Kinachoweza kuviokoa vyama vya upinzani Tanzania

Rais Jakaya Mrisho Kikwete akizungumza na Wajumbe wa Kituo cha Demokrasia Tanzania (TCD) alipokutana nao Ikulu ndogo  mjini Dodoma ,wakati huo akiwa bado madarakani kuzungumzia mustakabali wa kupatikana Katiba Mpya. Picha ya maktaba.

Muktasari:

  • Hata hivyo, mara baada ya uchaguzi huo kukamilika na Serikali kuingia madarakani matukio kadhaa yalijitokeza katika medani za siasa za nchi ikiwamo kupigwa marufuku matangazo ya moja kwa moja ya vikao vya Bunge, lakini pia kupigwa marufuku shughuli za kisiasa za majukwaani.

Mwaka 2015 Tanzania ilifanya Uchaguzi Mkuu ulioiweka madarakani Serikali ya Awamu ya Tano chini ya Rais John Magufuli baada ya kuibuka kidedea na kuwabwaga wapinzani wake akiwamo Waziri Mkuu wa zamani, Edward Lowassa aliyekuwa akigombea nafasi hiyo kupitia Chadema.

Hata hivyo, mara baada ya uchaguzi huo kukamilika na Serikali kuingia madarakani matukio kadhaa yalijitokeza katika medani za siasa za nchi ikiwamo kupigwa marufuku matangazo ya moja kwa moja ya vikao vya Bunge, lakini pia kupigwa marufuku shughuli za kisiasa za majukwaani.

Aidha, imeshuhudiwa matukio mbalimbali ya kukamatwa kwa wapinzani kwa sababu mbalimbali zikiwamo kuhutubia katika mikutano, lakini pia kuhusishwa na madai ya uchochezi.

Mpaka sasa wapinzani kadhaa wamefikishwa katika vituo mbalimbali vya polisi, kufunguliwa mashtaka huku wengine wakihukumiwa vifungo jela.

Mbunge wa Mbeya mjini, (Chadema) Joseph Mbilinyi maarufu kama ‘Sugu’ ni miongoni mwa mpinzani aliyekumbwa na kadhia hiyo baada ya Mahakama ya Hakimu Mkazi Mbeya kumuhukumu kifungo cha miezi mitano jela baada ya kutiwa hatiani kwa kosa la kutumia lugha ya fedheha dhidi ya Rais John Magufuli

Sugu anatumikia kifungo hicho sambamba na Katibu wa Chadema Kanda ya Nyanda za Juu Kusini, Emmanuel Masonga ambaye walishtakiwa pamoja.

Jinsi inavyopaswa kuwa

Mfumo wa vyama vingi ni hali ya kuwa na chama zaidi ya kimoja, katika nchi moja huku madhumuni yake makuu ni kuleta ushindani wa kisiasa ili kuleta maendeleo ya nchi.

Kutokana na ukweli huo ni wazi kwamba upinzani wa kisiasa siyo uadui kama watu wengi kwenye nchi zinazoendelea wanavyodhani, badala yake kuwa na vyama vingi ni kuongeza wigo wa demokrasia katika jamii husika.

Tanzania ni kama ilivyo kwa nchi nyingine zinazo endelea ina mfumo wa vyama vingi vya siasa uliorejeshwa katika Katiba ya Tanzania mwaka 1992. Wakati wa Uchaguzi Mkuu wa 2015 Ofisi ya Msajili wa Vyama vya Siasa nchini ilitaja vyama 22 ambavyo vilitakiwa kushiriki uchaguzi huo.

Tofauti na chaguzi nyingine mwaka 2015 upinzani ulionekana kupata nguvu kutokana na matokeo yake kufika kura zaidi ya 600,000 baada ya mgombea kupitia Ukawa Edward Lowassa kushika nafasi ya pili, kura ambazo hazikuwahi kufikiwa na mgombea yoyote kutoka upinzani.

Matokeo ya uchaguzi huo angalau yalitoa matumaini kwamba upinzani umepata nguvu. Mara baada ya uchaguzi huo kukamilika vyama vya upinzani vilianzisha harakati mbalimbali ikiwamo kufanya mikutano, kuanzisha operesheni kadhaa kama Sangara na nyinginezo.

Wapinzani pia waliweza kujinasibu kupitia matangazo ya moja kwa moja ya Bunge ambako walikuwa wakishindana kwa hoja ama na Serikali au na wabunge wa chama tawala.

