kujiongezea muda wa kuitawala Burundi.

Mgogoro wa kisiasa ulioikumba nchi jirani ya Burundi tangu mwaka juzi umeanza kupata mwanga wa amani baada ya mazungumzo yanayoendelea chini ya Rais mstaafu wa Tanzania, Benjamin Mkapa.

Mazungumzo hayo yanafanyika baada ya nchi hiyo kukumbwa na machafuko yaliyosababisha vifo vya mamia ya wananchi waliokuwa wakiandamana kwenye mitaa ya Jiji la Bujumbura, kupinga Rais wa nchi hiyo, Pierre Nkurunziza kujiongezea muda wa kuitawala Burundi.

Katika machafuko hayo si wananchi wa kawaida pekee waliopoteza maisha, bali hata viongozi wakubwa kisiasa akiwamo aliyekuwa Mbunge wa Bunge la Afrika Mashariki (Eala), Hafsa Mosi na maofisa wengine wa jeshi na wanasiasa waliuawa katika kipindi hicho.

Sababu kuu ya sintofahamu hiyo ni uamuzi wa Nkurunziza kugombea urais kwa awamu ya tatu, kinyume na mkataba wa amani uliotiwa saini Arusha, Tanzania mwaka 2000 baada ya nchi hiyo kuwa kwenye mapigano ya muda mrefu.

Hata hivyo, madai ya Nkurunziza kugombea kwa awamu ya tatu yalipingwa vikali na wapinzani wake wakisema alikuwa amekamilisha vipindi viwili vinavyotakiwa kikatiba, lakini kambi yake ilidai bado Rais huyo alikuwa anaruhusiwa kuongoza kwa kipindi kimoja zaidi.

Kambi yake ilishikilia hoja kwamba katika awamu ya kwanza mwaka 2000, Rais Nkurunziza hakuchaguliwa na wananchi bali na Bunge, hivyo awamu hiyo haiwezi kuhesabiwa kwa kuwa Katiba inasema Rais wa Burundi ataongoza nchi hiyo katika vipindi visivyozidi viwili kwa kuchaguliwa na wananchi.

Baada ya tafsiri hiyo iliyotolewa na Mahakama ya Burundi na Nkurunziza kushikilia msimamo huo kugombea na hatimaye kushinda, ndipo yalizuka mapigano ya kisiasa yaliyoua mamia na kuzalisha maelfu ya wakimbizi katika nchi jirani za Tanzania, Uganda, Rwanda wanaofikia 400,000.

Jumuiya ya Afrika Mashariki (EAC) Mei, 2015 iliitisha mkutano wa dharura jijini Dar es Salaam kujadili ili kupata ufumbuzi wa kudumu wa mgogoro huo, hata hivyo wakati Rais Nkurunziza akiwa Dar es Salaam, kuliibuka taarifa za mapinduzi ya kijeshi yaliyoongozwa na Meja Jenerali Godefroid Niyombare aliyewahi kuwa Mkurugenzi wa Usalama wa Taifa kabla ya kufukuzwa kazi baada ya kupinga wazi Nkurunziza kugombea awamu ya tatu.

Hata hivyo, mapinduzi hayo hayakufanikiwa na Nkurunziza akafanikiwa kurejea Burundi na kudhibiti hali hiyo. Wakuu wa EAC walimteua Rais wa Uganda, Yoweri Museveni kuwa Mpatanishi Mkuu (Mediator)

Hatua ya Wakuu wa EAC kumteua Museveni ilipokewa kwa shauku kuwa kwani ililenga kuwasaidia Warundi kuondoa tofauti zao za kisiasa na kuendelea na maisha ya kawaida.

Rais Museveni wakati huo alikuwa kwenye harakati za uchaguzi kupeperusha bendera ya chama chake cha NRM hivyo kuomba wakuu wenzake apatikane msuluhishi wa kumsaidia majukumu hayo ambaye ni Rais mstaafu wa Tanzania, Benjamin Mkapa ambaye ameshaongoza awamu tatu za mazungumzo na kuonekana mwanga wa matumaini.

Licha ya kasoro ambazo zimekua zikilalamikiwa kwenye awamu ya kwanza na ya pili ya mazungumzo ya kutafuta suluhu ya Burundi, kuhusu idadi na aina ya wajumbe wanaotakiwa kushiriki mazungumzo hayo, kumekuwa na maendeleo muhimu katika kumaliza mgogoro huo.

Mkapa amekuwa akishirikiana na wadau muhimu kupata wajumbe wanakaowakilisha makundi mengine ambayo ni vyama vya siasa, asasi zisizo za kiserikali yakijumuishwa wanawake na vijana, Serikali na jumuiya ya kimataifa ambao ni wadau muhimu katika kufanikisha mazungumzo hayo.

Akifunga mazungumzo ya awamu ya tatu yaliyofanyika Arusha wiki iliyopita, Mkapa alisema licha ya kwamba pande zote zinazohusika katika mchakato huo wameonyesha nia ya dhati kutafuta suluhu, yapo mambo yanayozuia kusonga mbele ambayo yanahitaji kauli ya viongozi wakuu wa EAC kuitisha mkutano wa dharura kuyajadili na kutoa majibu.

