Kenya itaheshimu uamuzi wa kumrejesha Miguna?

Muktasari:

Jaji wa Mahakama ya Juu, Luka Kimaru alitoa uamuzi huo Alhamisi alasiri baada ya mawakili wa Miguna, Otiende Amollo na James Orengo kuwasilisha kesi ya kutaka kiongozi huyo matata arejee Kenya kwa kuwa “Kenya ni nchi yake ambapo alizaliwa na ana haki ya kuishi hapa bila kushurutishwa kuhamia nchi nyingine.”

Hata kabla ya wino uliotumika kuandika uamuzi wa mahakama kukauka, Serikali ya Kenya imepinga vikali uamuzi kwamba kutimuliwa kwa kiongozi wa vuguvugu la National Resistance Movement (NRM) ulikwenda kinyume cha sheria.

Jaji wa Mahakama ya Juu, Luka Kimaru alitoa uamuzi huo Alhamisi alasiri baada ya mawakili wa Miguna, Otiende Amollo na James Orengo kuwasilisha kesi ya kutaka kiongozi huyo matata arejee Kenya kwa kuwa “Kenya ni nchi yake ambapo alizaliwa na ana haki ya kuishi hapa bila kushurutishwa kuhamia nchi nyingine.”

Serikali inasema uamuzi huo wa Jaji Kimaru hauna msingi kisheria kwa sababu Miguna alifukuzwa kihalali.

Kauli ya Serikali ilisema; “uamuzi wa Kimaru unaenda kinyume na azimio la nchi kuhusu watu wasiotakikana.”

Lakini, Kimaru aliweka wazi kwamba Serikali ilifanya makosa kumfukuza Miguna kutoka nchi yake aliyozaliwa.

Huku Serikali ikionyesha kuudhika na uamuzi huo, Kimaru aliendelea na kuiamuru serikali imrejeshee Miguna hati yake ya kusafiria inayoshikiliwa.

Mahakama ilitoa notisi ya siku saba kwa Serikali ya kuwataka wawasilishe mahakamani pasipoti ya Miguna.

Miguna alifukuzwa Kenya Februari 7 baada ya kukamatwa na kuzuiwa katika vituo mbalimbali vya polisi kwa siku nne.

Waziri wa Mambo ya Ndani, Fred Matiang’i alisema Miguna si Mkenya halisi na alipata pasipoti kwa njia za ujanja.

Hata hivyo, wengi walishangaa kwa nini mwanasiasa huyo aliyejitangaza kama Jemedari mkuu wa vuguvugu la NRM alikubaliwa kuwania ugavana wa Jimbo la Nairobi mwaka jana ilhali alikuwa mgeni nchini.

Matiang’i alisisitiza kwamba mwanasiasa huyo ni raia wa Canada na kwa hivyo ilifaa arudi kwao kwa sababu nchi hiyo inamuhitaji sana.

Wafuasi wa NRM na Nasa walihuzunishwa mno na kufurushwa kwa Miguna. Maandamano yalitokea maeneo ya Kisumu na Migori lakini polisi waliyazima.

Lakini, kilio kiligeuka furaha baada ya Jaji Kimaru kutangaza kwamba Miguna ni Mkenya na anafaa kurejea nyumbani haraka iwezekanavyo.

Wafuasi hao walikejeli Serikali katika mitandao ya kijamii kufuatia taarifa yake ya kupinga uamuzi wa mahakama.

Dalili ya mvua ni mawingu na kulingana na matamshi ya Serikali kufuatia uamuzi huo, ni wazi kwamba maagizo hayo yanaweza kupuuzwa na Miguna ataendelea kuishi Canada. Hata hivyo, ni ombi la upinzani kwamba Serikali ya Uhuru Kenyatta itaheshimu amri za mahakama na kukubali Miguna arudi nyumbani.

Huku hayo yakiendelea, Miguna alianzisha kampeni inayolenga kuandikisha wafuasi wengi wa vuguvugu hilo la NRM lilioharamishwa na Serikali. Miguna anasema zoezi hilo litaanza kutimua vumbi kuanzia keshokutwa Februari 19 nchini kote.

Haijulikani mwanasiasa huyo atatumia mbinu gani katika kuhakikisha zoezi hilo linashika kasi ikikumbukwa kwamba bado yuko Canada.

Alifukuzwa baada ya kushiriki katika hafla ya kuapisha Raila Odinga Januari 30, huku Serikali ikisema Miguna ni hatari kwa usalama wa nchi na ikaharamisha vuguvugu lake.

Matamshi yake katika ukurasa wake wa Twitter muda mfupi baada ya kesi yake kutolewa huku, Miguna alimwambia Rais Uhuru amfukuze mkewe Margaret Kenyatta ambaye ana uraia wa nchi mbili—moja ya Kenya na mwingine wa Ujerumani ambapo mamake alitoka.

