Kerr: Ninavisikia vishindo vya Kichuya huko

Muktasari:

  • Ni mambo manne tu ametaja kuhusu ligi zote mbili baada ya kuhudumu Tanzania kwa mwaka mmoja katika klabu cha Simba.

Kocha wa zamani wa Simba ambaye sasa anafundisha Gor Mahia, Mwingereza, Dylan Kerr amesema anapenda kufuatilia Ligi ya Kuu ya Tanzania na vile vile ligi za kote Barani Afrika.

Ni mambo manne tu ametaja kuhusu ligi zote mbili baada ya kuhudumu Tanzania kwa mwaka mmoja katika klabu cha Simba.

Wachezaji wa Kenya na Tanzania“Kuna baadhi ya wachezaji wazuri sana kwenye mazoezi kisha wanaogopa mechi na wanakuwa butu.

“Wakati wangu Simba kulikuwa na mchezaji anaitwa Sserunkuma (Danny) alikuwa hivyo. Wengi wa wachezaji wa Tanzania hawajitumi kama hapa Kenya.

“Nikikumbuka, wachezaji wengi ni wazembe, wapo wachache tu wanaojituma na kama nikipewa nafasi ya kusajili, naweza kumsajili Kichuya (Shiza).

Nimekuwa nikimsikia huyu Kichuya mara nyingi, anafanya mambo makubwa.

“Pia Okwi ninaambiwa anafunga sana, lakini kwangu siwezi kumpa nafasi

kikosi changu. Wakati wangu kulikuwa na akina Kiiza (Hamis) walikuwa wazuri sana lakini ninafikiri sasa hivi umri umekwenda unajua nataka wachezaji wenye nguvu ya kustahimili dakika zote 90.

“Nimetazama mechi kadhaa Ligi ya hapa Kenya ya KPL ninafikiri kuna vipaji. Wengi wao wanajituma sana ikilinganishwa na Tanzania haswa wakicheza dhidi ya Gor Mahia manake wanataka kuonyesha uwezo wao kwa timu kubwa.

“Tanzania ukweli hili halipo. Timu nyingi ndogo pamoja na wachezaji wao wengi wao wanaogopa timu kubwa haswa Simba na Yanga,” anasimulia Kerr katika mahojiano mafupi na Spoti Mikiki.

Kerr anasema kuwa hakudhani kama angepata fursa ya kufundisha soka Afrika Mashariki tena baada ya kuhudumu Simba kwa mwaka mmoja uliokosa mafanikio.

Baada ya kutoswa Simba, Kerr (50) alifanya mazungumzo na mwenyekiti wa klabu ya Gor Mahia, Ambrose Rachier siku chache baada ya kocha wa wakati huo, Mbrazili Jose Marcelo Ferreira ‘Ze Maria’ kujiuzulu na kuelekea klabu ya KF Tirana ya Albania.

“Kocha Iddi Salim aliniuliza iwapo ningetaka kazi ya Gor nikasema mbona freshi tu kama ipo basi niko tayari, akanijulisha kwa mwenyekiti na papo hapo nikatumiwa tiketi yangu kuja Kenya,” anasimulia

“Nilipewa mkataba wa miaka miwili, nikaambiwa huu ndo utakuwa mshahara wako na ndivyo nilivyoanza kazi Julai 10, 2016.”

Arudi Tanzania

Baada ya Kerr kuchukua timu, siku chache timu ikaja Dar es Salaam, Tanzania kuchuana na Everton ya Ligi Kuu ya England Julai 13 na kupoteza 2-1.

“Nilipendezwa na jinsi mashabiki wa Simba walinikaribisha Uwanja wa Taifa. Walifahamu kazi yangu japo sikupewa muda wa kukisuka kikosi kwa sababu ya uamuzi wa baadhi ya viongozi walinipiga fitna.

“Eti nilishindwa kunyakua ubingwa wa Mapinduzi ilhali tulikuwa nambari mbili kwenye ligi. Mkataba wangu mwanzoni ulikuwa na malengo ya kushinda ubingwa au nimalize nafasi tatu bora na tulikuwa tunacheza vizuri wakati huo.

“Unajua timu ikifanya vizuri halafu panaibukia mashindano fulani utakichezesha kikosi cha pili ili na wao wapate nafasi ya kuonyesha uwezo wao lakini kumbe hawakulipenda hili, walitaka kikosi cha Ligi

Kuu. hilo kama ni kocha mzuri unajitambua huwezi chezesha walewale.

“Baada ya nusu fainali tukaondolewa na mmoja wao aliniambia hajawahi

shuhudia mchezo mbovu wa Simba kama leo kisha Kaburu (Geofrey) naye akanisifia sana jinsi tulivyomakinika.

“Kumbe siku iliyofuata, akawaita waandishi wa habari kulalamikia kiwango cha timu na kocha wake, baadaye wakaniondoa kwenye timu,” anasema Kerr kwenye mahojiano ya moja kwa moja na Spoti Mikiki hotelini Lavington Mall.

Nilipokwenda Dar es Salaam kucheza na Gor Mahia: “Unajua walishtuka sana kuniona nimeingia na K’Ogalo na mimi huyo naiongoza dhidi ya Everton, mechi ambayo ilinifunza mengi haswa kukifahamu kikosi changu kipya.

“Sasa pale Tanzania, tulicheza soka nzuri, na ilinikumbusha wakati wangu nilipokuwa Simba. Lakini uongozi wa klabu ndiyo mbovu zaidi.

Akipewa nafasi Simba atarudi?

Kerr anagoma ikiwa italetwa ofa mezani.“Ikitokea nimepewa nafasi sasa hivi kurudi SDimba, hilo halipo, nimeshaifuta Simba labda nijiunge na Yanga, lakini sio Simba japo naipenda lakini kwa sababu ya uongozi wa sasa bado upo madarakani, siwezi.

“Simba wamenikataa, lakini kipindi kifupi Gor Mahia imebadilika na kwa upande wangu sasa hivi Kenya mambo mazuri, kama hivi unavyoona tumetwaa ubingwa, hii ni historia maishani kwangu, lazima niwashukuru wachezaji wangu.

“Mwenyekiti Rachier ni mtu nzuri sana. Hana mambo mengi yake ni kazi tu. Nilifurahi sana aliponipongeza wakati tulishinda Ulinzi Stars mjini Kericho kwenye mechi iliyotuhakikishia kombe na mechi nne mkononi,”

“Sasa ni kulenga kumaliza msimu kisha tuangalie mambo ya usajili ambapo tayari tumeshaanza mazungumzo na wachezaji kadhaa kutoka humu nchini na nje.

Muhimu mwakani ni kufanya kweli Ligi ya Mabingwa Afrika na pia kujaribu kutetea ubingwa. Mipango ipo kabambe sana, mtatushtuka,” anasema kocha huyo ambaye aliwahi kufanya kazi Mpumalanga Black Aces ya Sauzi na pia nchini Vietnam alisema.

Mchezaji anayemuhusudu

Kerr anasema beki wake Harun Shakava ni mtu ambaye ana uwezo wa kupiga soka hata Tanzania klabu moja kubwa lakini iwapo tu watatoa kitita cha Dola za Marekani 1 milioni.

“Huyu jamaa ni bonge moja la sentahafu, ni mzuri sana ambaye anaweza fedha nitawaachia tu.

Mara ya kwanza nilimtazama akifunga dhidi ya Yanga mechi za Kombe la Kagame mwaka 2015 nikapendezwa na kipaji chake, wakija na hiyo mihela nitawapa lakini najua hawawezi kufika bei, wale ni jamaa wa Dola 60,000 mwisho tu.”