Kinana alibaki katibu mkuu wa CCM asiye na furaha tangu Julai 2016

Muktasari:

  • Angalau sasa baada ya Katibu Mkuu wa CCM, Abdulrahman Kinana kukubaliwa ombi lake la kujiuzulu, mabadiliko ya kiutendaji yanaweza kutokea, maana chanzo cha mdororo wa kiufanisi katika ofisi ya katibu mkuu ni Kinana ‘kukaa na barua kujiuzulu mkononi’ na bila shaka hakuwa furaha kwenye nafasi yake.

Mwandishi wa habari, aliye pia mtunzi wa vitabu na simulizi fupi, Fyodor Dostoevsky aliacha hekima kuhusu furaha. Alisema, furaha kubwa kuliko zote hupatikana baada ya kugundua chanzo cha kutokuwa na furaha. Dostoevsky alikuwa raia wa Urusi na aliishi Karne ya 19.

Angalau sasa baada ya Katibu Mkuu wa CCM, Abdulrahman Kinana kukubaliwa ombi lake la kujiuzulu, mabadiliko ya kiutendaji yanaweza kutokea, maana chanzo cha mdororo wa kiufanisi katika ofisi ya katibu mkuu ni Kinana ‘kukaa na barua kujiuzulu mkononi’ na bila shaka hakuwa furaha kwenye nafasi yake.

Maneno ya Lelouch Lamperouge ambaye ni mhusika mkuu wa kutengeneza mfululizo wa tamthiliya za “Code Geass: Lelouch of the Rebellion” yanaweza kutuleta karibu. Lelouch amepata kusema:

“Furaha ni kama kioo, ukiwa nayo popote ukiwepo itakuzunguka. Lakini bado haitaoneka. Hata hivyo, ukibadili namna ya kuitazama, hung’ara na kupendeza kuliko kitu kingine chochote.”

Tafsiri ni kuwa furaha haionekani lakini hung’ara machoni na kwa vitendo kwa yule mwenye nayo. Inatafsiri pia kwamba asiye na furaha unaweza kumbaini haraka kwa vitendo vyake. Maana hupoteza nuru. Tumeambiwa furaha ni kama kioo. Ikiwepo huakisi nuru, isipokuwepo ni giza.

Mfano wa karibu zaidi ni Katibu wa Itikadi na Uenezi CCM, Humphrey Polepole. Uhusika wake kwenye majukumu aliyonayo unaakisi furaha yake katika nafasi aliyopo. Polepole yupo hai sana kiutendaji na kimijadala. Ukimtazama Polepole kwa uelekeo tofauti, unauona mng’aro wake.

Kwa tafsiri hiyohiyo, ukimya wa Kinana ulikuwa unadhihirisha ni kiasi gani alivyopoteza furaha. Uzuri ni kuwa hakuwa mpya kwenye nafasi yake. Alikuwepo tangu mwaka 2012. Kazi alizofanya zilionekana. Uwajibikaji wake ulijipambanua mno.

Ni kwa msingi huo ndiyo maana alivyobadilika ikawa rahisi kumtambua. Mabadiliko hayo yalisababisha minong’ono mingi. Uvumi wa Kinana ama kujiuzulu au kususa uliibuka na kupotea mara kadhaa kati ya Machi mwaka jana hadi hivi karibuni alipokubaliwa kung’oka.

Machi 23, mwaka jana, mbunge wa Mtama (CCM), Nape Nnauye aliondolewa kwenye nafasi ya Waziri Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo. Iliaminika sababu ya Nape kung’olewa ni msimamo wake wa kufuatilia na kutaka haki itendeke juu ya tukio la uvamizi kwenye kituo cha Clouds TV.

Machi 17, mwaka jana, Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Paul Makonda alidaiwa kuvamia kituo cha Clouds TV na kulazimisha kurushwa hewani maudhui yaliyokataliwa na waandaaji wa kipindi cha Shilawadu pamoja na wamiliki wa kituo. Tukio hilo lilitikisa mno lakini iliisha kimya kimya.