Pia, Miguna anamtaka Uhuru amfukuze binamu yake Anna Nyokabi kutoka Kenya kwa sababu pia ana uraia wa Canada na Kenya. Nyokabi alikuwa mbunge mwakilishi wa Wanawake wa jimbo la Kiambu tangu 2013 hadi mwaka jana.

Uzoefu wa Jaji

Hii si mara ya kwanza kwa Jaji Kimaru kuharamisha kufukuzwa kwa raia wa Kenya.

Mnano 2008 alikomesha kufukuzwa kwa mwanasiasa Muhammad Sirat. Mwanasiasa huyo baadaye alichaguliwa Mbunge wa Wajir Kusini katika jimbo la Wajir. Kimaru ameonyesha tena kwamba anazingatia sheria kwa kutangaza kwamba Miguna ni Mkenya na anafaa kurudi nyumbani haraka iwezekanavyo.

Seneta wa Busia, Moses Wetangula anasema amesikishwa na jinsi Serikali inawatesa viongozi wa upinzani.

Kuna wengine wasiofurahia ushindi wa kesi ya Miguna na wanauliza kwa nini akaenda kortini ilhali alikuwa ametisha kurejea nchini kwa vyovyote vile.

Akizungumza wiki jana baada ya mumewe kufurushwa, mke wa Miguna alisema mwanasiasa huyo alikuwa amepanga kusafiri hadi Canada baada ya kuapishwa kwa Raila, lakini hakufika hadi Februari 7 alipofukuzwa.

Mwanamke huyo anaishi Canada alizungumza na Jarida moja la Canada linaloitwa Maclean, muda mfupi baada ya mumewe kufukuzwa.

Alisema watoto wao hawakuwa wanajua kwamba baba yao alikuwa amenaswa na kuzuiliwa na polisi ijapokuwa yeye alikuwa ana habari hizo.

Mwanamke huyo alisema hakuwa anajua kama mumewe angetoka katika mikono ya polisi akiwa hai.

Miguna alipokuwa mikononi mwa polisi hakuruhusiwa kuwasiliana na mawakilii wake, familia yake au mtu yeyote.

“Polisi walinidhalilisha kwa siku tano mfululizo huku wakiniweka katika mazingara maovu ambayo hakuna binadamu anafaa kuishi,” alisema.

Kufukuzwa kwake kulichochewa na amri ya mahakama kwamba, Serikali isitishe kesi zote zinazomkabili Miguna. Hata hivyo, idara ya upelelezi haikujali chochote zaidi ya kuharakisha hatua za kumfukuza nchini humo Miguna.

Huku Wakenya wakisubiri ikiwa Miguna atarejea, wabunge wa Bunge la Kitaifa kutoka mrengo wa Nasa wanaendelea kususia shughuli za Bunge.

Wabunge hawakushiriki kwenye zoezi la kuwahoji mawaziri wapya wakisema kamwe hawatambui Serikali ya Uhuru.

Ingawa walifanya hivyo, wabunge wa Jubilee hawakutishwa na wakaendelea kuwahoji na kupitisha majina yote ya mawaziri wateule. Mawaziri hao waliapishwa Februari 16.

Baada ya kuwahoji watu hao tisa walioteuliwa, wabunge hao wa Jubilee walikuwa na tashwishi kuhusu waziri mteule wa Michezo, Mohammed Achesa kwa sababu ya tabia yake ya kujihusisha na uhalifu.

Pia, walikuwa hawajaridhishwa na elimu yake. Achesa ana cheti cha Shahada cha Chuo Kikuu lakini hakuna anayefahamu jinsi alivyokipata. Habari za kuaminika zinasema kisomo chake kiliishia Darasa la Saba.

Lakini, Jubilee ambayo imemteua haina tatizo lolote na elimu yake; cha muhimu ni kwamba anatosha kuchapa kazi.

Wabunge wa upinzani licha ya kususia shughuli za Bunge, hawajasusia kupokea mishahara kila mwezi.

Je, ukisusia kitu, si ususie hadi malipo yanayoambatana nayo? Ya nini kujifanya ilhali unameza mate huko nyuma?

Na je, wabunge hao wataendelea kususia shughuli hizo hadi lini ilhali wanafaa kuwa wanawakilisha maazimio ya waliowachagua?

Hatua hii ya wabunge wa upinzani inaathiri vibaya maendeleo katika maeneo yao ya ubunge.

Wanafaa kufahamu kwamba, wanajidanganya kama wanafikiri kwamba uchaguzi mwingine utafanywa Agosti.

Hayo tisa, kumi ni kwamba nchi inasubiri kuona sinema itakayochezwa wakati Miguna atarejea nchini.