UCHAMBUZI: Kero ya watumishi kuishi nje ya vituo itatuliwe

Muktasari:

Katika agizo hilo, Serikali inashikilia msimamo kuwa watendaji wa mitaa na vijiji ndiyo wenye haki ya kumiliki mihuri kwa sababu ni waajiriwa na watendaji wa shughuli zote za kiserikali katika maeneo yao.

Mwishoni mwa mwaka jana, kulikuwa na mgogoro wa umiliki wa mihuri miongoni mwa watendaji wa umma. Ingawa kulikuwa na agizo la Ofisi ya Waziri Mkuu Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (Tamisemi) kuwataka wenyeviti hao kusalimisha mihuri yao kwa watendaji wa mitaa, bado suala hilo linafukuta chini kwa chini.

Katika agizo hilo, Serikali inashikilia msimamo kuwa watendaji wa mitaa na vijiji ndiyo wenye haki ya kumiliki mihuri kwa sababu ni waajiriwa na watendaji wa shughuli zote za kiserikali katika maeneo yao.

Ili kujibu hoja za wenyeviti kwamba watendaji hawako karibu wala hawashughulikii kwa wakati kero, changamoto na malalamiko ya wananchi kwa sababu asilimia kubwa wanaishi nje ya maeneo yao ya kazi, serikali iliagiza watendaji wote kuishi ndani ya maeneo yao.

Pamoja na watendaji wa mitaa na vijiji, kada nyingine inayokabiliwa na changamoto ya nyumba za kuishi maeneo yao ya kazi ni walimu wa shule za msingi na sekondari nchini.

Wapo baadhi ya walimu wanaolazimika kutembea zaidi ya kilometa tano kwenda na kurudi kazini kila siku kutokana na kukosa nyumba za kuishi shuleni au maeneo yaliyo jirani.

Kwa mfano, katika Wilaya ya Nyamagana walimu 1, 816, sawa na asilimia 96.6 ya wa shule za msingi za umma wanaishi nje ya vituo vyao vya kazi kutokana na kukosa nyumba. Wilaya hii inasadikiwa kuwa na upungufu wa nyumba 1, 376 za walimu.

Kwa mujibu wa Ofisa Elimu Msingi wa halmashauri hiyo, Claude Bulle ni walimu 64 pekee wenye nyumba za kuishi kwenye vituo vyao vya kazi.

Tatizo la nyumba za kuishi watumishi ni mtambuka kwa sababu hata baadhi ya watendaji wakuu katika baadhi ya halmashauri, hasa mpya bado wanaishi katika nyumba walizokuwa wakiishi kwenye halmashauri mama kabla ya mgawanyo. Mfano hai ni baadhi ya watendaji wa halmashauri ya Busega mkoani Simiyu ambao wanaishi katika Magu Mkoa wa Mwanza.

Akiwa ziarani mkoani Mwanza, Novemba mwaja jana, Makamu wa Rais, Samia Suluhu Hassan naye akabaini baadhi ya watendaji wa Wilaya ya Ilemela wanaoishi Nyamagana.

Licha ya kukemea na kuagiza wote wahamie na kuishi ndani ya halmashauri zao ili kutambua matatizo na changamoto zinazowakabili wananchi na kuyashughulikia kwa wakati, Makamu huyo pia aliuagiza uongozi wa halmashauri hiyo kuharakisha ukamilishaji wa ujenzi wa nyumba za watumishi. Hii ni mifano michache inayothibitisha changamoto ya nyumba za watumishi katika halmashauri jambo linalozorotesha huduma kwa wananchi.

Muda umefika kwa Serikali kuongeza kasi ya kujenga nyumba za watumishi katika maeneo yao. Kama ilivyofanyika katika utengenezaji wa madawati, na inavyoendelea kwenye ujenzi wa vyumba vya madarasa, nguvu hiyo ielekezwe kwenye kujenga nyumba za walimu pia.

Hii itasaidia kuboresha na kuinua viwango vya ufaulu kwa sababu walimu watapata muda mwingi wa kufanya maandalizi ya masomo kulinganisha na hali iliyopo sasa kwani wanapoteza muda mwingi kwenda na kurudi shule.

Mwalimu aliyechoka kwa kutembea na anayewaza umbali unaomsubiri kurejea nyumbani hawezi kutimiza vema wajibu wake katika kuwaandaa watoto darasani.

Naamini siyo walimu wala watendaji wa mitaa na vijiji wanaopenda kuishi nje ya vituo vyao vya kazi bali wanalazimika na, kwa hakika naamini suala hilo linawanyong’onyesha kiutendaji. Serikali na jamii itimize wajibu wa kuwawekea watumishi mazingira bora kiutendaji.

Ngollo John ni Mwandishi wa gazeti hili aliyepo mkoani Mwanza, anapatikana kupitia [email protected].