Kinga za viongozi zisiwe kigezo kuficha maovu

Kinga ni mhimu sana katika maisha ya binaadamu na hata kwa harakati za kawaida za maisha kama kujiepusha na majanga ya hali ya hewa au ajali.

Si jambo la kawaida kwa mtu kuweka mazingira ya kuhatarisha maisha yake au ya watu wengine na baadaye kusema kwa upole kuomba kinga asiwajibishwe kisheria.

Kutoa tafsiri ya kwamba kiongozi aliyeondoka madarakani anakomolewa kisiasa au analipiziwa kisasi kwa aliyoyatenda alipokuwa katika uongozi ni tafsiri potofu na ni kisingizio cha kutaka kuficha maovu.

Kama kiongozi alitenda haki alipokuwa madarakani hapatakuwepo mwanya wa kumsingizia maovu ya aina yoyote.

Mathalan, mmiliki wa meli au jahazi kufanya safari na chombo chenye hitilafu au hali ya hewa ikiwa hatarishi na ikiwa kumetolewa onyo na wataalamu kutaka vyombo visisafiri yeye akafanya safari, yakitokea maafa na baadaye mtu huyo akaomba kinga ya kutowajibishwa kisheria, hii haiwezekani.

Hivyohivyo, haieleweki mtu kuiba au kubaka mtoto na baadaye kuomba kinga asishtakiwe. Kiga nzuri ni kutofanya kosa na neno bahati mbaya siku zote haliwezi kuwa leseni ya mhalifu kupata msamaha.

Lakini, tunachokiona kwa vingozi wengi wa Afrika, kama sasa Zimbabwe ambapo Rais Robert Mugabe aliyetawala kwa miaka 37 anajiuzulu kwa masharti kwamba yeye, mke na watu wake wa karibu wasiguswe kwa tuhuma za ukiukaji katiba, mauaji, kutesa watu na ubadhirifu wa fedha za umma wapewe kinga ya wasishtakiwe kwa lolote lile.

Kwa hakika sifahamu ni kwa mantiki gani hata viongozi wa Afrika katika hiyo klabu yao inayoitwa Umoja wa Afrika, viongozi wa Afrika waliamua miaka mitatu iliyopita kupitisha azimio la kujiwekea kinga wakiwa madarakani.

Mwenendo huu kwa njia yoyote ile unadhoofisha dhana ya utawala bora kwa sababu unampa kamba ndefu kiongozi wa nchi kufanya atakavyo kwa kuelewa anayo kinga ya kutoshtakiwa baada ya kuondoka au kuondolewa madarakani.

Kwanza kinga hii inawapa mwanya viongozi wa Kiafrika kulazimisha kwa njia yoyote ile kubaki madarakani kwa muda watakao au hata maisha na kwa njia yoyote ile, iwe kubadili Katiba au kufanya uchaguzi na kutumia mizengwe kuonyesha kwamba wamepata ridhaa ya wananchi wao.

Hesabu za harakaharaka zinatoa sura kwamba kama kiongozi wa nchi amefanya maovu ya kukiuka katiba au kutoheshimu haki za raia wake, hatakuwa tayari kuondoka madarakani kwa hiari.

Kwa kuhofia kuwajibishwa katika Mahakama ya Kimataifa (ICC) ambayo hapo mwanzo waliridhia, viongozi wa Afrika waliamua miaka 10 iliyopita kuunda Mahakama ya Afrika na makao yake makuu yapo Arusha.

Lakini, hata hiyo Mahakama ya Afrika yenye majaji kutoka nchi mbalimbali wanachama walioiunda, sasa wanaiogopa na tayari wapo waliojitoa, walioelezea nia yao ya kujitoa na wengine kusuasua kutoa ridhaa ya kuikubali kwa kuhofia kushtakiwa kwa uhalifu wa kivita au vitendo vya ukiukaji wa haki za binadamu.

Hapa inafaa kukumbusha namna viongozi wa nchi nyingi za Kiafrika walivyotaka watawala wa serikali ya makaburu ya Afrika Kusini wakati wa utawala wa kibaguzi wawajibishwe kisheria na jumuiya ya kimataifa na kutengwa katika medani ya kisiasa, kiuchumi na michezo kinyume na wanavyotaka wao.

Lakini leo viongozi hao wa Afrika wanatuhumiwa na uhalifu kama wa mauaji na ukiukaji mkubwa wa haki za binadamu, wasiwajibishwe na nchi zao wala katika medani ya kimataifa wanapoondoka madarakani.

Kwa kawaida mtu ambaye hajatenda kosa huwa hana wasiwasi anapotuhumiwa kutenda uhalifu kwa vile kama hajafanya hapatakuwa na ushahidi wa kumtia hatiani na zuri zaidi ni kwamba hiyo itakuwa nafasi nzuri ya kusafisha matope aliyopakwa.

Wengi tulitarajia mauaji ya halaiki yaliyofanyika Rwanda yangetoa fundisho kwa nchi nyingine za Kiafrika ili zisijaribu kurudia unyama kama ulioonekana Rwanda bali kuchukua kinga za kutokaribia huko.

Lakini yaliyotokea Siera Leone na kwingineko yanasikitisha na inaonyesha baadhi ya viongozi wetu wanaona wapo huru kufanya watakavyo, ikiwa ni pamoja na kudhulumu roho za raia wanapokuwa madarakani. Hili haliwezi kukubalika.

Baadhi ya viongozi wameonekana kulindana na kuzilaumu nchi za Magharibi kwa kuwa na agenda ya siri dhidi ya viongozi wa Kiafrika. Je, na hawa wanaonyooshewa vidole kwa kudaiwa wanatawala kwa mkono wa chuma hawana agenda ya siri katika nchi zao?

Kwa kweli hatua yoyote ile ya viongozi wa Kiafrika kujiwekea kinga ni kudhoofisha upatikanaji wa haki na kuimarika kwa utawala wa haki na sheria.

Popote pale ambapo hakuna uwajibikaji, hapawezi kuwa na utawala wa haki na sheria.

Ni vizuri kwa nchi za Kiafrika kuchukua hatua za kujipima upya na kuondokana na huu utamaduni mpya unaojengekea kwa kasi hivi sasa katika nchi mbalimbali, wa kuwawekea kinga viongozi wao wakuu wa nchi, hata kwa maovu ya kinyama waliyoyatenda walipokuwa madarakani.

Kama vingozi wakuu wa nchi wanawekewa kinga kwa nini watumishi wengine wa Serikali nao wasipewe kinga hiyo?

Sheria lazima iachiwe kuchukua mkondo wake kwa viongozi wanaokiuka Katiba na kusababisha maafa kama anavyowajibishwa mtu anayejiingiza katika vitendo vya uhalifu vya wizi wa nazi, ndizi na maandazi.

Utawala bora ni ue wa watu wote kuwa sawa mbele ya sheria na si wengine kuwa juu ya sheria na kinga nzuri ni kuheshimu Katiba na kujizuia kuvunja sheria za nchi na za kimataifa.

Tumeridhia mikataba mbalimbali ya kimataifa na ya kanda na kuahidi kuheshimu haki za binaadamu na kuwa na uongozi wa haki na sheria katika nchi zetu.

Tuonyeshe huko kuridhia kwetu kwa vitendo na si kwa maandishi mazuri na kauli peke yake.