“Nitawasilisha mapendekezo haya kwa haraka zaidi kwa Msuluhishi Mkuu (Rais wa Uganda,Yoweri Mseveni) na Mwenyekiti wa Wakuu wa Jumuiya ya Afrika Mashariki (EAC), Rais John Magufuli kwa ajili ya uamuzi zaidi baada ya kuona nia ya dhati kutoka kwa wajumbe,” anasema Mkapa

Marais watatu wastaafu wa Burundi, Sylvester Ntibantunganya, Pierre Buyoya na Domicien Ndaizeye ni miongoni mwa viongozi walioyapa heshima majadiliano hayo kwa kushiriki.

Mbali na hao, wengine waliohudhuria ni viongozi wa Chama cha Forces of National Liberation (FNL-Amizero) ambaye ni Makamu wa Rais wa Bunge, Aghaton Rwasa, Mwenyekiti wa CNDD, Leonard Nyangoma na Mjumbe maalumu wa Umoja wa Mataifa nchini Burundi, Jamal Benomar na ujumbe wa Umoja wa Afrika.

Katika mwanga huu ambao haupaswi kuzimwa unawalazimu wanasiasa kuweka kando masilahi binafsi na kutoa kilio chao kwa jumuiya ya kimataifa kusaidia hali ya kibinadamu inayowakumba wananchi wengi na njaa iliyosababishwa na ukame wa muda mrefu.

Mwanga wenyewe

Kwa mujibu wa Mkapa, wajumbe wanaamini kuwa Burundi ni taifa lenye mamlaka yake kamili, hivyo lina wajibu wa kuhakikisha ulinzi, usalama na kulinda haki za binadamu kwa wananchi wote na kuwa mgogoro huo ambao chanzo chake ni kutokuafikiana kisiasa, unaweza kupatiwa ufumbuzi.

Anasema wamekubaliana kukomesha kila aina ya vurugu na kuondoa tofauti zilizopo za kisiasa na kuendelea na mazungumzo ya kisiasa, ili kuimalisha uchumi wa nchi wakati mabadiliko yakifanyika kuwa na uchaguzi huru na haki mwaka 2020.

Naibu Spika wa Bunge, Aghaton Rwasa anasema kumekua na mafanikio katika mazungumzo hayo na anaamini Wakuu wa EAC watatoa mwongozo mzuri kwa haraka ili kutoa nafasi kwa wananchi wa Burundi kufanya shughuli za kiuchumi kwa uhuru zaidi.

“Naamini mambo ya msingi yako wazi kama anavyosema msuluhishi kuwa kuna utashi wa pande zote, jambo la msingi ni wakuu wa EAC watoe mwongozo wa nini kifanyike na lini kifanyike ili kutoa njia ya amani ya kudumu,”anasema Rwasa ambaye alikuwa mmoja wa wapiganaji wa msituni kabla ya makubaliano ya mkataba wa Arusha mwaka 2000.

Leonard Nyangoma anasema ili kuongeza msukumo katika kusaka amani ni wakati wa Serikali kushiriki mazungumzo hayo moja kwa moja na kuwataka Warundi kuwa na subira na matumaini ya kupata amani licha ya kuamini kuwa inaweza kuchukua muda zaidi.

Kwa upande wake Katibu Mkuu wa chama tawala cha CNDD-FDD, Evareste Ndayishimiye anaamini hatua iliyofikiwa katika mazungumzo ya vyama vya kisiasa ni mazuri na ametoa wito kwa wananchi walio katika nchi jirani kurejea nyumbani kutokana na hali ya utulivu kurejea.

“Natoa wito kwa wananchi waliokimbilia nchi jirani warudi nyumbani kumekuwa na utulivu, njooni tujenge nchi yetu,” anasema.

Kutokana na mgogoro huo wa takribani miaka miwili, Mkapa anaamini ukimalizika utaisaidia Burundi kurejesha matumaini katika jumuiya ya kimataifa kuanza kuisaidia baada ya kuitenga kutokana na mvutano huo wa kisiasa na kuwa ushiriki wa Serikali ya Burundi utaongeza thamani ya majadiliano.

Serikali ya Burundi ilitoa taarifa ya kutoshiriki kwa madai ya kushirikishwa watu waliofanya jaribio la mapinduzi lililoshindwa kutoka kikundi cha muungano wa vyama vya siasa pamoja na sehemu ya wanajeshi cha CNARED.

Mwenyekiti wa Chama cha FNL, Jacques Bigirimana anasema umefika wakati kuweka kando tofauti zao na kutanguliza masilahi ya Burundi ambayo ni amani akisema katika siasa hakuna adui wala rafiki wa kudumu bali yaangaliwe maslahi mapana ya nchi.

Ajenda zilizojadiliwa mbali na kudumisha hali ya usalama, ni kuhakikisha kuna utawala wa kisheria na kukomesha vitendo viovu. Nyingine ni utekelezaji wa mkataba wa amani na maridhiano wa Arusha, kuimarisha utamaduni wa utawala wa kidemokrasia na uhuru wa kisiasa na masuala ya haki za binadamu.