Kilio cha shule ya msingi Pongwe

Sehemu ya wanafaunzi wenye mahitaji maalumu katika Shule ya Msingi Pongwe iliyopo mkoani Tanga. Wanafunzi hawa pamoja na mambo mengine wanakabiliwa na changamoto ya uhaba wa chakula. Picha na Constantine Akitanda

Muktasari:

Shule hii iliyoanzishwa 1959 ikipokea wanafunzi wa darasa la tano hadi la nane, iko takribani kilomita 15 nje ya jiji hilo

       Shule ya msingi Pongwe iliyoko katika kata ya Pongwe ndani ya jiji la Tanga ni miongoni mwa shule chache nchini zinazotoa huduma kwa wanafunzi wenye mahitaji maalumu.

Shule hii iliyoanzishwa 1959 ikipokea wanafunzi wa darasa la tano hadi la nane, iko takribani kilomita 15 nje ya jiji hilo

Mwaka 1968, shule ilianzisha rasmi kitengo cha watu wenye ulemavu wa macho na ilipofika mwaka 2009 kitengo cha watu wenye ulemavu wa ngozi nacho kikaanzishwa na Serikali. Hii ilitokana na matukio kadhaa ya mashambulizi dhidi ya watu wenye ulemavu wa ngozi.

Shule ikapewa jukumu la kupokea wanafunzi wenye ulemavu wa ngozi kutoka mikoa mbalimbali ya Tanzania, uamuzi huu ulifanynywa na Serikali kutokana na ukweli kwamba wenye ulemavu wa ngozi pia wanakabiliwa pia na tatizo la uoni hafifu.

Mwalimu Mkuu wa shule hiyo Yahya Mafita anasema kuendesha shule hiyo si jambo la mchezo, changamoto ni nyingi na ruzuku ya Serikali haitoshelezi katika kukabiliana na mambo mbalimbali ikiwemo upatikanaji wa chakula cha watoto wenye mahitaji maalumu shuleni hapo.

Anasema, Serikali iliamua kwa makusudi kuifanya Pongwe kuwa eneo maalumu na la kupigiwa mfano katika utoaji wa elimu kwa wanafunzi wenye mahitaji maalumu, lakini lengo hilo limegubikwa na changamoto.

Mojawapo ya changamoto hizo ni uhaba wa fedha kugharimia chakula kama anavyoeleza: “Chakula cha wanafunzi pekee kwa mwezi ni takribani Sh6 milioni, sisi tunapokea Sh3 milioni, hii ni changamoto kubwa ukizingatia kuwa hii ni shule maalumu na ina wanafunzi 79 wenye mahitaji maalumu wanaoishi hapa shuleni.”

‘’Elimu bila malipo ni jambo jema, lakini ni muhimu ruzuku ya Serikali iendane na uhalisia wa mahitaji ya kila shule. Ikumbukwe kwamba Shule ya Msingi Pongwe haihudumii wanafunzi wenye mahitaji maalumu pekee kutoka sehemu mbalimbali za nchi, bali pia hutumiwa na wanafunzi wenyeji wa eneo hili la Pongwe,’’ anaeleza.

Changamoto nyingine ni uhaba wa vyumba vya madarasa. Uhaba huu umesababisha darasa moja kuchukua wanafunzi hadi 120, hali inayosababisha wanafunzi kusongamana, lakini pia mwalimu kukosa udhibiti wa kutosha kwa wanafunzi na hasa namna bora ya kuwafundisha na kuwasimamia.

Kimsingi, idadi ya wanafunzi 120 kwa darasa inakinzana na sera ya elimu na miongozo mbalimbali inayotaka chumba kimoja cha kufundishia wanafunzi kisizidi idadi ya wanafunzi 40. Lakini hili limekuwa kinyume katika shule hii yenye mahitaji maalumu.

Mwanafunzi Marieta John mwenye ulemavu wa ngozi, anasema wanahitaji ulinzi wa kutosha katika jamii hasa kwa kuzingatia kuwa uzio uliokamilika, jambo linaloweza kusababisha wanafunzi wenye ulemavu wa ngozi kufanyiwa ukatili.

Shule haina uzio, uliopo umejengwa upande wa mbele pekee, eneo lote la nyuma ya shule liko wazi na huko ndiko kwenye pori, usalama wetu uko wapi? Kupafanya Pongwe kuwa shule yenye mahitaji maalumu lilikuwa ni jambo jema, lakini kuacha miundombinu ikiwa nusu ni hatari, tunaomba tusaidiwe kwa hili, anasema Marietha.

Ofisa elimumsingi wa jiji la Tanga, Khalifa Shemahonge anakiri kuzitambua changamoto za Pongwe na kwamba mahitaji ya wanafunzi maalumu kwa kawaida huwa ni gharama.

‘’Ni lazima Serikali tushirikiane na wadau wengine katika kusaidia kupunguza kama siyo kuzimaliza changamoto, ili tuweze kuwahudumia wanafunzi wetu. Tuwachangie watoto wenye mahitaji maalumu kwa kuwa watoto ni sehemu ya jamii, ’’anasema

CDTF yainusuru shule ya Pongwe

Mwalimu Mafita anatoa pongezi kwa taasisi ya ya Community Development Trust Fund (CDTF) ambayo ni miongoni mwa taasisi za kijamii iliyosikia kilio na kuitikia kwa haraka kutatua kero ya vyumba vya kulala wanafunzi wenye mahitaji maalumu sambamba na kutafuta gari.

‘’Gari hili sasa limerahisisha huduma kwa wanafunzi hasa kunapotokea suala la ugonjwa,’’ anaeleza.

CDTF ni moja ya mashirika yanayokusudia kuacha alama kwenye shule ya wanafunzi wenye mahitaji maalumu, ambapo baada ya kusikia kilio cha uongozi wa shule hiyo kupitia maombi maalumu, shirika likajielekeza kujionea uhalisia na kisha kuanza kutafuta fedha ili kuwa sehemu ya utatuzi wa changamoto badala ya kuiachia Serikali pekee.

Mkurugenzi Mkuu wa CDTF Henry Mgingi anasema taasisi yake imebaini mahitaji kadhaa katika shule ya Pongwe, lakini imefanikiwa kuyatatua machache, miongoni mwa changamoto zilizopewa ufumbuzi ni pamoja na ununuzi wa gari moja kwa kushirikiana na Emirate Foundation

Ukiondoa kuwapatia wanafunzi bima ya afya, CDTF pia imefanikiwa kujenga nyumba ya kulala wanafunzi hao yenye uwezo wa kubeba zaidi ya wanafunzi 78 ambayo imegharimu jumla ya Sh98 milioni na kwamba jengo hilo la kisasa linatarajiwa kukabibiwa serikalini mwishoni mwa Novemba 2017.

‘’ Jamii na wadau wengine wote wakumbuke majukumu yao ya msingi katika kuwahudumia watoto wenye mahitaji maalumu, kwa kuwa jamii ndiyo chombo kikubwa cha kujenga misingi ya kuwajenga watoto wetu,’’ anashauri.