Kifungashio hakitunzi tu bidhaa, kinavutia wateja pia

Muktasari:

Si hayo tu, kifungashio hurahisisha usafirisha wa bidhaa husika na kinatoa maelezo ya bidhaa kwa mteja. Mteja wa mara ya kwanza anapata taarifa zote muhimu kuhusu bidhaa kutoka kwenye kifungashio.

        Kifungashio ni kitu kinachotengenezwa kwa ajiri ya kuhifadhi bidhaa. Kinafanya kazi ya kuhifadhi na kuilinda bidhaa isiharibike kwa urahisi.

Si hayo tu, kifungashio hurahisisha usafirisha wa bidhaa husika na kinatoa maelezo ya bidhaa kwa mteja. Mteja wa mara ya kwanza anapata taarifa zote muhimu kuhusu bidhaa kutoka kwenye kifungashio.

Kifungashio kinaeleza bidhaa zilizotumika katika utengenezaji wa bidhaa husika, hutoa tahadhari kama kuna madhara kwa baadhi ya watu kuitumia mfano wajawazito, watoto au wagonjwa.

Kifungashio hueleza lini bidhaa ilitengenezwa na muda ambao inapaswa kutumika. Mteja anaweza kufahamu kama bidhaa imeisha muda wake wa matumizi kwa kuangalia tarehe zilizomokwenye kifungashio chake. Hata wasambazaji na wauzaji wanafahamu na kupanga ipi iuzwe kwanza na ipi ifuate kutokana na taarifa hizo.

Kitu muhimu zaidi kwa mzalishaji ambacho kifungashio kinafanya ni kumvutia mnunuaji ambaye huamini ubora wa bidhaa iliyomo ndani ya kifungashio. Wapo watu wanaoshawishika kununua bidhaa kutokana na muonekano wa kifungashio. Wanaweza kuinunua hata kama hawaifahamu.

Baadhi ya wateja hawawezi kununua bidhaa kutokana na uduni wa vifungashio vyao hivyo ni muhimu kwa kila mjasiriamali kuangalia jinsi anavyoweza kuboresha eneo hili ili kuwa na uhakika wa soko.

Ukubwa na aina ya kifungashio inategemea aina ya bidhaa na hali ya soko kwa maana ya uelewa wa wateja waliolengwa. Zipo faida za kuwa na vifungashio kwa kila bidhaa.

Kwanza ni kuikinga bidhaa isiharibike kutokana na sababu tofauti zinazoweza kuchangia hilo. Bidhaa inapozalishwa husafirishwa kwenda kwa mlaji na barabarani au namna nyingine yoyote ya usafiri unaotumika hukutana na mitikisiko mingi ambayo bidhaa ikikosa kifungashio itaharibika kwa urahisi.

Pia inapokaa katika shelfu za maduka inakingwa na vumbi ama chochote kinachoweza kuidhuru bidhaa na kuifanya itumike wakati wowote itakapohitajika au kununuliwa.

Vilevile kifungashio kikitengenezwa katika muonekano mzuri humvutia mteja kuiangalia hatimaye kuinunua kwa urahisi bidhaa. Hivyo mjasiriamali anatakiwa kutengeneza vifungashio vyenye mvuto wa rangi na dizaini nzuri.

Kama nilivyosema awali, vifungashio makini vinapaswa kuwa na maelezo ya bidhaa ambayo huweza kumshawishi mteja kuinunua bidhaa bila ugumu. Maelezo hayo ni kama muda wa matumizi ya bidhaa, jinsi ya kuitumia, jinsi ya kuibeba pamoja na alama za uthibitisho wa viwango.

Kifungashio huweza kubadili uamuzi wa mteja. Maelezo yaliyopo katika kifungashio yanasaidia mteja kufanya uamuzi wa ununuzi wa bidhaa bila kuwa na maswali mengi kwa muuzaji.

Muuzaji huraisishiwa kazi ya kumfanya mteja anunue bidhaa. Maelezao ya malighafi iliyotumika kutengeneza bidhaa huandikwa katika kifungashio na kumshawishi mteja kuinunua bidhaa kama inaendana na matakwa yake.

Vifungashio hutumika kutofautisha bidhaa kutokana na rangi, alama ya biashara ama muundo ulotumika kutengeneza kifungashio husika. Hali hii humsaidia mteja kutofautisha bidhaa mbalimbali katika dukani au sokoni.

Mjasiriamali anatakiwa kutafuta na kupata elimu ya biashara ili awe na uwezo wa kuchambua na kutathmini mwenendo wa biashara yake.

Elimu itamsaidia kujiamini na kutambua fursa kwa uhakika. Itakuwa vigumu kudanganywa na matapeli ama wababaishaji wa mitaani. Elimu ni sifa muhimu kwa mjasiriamali. Elimu hufungua na hutanua akili ili iwe na upeo wa juu wa kufikiri na kutafakari.

Kifungashio kizuri kinategemea ubunifu wa mjasiriamali husika kubuni na kurekebisha muonekano.