Lakini, hali hiyo ilibadilika baada ya Serikali kupiga marufuku mambo kadhaa ikiwamo kuonyesha Bunge moja kwa moja lakini pia kufanya mikutano ya kampeni hadi 2020 kipindi ambacho Tanzania itaingia katika uchaguzi mwingine.

Kutokana na hali hiyo ni wazi sasa wapinzani wamejikuta katika wakati mgumu pengine kuliko vipindi vilivyopita hii inatokana na ukweli kwamba wanashindwa kufanya mambo yanayohusu siasa.

Mara kwa mara wapinzani wamejikuta wakikamatwa au kuzuiwa na Jeshi la Polisi kufanya mikutano ya nje na wengine kufikishwa mahakamani wakituhumiwa kutoa lugha ya matusi.

Wanavyoweza kufanya siasa?

Katibu Mkuu wa Chadema Dk Vincent Mashinji anasema kuwa wao kama vyama vya upinzani hawajakata tamaa na kwamba wataendelea kufuatilia kila kinachofanywa na Serikali na kukikosoa kwa hoja zenye nguvu siyo nguvu ya hoja.

Kuhusu kuzuiwa kwa matangazo ya moja kwa moja ya Bunge, Dk Mashinji anasema hatua hiyo haiwezi kuwarudisha nyuma na badala yake vyama vya upinzani vinapaswa kuvichukulia vikao hivyo

kuwa ni zaidi ya kampeni za uchaguzi kwa kusababisha vinakuja na mkakati madhubuti jinsi ya kushirikiana na kukabili hoja za chama tawala.

“Sasa ni muda wa kujipambanua kwa njia zote, kuzungumza na wananchi kupitia vyombo vya habari ili maoni ya wapinzani nayo yasikike. Kwa njia hii ndiyo tunaweza kubaki salama lakini pia ujumbe wetu kufika bila matatizo,” anasisitiza

Vile vile Dk Mashinji anaongeza kuwa jambo lingine ni kutumia ipasavyo fursa ya kampeni za chaguzi ndogo kwa lengo la kupeleka ujumbe kwa wananchi.

“Unaweza usishinde katika chaguzi hizo kwa sababu tu chama tawala kimeamua kutumia nguvu na kubadili ukweli lakini ukishiriki ipasavyo na kunadi sera zako wananchi wataelewa na wao wenyewe kuamua.”

“Ninachoweza kusema tu haya mambo yana mwisho, hivyo wasifikiri siku zote wananchi watakuwa wajinga na kukubali kila jambo ipo siku watasema imetosha,” anasisitiza Dk Mashinji.

Dk Mashinji anasema pia kwa sasa njia nzuri kwao ni kuanika mambo mabaya yote yanayofanywa na utawala kwa lengo la kuwashtaki ili wananchi waamue wenyewe.

“Siasa lazima ziendelee hata watumie mabavu kiasi gani. Siasa huwezi acha maana ndiyo zinazotuongoza katika mfumo wa kupata viongozi ina maana tukiacha maana yake ni kwamba tumeamua kutofanya demokrasia, huo ni uongo sisi siyo wakimbizi hatuwezi ishi hivyo,” anasisitiza.

Anasema kwa upande wa chama chake wameshaliona hilo na mara kwa mara kiliamua kuasisi mipango mbalimbali kama maandamano yaliyopewa jina la Ukuta ingawa baadaye ilipata busara kutoka kwa viongozi wa dini na kuachana na mpango huo.

“Tulitangaza kampeni ya Nzengo na kampeni nyingine lukuki lengo ikiwa ni kuwafikia watu kutoka chini katika jumuiya zao. Zimeonyesha zina mafanikio makubwa, wanachama wetu wameshiriki katika misiba na sherehe pamoja na wananchi.”

Hata hivyo, Dk Mashinji anasema kampeni hizo zilianza kuingiliwa na Jeshi la Polisi na kuanza kuwakamata kwa kisingizio cha kuvunja amani jambo ambalo ni uongo na badala yake akadai kuwa lengo lao lilikuwa ni kuwadhoofisha.

“Tunahitaji mabadiliko hali ilipofika sasa ni mbaya, viongozi wa dini wanakamatwa, waandishi wanapotea na wanasiasa kila kukicha tunakamatwa hili si la kulipuuzia ni lazima tuache woga tuendeleze siasa ipo siku watu wataelewa tu.”

