Kiboko ya mashabiki wenye viherehere

Dondoo:

Yvonne ndiye staa katika wimbo African Queen uliomtambulisha mwanamuziki wa Nigeria, 2 Face Idibia

Alizaliwa Agosti 25, 1983 nchini Nigeria

Alipokuwa mtoto alitamani kuwa mwanamitindo lakini ndoto hiyo iliyeyuka baada ya kukutana na Charles Nobia aliyemwingiza katika ulimwengu wa filamu.

Muktasari:

Wapo mashabiki wanaotoa maoni ya kuwajenga mastaa anaowafuatilia, wengine hutoa maneno ya kejeli za kila namna.

Mitandao ya kijamii huwapa wakati mgumu mastaa wanaoogopa kukosolewa. Ukisoma maoni katika posti za mastaa unaweza kucheka na kulia kwa wakati mmoja.

Wapo mashabiki wanaotoa maoni ya kuwajenga mastaa anaowafuatilia, wengine hutoa maneno ya kejeli za kila namna.

Waathirika wa vitendo hivi huchukua hatua ya kuwafungia mashabiki wao wasione taarifa hizi, hata hivyo huwa siyo dawa kwani wengine hufungua akaunti kwa majina mengine na kuendeleza tabia ya kutoa maneno ya kejeli na wakati mwingine matusi ya nguoni.

Lakini mwigizaji wa Nigeria, Yvonne Jegede ndiye kiboko ya mashabiki wa aina hii kwani kila wanapoaandika maneno ya kejeli huwajibu papo kwa papo.

Mara kadhaa ameingia katika mgogoro na mashabiki wake pale alipowajibu ‘utumbo’ kwa kipimo kilekile bila kujali ukubwa wa jina lake.

Kwa mfano hivi majuzi alipoweka video katika mtandao wa instagram na kubezwa kuwa anaonyesha matiti yasiyo na mvuto.

Staa huyo alimjibu shabiki huyo akihoji kama ana ubongo au la! “Umeacha wapi ubongo wako? Kama huna ubongo ni bora upite bila kuandika chochote katika posti zangu.”

Shabiki mwingine aliandika: “Funika matiti yako hayana mvuto”. Naye hakuna na subira alimjibu shabiki huyo akimtaka aende hospitali kutibiwa akili na siyo katika ukurasa wake wa Instagram kwa kuwa siyo hospitali.

Suala la mwigizaji huyo kuacha matiti yake nje limeongolewa kwa miaka mingi, lakini Yvonne anasema asilaumiwe kwa kuwa yeye siyo fundi nguo.

“Mimi nina matiti makubwa, kuna wakati yanatoka nje ya nguo sasa hapo nilaumiwe kwa sababu gani wakati mimi sijaitengeneza?” anahoji Yvonne.

Mwigizaji huyo ambaye ana shahada ya kwanza ya uhusiano wa kimataifa anasema umaarufu haujawahi kumsumbua hasa kwa kuwahofia mashabiki wanaomzodoa.

Anasema waigizaji wengi wameshindwa kuchanua kutokana na kuwahofia mashabiki wao na kujikuta wakifanya mambo ambayo yanawatoa kwenye mstari.

“Mimi siwezi kuacha kumjibu shabiki, iwe mtandaoni hata katika maisha ya kawaida, nitahakikisha analala na dozi kutoka kwangu, mashabiki ni watu wanaotujenga na kutuangusha lakini mimi hawaniwezi,” anasema.

Anasema wapo waandishi ambao hutumia picha zake na kutengeneza stori huku wakigeuza maneno kumfanya aonekane mtu wa ovyo.

“Mwandishi kama huyu huwa nampuuzia na kumuona hajui maadili ya kazi yake, mtu anapoamua kuweka picha katika mtandao maana yake ameridhika ionekane, sasa anapoigeuza kuwa stori ya ajabu huwa nampuuza,” anasema.

Hata hivyo, anasema pamoja na kuwa huwa ana wajibu mashabiki wanoko, kuwaheshimu wale wanaonunua kazi zake na kumpa mchango mzuri wa mawazo katika mitandao ya kijamii.

“Huwa ninachukua mawazo mazuri kutoka kwa mashabiki wangu na kuyafanyia kazi, ninafurahi pale wanapochangia vitu vya maana,” anafafanua.