Kitendo cha kuvuliwa uwaziri Nape, kiliibua minong’ono kuwa Kinana hakufurahia na uamuzi huo, hivyo akaamua kususa. Yapo maneno yalinong’onwa kwamba alikuwa ameachia ngazi na kwamba alikuwa haingii kabisa kwenye ofisi yake. Ikavumishwa pia kuwa hakuwa akijulikana alipo.

Ni Mwenyekiti wa CCM, Rais John Magufuli aliyeondoa sintofahamu hiyo akatoa ufafanuzi kuwa Kinana alikuwa nje ya nchi kwa matibabu kwa ruhusa aliyompa. Pamoja na kufafanua hilo minong’ono iliendelea.

Tukubali furaha ni kioo

Julai 2016, kuelekea mkutano mkuu maalumu wa CCM, uliomchagua Rais Magufuli kuwa mwenyekiti wa chama, Kinana alikuwapo na kutangaza kusudio lake la kuachia ngazi. Alisema kuwa hata nafasi yenyewe aliishika kwa ombi la wazee, ila hayakuwa mapenzi yake.

Wakati wa mkutano mkuu, Rais Magufuli aliikataa barua ya Kinana na kumtaka aendelee kushika nafasi ya katibu mkuu. Kinana alipokuwa akielezea alivyoafiki kuendelea na nafasi hiyo, alisema alipokea kijiti cha ukatibu mkuu kutoka kwa mtangulizi wake, Wilson Mukama baada ya kuombwa mara nyingi na Rais mstaafu, Jakaya Kikwete.

Kwa maneno yake mwenyewe, Kinana alisema: “Niliona si heshima kumkatalia Rais wa nchi.” Kauli hiyo inadhihirisha kuwa hata Rais Magufuli alipoikataa barua yake ya kuomba kuachia ngazi, alikubali kwa sababu aliyemkatalia kujiuzulu ni Rais.

Kikwete pia alipata kuelezea safari ya kumshawishi Kinana kuwa Katibu Mkuu wa CCM, kwamba kila mara alipomuomba alikataa. Kabla ya Yusuf Makamba kuwa katibu mkuu, alipeleka ombi kwa Kinana akakataa. Mwaka 2012 baada ya Mukama, Kikwete alisema, alimwambia Kinana kuwa safari hiyo hakuwa na namna zaidi ya kukubali ili kukiokoa chama.

Hivyo basi, suala kwamba Kinana hakuwa akitaka awe Katibu Mkuu CCM halibishaniwi. Maana limezungumzwa mara kadhaa na yeye mwenyewe, kisha Kikwete alilitolea ufafanuzi mzuri. Huo ni uthibitisho tosha kuwa majukumu aliyopewa kwa imani kubwa kuwa anayaweza, yeye hakuyataka.

Hata hivyo, ipo tofauti kubwa ya kiutendaji kati ya Kinana aliyeombwa na Kikwete kuwa katibu mkuu na yule aliyehitajika kubaki kwenye nafasi hiyo kama alivyoombwa na Magufuli. Kinana chini ya wenyeviti wawili, ni tofauti kama usiku na mchana.

Kinana chini ya Kikwete alionekana injini ya chama. Zipo taarifa kwamba alikuwa akitumia mpaka rasilimali zake binafsi kuzunguka mikoa, wilaya, majimbo, kata na vijiji ili kukijenga chama. Akiwa na kijana wake, Nape, alipokuwa Katibu wa Itikadi na Uenezi, walikatiza porini na kuvuka mito, maziwa na bahari kukipa uhai chama.

Kinana alikuwa mwenye kukisemea chama hasa. Alikuwa tayari kugombana na mawaziri wa Serikali iliyoongozwa na mwenyekiti wake (Kikwete) ili kuwafanya wananchi waone kwamba CCM ni chama chenye kujali na kutetea masilahi ya umma. Alitaka ionekane kuwa makosa ya Serikali chanzo chake siyo CCM.

Kinana chini ya Kikwete alitaka mawaziri wawajibike kwenye chama. Miaka ya nyuma Katiba ya CCM iliipa mamlaka sekretarieti ya chama kuita watendaji wa Serikali kasoro Rais ambaye ni mwenyekiti wao, na kuwahoji kuhusu utendaji. Kinana alitaka hilo litekelezwe. Ndiyo sababu alianzisha msamiati wa mawaziri mizigo.