Dk Mashinji anatoa wito kwa vyama vya upinzani vyote kuunganisha nguvu ili kupambana na hali ilivyo sasa.

“Adui sasa ni mmoja, hakuna sababu ya kutafuta shujaa badala yake tunapaswa kuwa kitu kimoja kama kweli tunataka kuvuka katika kipindi kilichopo na hiyo ndiyo itakuwa jambo la msingi sana kwetu badala ya kila mmoja kuona ni mpinzani wa mwenzake,” anasema.

Dk Mashinji anasema kuwa jambo lingine ni kwa wanachama wao kutotishika na badala yake waendelee kufanya programu zao za chama bila woga kwani hakuna sheria yoyote ambayo wanaivunja.

Kwa upande wake Katibu Mkuu wa NCCR- Mageuzi Juju Danda anasema kwa sasa tayari kuna tatizo la kufanya siasa nchini ingawa ukweli ni kwamba tafsiri ya siasa pamoja na mambo mengine ni kufanya mikutano ya hadhara na maandamano.

“Kutokana na ukweli huo ni wakati sasa vyama vya upinzani vikabadili ‘approach’ na kuchagua ‘soft approach’. Hakuna haja ya kupambana na dola kwani mwisho wa siku watakaoumia ni wananchi.”

Anazitaja njia hizo kuwa ni pamoja na kwenda mahakamani kudai na kuhoji haki hiyo ya kikatiba; “Mahakama yenyewe ndiyo itaamua kwani bahati nzuri ni muhimili unaoheshimika na pande zote.”

Anasema njia nyingine ni kutumia chombo cha Kituo cha Demokrasia Tanzania (TCD) kwani kila mwakilishi wa pande zote ikiwamo chama tawala cha CCM inakitambua hivyo kwa kutumia jukwa hilo ujumbe utafika.

Njia nyingine anasema ni kutumia Baraza la Vyama vya Siasa kujadiliana na kuhakikisha ujumbe wao unawafikia watawala.

“Unajua kazi kubwa ya baraza hili pamoja na mambo mengine ni kuishauri na kuikumbusha Serikali wajibu wake hivyo mlango huo ni sahihi kwetu kuupitia.

Hata hivyo, Danda anasema kuwa anatambua kuna changamoto kadhaa katika baraza hilo ikiwamo viongozi wakuu kutohudhuria lakini hilo bado linaweza kuzungumzika na hatimaye kufikia malengo.

Anataja njia nyingine ni kwa wapinzani wenyewe kutafakari kwa pamoja na kuungana ili kuongeza nguvu za mapambano.

“Unaweza kuona kwamba sasa wapinzani hatuwi kitu kimoja katika masuala ya msingi lakini ukweli ni kwamba lazima tubadilike, tufikiri kwa pamoja badala ya kila mmoja kutumia njia yake.”

“Mara kwa mara nimekuwa nikikutana na wadau mbalimbali wakiwamo mabalozi wanaoziwakilisha nchi zao hapa nchini, wamekuwa wakitushauri mambo mengi lakini kubwa ni jinsi gani tutatumia njia rahisi na salama ikiwamo mazungumzo. Naungana nao kwani njia zilizo zoeleka kama maandamano zinapaswa kupimwa kwanza ili kuona kama yana manufaa au la isije ukasababisha maafa.”

Naibu Katibu wa Zanzibar (CUF) Nassor Ahmed Mazrui yeye anasema kuwa kwa sasa kufanya siasa Tanzania imekuwa vigumu kuliko kipindi chochote cha utawala.

“Huwezi kuishi bila kupumua kila mwanadamu anapopata joto ni lazima awe na pakupumulia lakini sasa Tanzania wapinzani hatuna pa kupumulia. Asante Mungu, wanasiasa nchini wanatumia njia ya diplomasia sana kama ingekuwa kama nchi nyingine leo hii tungekuwa tunaongea tofauti,” anasisitiza.

Hata hivyo, Naibu Katibu huyo ambaye ni mfuasi wa upande unaomuunga mkono Maalim Seif Sharif Hamad anaonya endapo hali hiyo itaendelea itakuwa mbaya sana kwani watu watakosa uvumilivu jambo litakalo changia kutoweka kwa amani.

