Kibiga; kiungo anayebebwa na changamoto za soka

Muktasari:

  • Kiungo huyo, 21, katika mahojiano na Jarida la Spoti Mikiki anasema changamoto huwa zinamjenga ili kufikia malengo yake.

Moja ya viungo wanaochipukia kwa kasi msimu huu wa Ligi Kuu Tanzania Bara ni Yakubu Kibiga wa Majimaji ya Songea ambayo msimu uliopita ilinusurika kushuka daraja.

Kiungo huyo, 21, katika mahojiano na Jarida la Spoti Mikiki anasema changamoto huwa zinamjenga ili kufikia malengo yake.

“Nilikuwa mzee wa mechi za ndondo tu mitaani, hata Majimaji waliuona uwezo wangu kwenye mashindano hayo, mbali na Majimaji ambayo naichezea pia wakati ninasoma niliwahi kuichezea, Ashanti United ya Ilala.

“Wanasoka wengi hasa ambao tunatokea mitaani,tunakutana na changamoto nyingi sana, moja ya changamoto hizo ni nafasi, unaweza kuwa na uwezo mzuri lakini usipate timu ya kuichezea.

“Binafsi changamoto za namna hiyo zilikuwa zinanifanya kucheza kwa juhudi zaidi, popote pale ili niwe na ushawishi wa uwezo, ukifanya kuliko kawaida, hawawezi kukuacha,” anasema kiungo huyo.

Kibiga ameonyesha kuvutiwa mno na uchezaji wa kiungo wa Ruvu Shooting, Shaaban Kisiga na kusema wakati anakua kisoka alitamani siku moja kucheza soka kama analocheza kiungo huyo mkongwe. “Yule jamaa unaweza ukasema ni kijana, uwezo wake bado unamruhudu kucheza soka la ushindani,” anasema Kibiga ambaye kidunia nzima anamhusudu, Bastian Schweinsteiger wa Chicago Fire.

Nyota huyo wa Majimaji pia amesema hana neno juu ya kuzichezea Simba na Yanga kikumbwa ni wao kutekeleza mahitaji yake muhimu ambayo atayahitaji.

“Kila siku huwa nawaza namna ya kupiga hatua zaidi, ukweli haufichiki kuwa wachezaji wengi wanaweza kucheza Simba,Yanga na Azam kwa sababu ni timu kubwa.

“Ndoto zangu ni kucheza nje ya nchi lakini ikitokea moja ya timu hizo wamenihitaji, mbali na yote nitakuwa tayari kutumia nafasi hiyo kama njia, hizo ni timu ambazo zinacheza mashindano ya kimataifa.

“Nachojua mashindano ya kimataifa yanaweza kuwa fursa kwa mchezaji kujitangaza,” anasema mchezaji huyo ambaye alianza kucheza soka la utotoni kwenye timu ya Shababiy ya Kigamboni.