Kiingereza kinavyowatesa Watanzania nchini kwao

Muktasari:

Aidha, lugha za kigeni zinazotumika Tanzania ni asilimia ndogo ya Watanzania wanaozijua lugha hizo na kuzimudu katika matumizi.

Kwa sababu hiyo, lugha ya kigeni inapotumika, hapana budi kuwapo kwa ukalimani au ufasiri.

Kiswahili ni lugha ya Taifa na lugha rasmi nchini Tanzania. Wananchi wengi takriban asilimia 90 wanakijua Kiswahili.

Aidha, lugha za kigeni zinazotumika Tanzania ni asilimia ndogo ya Watanzania wanaozijua lugha hizo na kuzimudu katika matumizi.

Kwa sababu hiyo, lugha ya kigeni inapotumika, hapana budi kuwapo kwa ukalimani au ufasiri.

Kwa kuwa kundi kubwa la Watanzania wanakijua Kiswahili na kwamba ndiyo lugha yao ya mawasiliano popote wanapokuwapo, hapana budi taasisi zinazohusika katika utoaji wa huduma za kijamii kulizingatia hilo mawasiliano yanapofanyika.

Ili huduma ziweze kuwa na ufanisi, mawasiliano bora hayana budi kupewa kipaumbele. Ikiwa Mtanzania ambaye hajui lugha ya kigeni anawekewa tangazo linalomhusu kwa lugha asiyoifahamu, tangazo hilo haliwezi kuwa na tija kwake.

Kwa kuwa lengo ni kumfikishia ujumbe Mtanzania anayekijua Kiswahili, basi lugha yake ya Kiswahili ndiyo hasa lugha faafu katika mazingira hayo.

Katika baadhi ya ofisi, vyoo, vituo vya mabasi na sehemu nyinginezo; ni jambo la kustaajabisha kuona vibao vya maelekezo vimeandikwa kwa kutumia lugha ya Kiingereza bila ufasiri wowote.

Kwa Mswahili anayeijua lugha ya Kiingereza, hawezi kupata changamoto katika muktadha huo lakini kwa yule anayekijua Kiswahili pekee, ni vigumu kuelewa maelekezo ya namna hiyo na hivyo hupatwa na mkanganyiko.

Fikiria kwa mfano umekwenda nchini China, umeshuka katika uwanja wa ndege. Umebanwa na haja. Kila unapozunguka iwe milangoni na pahali pengine, maelekezo yote ni kwa Kichina. Bila shaka mtu mzima unaweza kuadhirika kirahisi.

Ikumbukwe kwamba kanuni ya utoaji maelekezo katika sehemu zitoazo huduma za kijamii, inaitaka mamlaka husika kulipa kipaumbele kundi kubwa linalotumia huduma hizo.

Katika muktadha huo, maelekezo katika nchi yetu katika sehemu tajwa hayana budi kuwa kwanza katika lugha ya Kiswahili yakifuatiwa na lugha za kigeni zinazotumika zaidi.

Hapa kwetu Kiingereza ni lugha ya kigeni ambayo wageni wengi huitumia. Kwa hivyo, mabango na maelekezo mengine yanapaswa kuzingatia kanuni hiyo. Kutumia lugha ya kigeni pekee si kuwatendea haki watumiaji wa Kiswahili.

Ofisa wa Benki ya Dunia Yonas Mchomvu katika mahojiano na wanafunzi wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam na Chuo Kikuu cha Humboldt (Ujerumani) waliotaka kujua zaidi kuhusu huduma za mabasi ya mwendokasi, anaeleza kwamba kutoa maelekezo katika huduma za kijamii kwa lugha inayofahamika kwa watu wachache ni kosa kubwa.

Anasimulia kuwa alishangaa kuona kioja huko Korogwe ambako katika kituo kizuri cha mabasi kilichojengwa na kuzinduliwa hivi karibuni, maelekezo yote katika mababgo yametolewa katika lugha ya Kiingereza. Aliona ni jambo la kushangaza kwa kuwa watumiaji wakubwa wa kituo hicho ni wazawa ambao katika mawasiliano yao hutumia Kiswahili zaidi kila siku.

Anaongeza kuwa, kwa kigezo cha kuzingatia watumiaji, mamlaka husika ilipaswa kutoa maelekezo kwa Kiswahili kisha yafuatiwe na maandishi madogo ya ufasiri katika lugha ya Kiingereza.

Anasema kwamba hilo ni tatizo kubwa katika nchi yetu, kwa kuwa katika utoaji wa maelekezo ya namna hiyo, mamlaka husika hazizingatii utaratibu unaotakiwa.

Mamlaka husika hazina budi kuwa makini katika utoaji wa maelekezo katika huduma za kijamii.

Ikumbukwe katika kufanya hivyo walengwa wawe kundi kubwa la watumiaji wa huduma husika.