Mazurui anataja mambo kadhaa ambayo kwa mtazamo wake anaamini yanaweza kusaidia wapinzani kufanya shughuli zao bila kuathiri chochote kuwa ni pamoja na kutumia vyombo vya habari.

“Vyombo vya habari vinawajibu wa kusema ukweli, vionyeshe ubaya na uzuri wa utawala na kwa kufanya hivyo na wapinzani kuvitumia ipasavyo itasaidia kubadilisha mtazamo ulipo.

Anataja jambo lingine ni kutumia taasisi za kimataifa ili kushawishi utawala uliopo kuona umuhimu wa kukutana na wapinzani ili kupata suluhu ya masuala hayo.

“Hapa pengine jumuiya hizi zitashinikiza utawala kuona umuhimu wa pande zote kukaa meza moja na kupata suluhu ya matatizo yaliyopo,” anasisitiza Mazurui.

Mazurui anataja njia nyingine kuwa ni kutumia viongozi wastaafu wanao aminika kuwa na busara katika nchi yetu ili wawashinikize na kuwashauri watawala kuona umuhimu wa kubadilika.

“Katika nchi yetu tumebalikiwa kuwa na marais wastaafu ambao wanaishi mpaka sasa, yupo mzee Ali Hassan Mwinyi, Benjamin Mkapa na Jakaya Kikwete. Hawa wote ni hazina ambayo tunaweza kuitumia vizuri na tukafanikisha,” anasisitiza.

Mazurui anasema katika viongozi hao pia wanaweza kuwatumia watu kama Jaji Warioba lakini pia viongozi wa dini ambao wanaonekana kuwa na ushawishi mkubwa pengine utawasikiliza.

Anasema jambo la msingi watawala wanapaswa kutambua kuwa Tanzania siyo ya chama tawala cha CCM au wapinzani badala yake ni ya wote hivyo kila mmoja anapaswa kuilinda kwa gharama yoyote.

Wachambuzi washauri

Akizungumzia hali hiyo Mkurugenzi wa Kituo cha Sheria na Haki za Binadamu (LHRC) Dk Hellen Kijo-Bisimba anasema kwa hali ilivyo sasa ni vigumu sana kwa wanasiasa kufanya siasa.

Dk Bisimba anasema hali hiyo inatokana na wanasiasa kuwawekea hali ngumu wanapotekeleza majukumu yao ambayo kwa mujibu wa sheria wanapaswa kufanya mikutano, maandamano na mazungumzo lakini sasa vyote hivyo haviwezekani.

Anasema ili kuondoka katika hali hiyo ni lazima mambo mawili yafanyike adha, kwa upande watawala au wapinzani.

Dk Bisima anashauri kwa upande wa Serikali kama wanataka kuendelea kuvibana vyama vya siasa hawana budi kupeleka mswada wa sheria ili kuvifuta vyama hivyo.

“Huwezi kusema unakubali upinzani lakini unaminya harakati zao zote; jambo la msingi mswada upite turudi katika mfumo wa chama kimoja ili dunia ijue kwamba Tanzania hatutaki upinzani,” anasisitiza.

Dk Bisimba anasema endapo hilo halitafanyika basi wapinzani wana jukumu kubwa la kupinga hali hiyo kwa kwenda mahakamani.” Tunajua Mahakama zetu haziaminiki wasikate tamaa wakishindwa katika za ndani watoke hata nje ya Afrika Mashariki na Afrika.

“Wasitishwe na changamoto zilizopo katika Mahakama kudai haki kuna gharama zake cha msingi wasione shida kutoka hata nje ya mipaka yetu ipo siku haki itatendeka.”

Jinsi walivyokuwa wakisirikishwa

Awali wapinzani walizoea siasa za majukwaani lakini pia palikuwa pakitokea sintofahamu na kutoelewana baina yao na utawala njia ya mazungumzo ilikuwa ikifanyika.

Ilishuhudiwa mara kwa mara viongozi kutoka vyama vya wapinzani walialikwa Ikulu kuzungumzia mambo mbalimbali na mwisho wa siku walitoka na kauli moja.

Mfano Rais Jakaya Kikwete mara kadhaa alivialika vyama mbalimbali vya upinzani kwa ajili ya kubadilishana mawazo lakini pia kipindi cha maandalizi wa mchakato wa Katiba mpya aliweza kukaa nao na kujadili kwa pamoja jambo lililosababisha kuanzishwa kwa mchakato huo.