Siku hizi kipengele hicho cha sekretarieti ya CCM kuwa na mamlaka ya kuwaita na kuwahoji watendaji wa Serikali hakionekani, yamebaki maagizo ya jumla kwenye majukumu ya Halmashauri Kuu kwamba mojawapo ni kusimamia maendeleo pamoja na usalama wa Taifa.

Kinana wa Magufuli

Uhodari wa Kinana katika kukipigania chama haupo tu kipindi alipoteuliwa kuwa katibu mkuu na Kikwete, bali hata alipokuwa akiyavaa ‘mabomu’ na kusimama mstari wa mbele kama meneja wa kampeni za urais wa Rais wa Tatu, Benjamin Mkapa, vilevile Kikwete kwa vipindi vyote viwili.

Vipimo viwili; jinsi Kinana alivyoipigania CCM akiwa katibu mkuu na kuipa uhai mpaka kushinda Uchaguzi Mkuu 2015 licha ya kukutana na misukosuko mingi, vilevile alivyosimamia kampeni za urais wa Mkapa na Kikwete, ndiyo unaweza kujua uhusika wa Kinana chini ya Magufuli ulivyobadilika.

Ni dhahiri tangu Julai 2016 alipokataliwa kujiuzulu alibaki kwenye nafasi hiyo bila kuonyesha furaha. Kinana akawa mwenye kuacha nembo ya chama awe Polepole. Kinana akawa kimya kabisa. Uhusika huo ndiyo ulisababisha minong’ono ya mara kwa mara kuwa alikuwa njia moja kung’oka.

Kauli ya Rais Magufuli kuwa Kinana alitaka mara nyingi kujiuzulu akawa anamkatalia au kumbadilishia mada ili asitamke kujiuzulu, inaleta afya kwenye minong’ono mingi iliyopita, kwamba kweli Kinana hakutaka tena kuendelea na cheo hicho.

Hata Desemba mwaka jana, aliporejeshwa baada ya uchaguzi wa CCM, wajumbe wa mkutano mkuu walishangilia, ila yeye alibaki hana furaha.

Inawezekana lugha ambayo aliitumia Kikwete ni tofauti au ilijaa vilainishi, maana siku ya Magufuli kukabidhiwa uongozi wa CCM, Kinana alimpa sifa nyingi Kikwete. Pengine Kinana na Kikwete waliwezana kwa sababu wote ni wanajeshi.

Jambo moja ambalo linaweza kuelezeka ipasavyo ni kwamba Kinana alipewa kazi ambayo hakuitaka, japo ni ya kukitumikia chama chake. Hivyo, kitendo cha kumbakisha muda mrefu wakati alikuwa ameshaomba kupumzika, ilikuwa ni kumnyima furaha na kuzidi kumuumiza.

Unaweza pia kupatia ukisema kuwa Kinana alipopokea kijiti cha ukatibu mkuu wa CCM, kulikuwa na joto kali la upinzani na chama chake kilikuwa kwenye tishio la kupoteza dola mwaka 2015. Pengine sasa wajibu wake mkubwa aliouona ni kutumia nguvu na maarifa yake kuhakikisha CCM inashinda Uchaguzi Mkuu 2015.

Ikiwa malengo yalikuwa ni hayo na kwa sababu CCM ilifanikiwa kushinda uchaguzi, ikaendelea kuongoza dola, nini tena alikuwa anasubiri? Na hapa ni kuonyesha kwamba hakuwa akitania alipotaka kujiuzulu Julai 2016. Aliona kazi aliyoombwa na swahiba wake Kikwete, alikuwa ameshaimaliza vema. Alipoombwa aendelee alipoteza furaha.

Kuna suala la umri. Ni mtu mzima sasa. Tangu jeshini, ubunge, uwaziri, akawa Spika wa Bunge la Afrika Mashariki kisha Katibu Mkuu CCM, nafasi ambayo ilimfanya awe na hekaheka nyingi na kuwa mbali na familia yake kwa muda mrefu, bila shaka ni vizuri pia Rais Magufuli amemkubalia apumzike. Wana CCM hawatamsahau Kinana.