Kiongozi bora huishi maisha mazuri baada ya kuondoka madarakani

Rais mstaafu wa Zambia,Kenneth Kaunda.  Picha ya Maktaba.

Muktasari:

  • Usiku utaufanya mchana kisha mchana wa jua kali utaugeuza kuwa asubuhi kwa sababu ya kiburi cha ujana. Utaliona jua linachomoza asubuhi, litachanua na utaitwa mchana, litapoa majira yatasoma magharibi kisha usiku utaingia. Ujana ukikutawala hutajua kama ndiyo nyakati zinasogea.

Upo msemo wenye kukumbusha nidhamu ya maisha kwamba ujana maji ya moto fainali uzeeni. Maana ujana unasahaulisha. Damu inachemka, nguvu zipo, ubongo unafanya kazi kwa kasi, macho yanaona na kadhalika. Kwa hiyo unajidanganya kuwa dunia imeganda na haizunguki kukupeleka uzeeni.

Usiku utaufanya mchana kisha mchana wa jua kali utaugeuza kuwa asubuhi kwa sababu ya kiburi cha ujana. Utaliona jua linachomoza asubuhi, litachanua na utaitwa mchana, litapoa majira yatasoma magharibi kisha usiku utaingia. Ujana ukikutawala hutajua kama ndiyo nyakati zinasogea.

Utafika mwaka mpya na utausherehekea kwa mbwembwe na kufuru kwamba umefanikiwa kuuona mwaka mwingine. Hata hivyo, kadiri utakavyohesababu sherehe za mwaka mpya ndivyo safari ya uzeeni inavyochanganya.

Uongozi ni sawa na ujana. Uongozi hulevya na kusahaulisha. Fainali ya kiongozi ni pale anapotoka madarakani. Aina ya maisha ambayo hukutana nayo huakisi moja kwa moja nyakazi alipokuwa madarakani.

Maisha ya mtu katika ujana wake huamua matokeo ya uzee. Vivyo hivyo kwa kiongozi, mtindo wake wa maisha akiwa madarakani, huamua taswira ya maisha yake baada ya kuachia ngazi.

Mfano wa Alhaj Jumbe

Rais wa Pili wa Zanzibar na Makamu wa Kwanza wa Rais mstaafu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Alhaj Aboud Jumbe Mwinyi alifariki dunia mwaka jana. Sisi sote ni wa Mwenyezi Mungu na kwake tutarejea.

Alhaj Jumbe akiwa tayari kwenye safari ya dawamu, chukua somo muhimu katika maisha yake. Jumbe alikuwa mnyenyekevu, hakuwa na makuu, si mbishi. Alipoambiwa asirudi Zanzibar alikubali, alikwenda kuishi Mji Mwema, Kigamboni jijini Dar es Salaam.

Ruhusu maisha ya Jumbe yaingie kwenye damu yako na yapenye kwenye mifupa kwa namna watu walivyompenda. Zanzibar, CCM na CUF wote waliguswa na kifo chake.

CCM ndiyo walikuwa wenzake, lakini walitofautiana kuhusu muundo wa Muungano, aliamini suluhu ni Serikali tatu, wenzake wakang’ang’ania Serikali mbili. Nguvu ya chama ikamwondoa na ili asieneze sumu ya Serikali tatu Zanzibar, akaambiwa abaki Dar es Salaam.

Upendo kwa Jumbe unafundisha kuwa hakuwahi kuchukiwa, ila alitofautiana na wenzake kwenye chama na Serikali. Watanzania walikuwa na hamu ya kuendelea kumpigania. Ndiyo maana kwa miaka 32 ya uwapo wake nje ya siasa, aliendelea kukumbukwa. Jumbe aliishi vizuri na watu ambao walimhifadhi moyoni.

Upo mfano wa Kaunda

Rais wa Kwanza wa Zambia na Baba wa Taifa hilo, Kenneth Kaunda (KK), aliposhindwa uchaguzi mwaka 1991 na Fredrick Chiluba (alifariki dunia), alikumbana na misukosuko mingi.

Tofauti na Jumbe ambaye aliendelea kuhudumiwa na kupewa ulinzi kama Rais mstaafu, Kaunda alipewa misukosuko. Aliishi nyumbani kwake kama jela, hakutakiwa kutoka. Nyumba ilizungukwa na jeshi.

Zipo nyakati Kaunda aliwekwa jela na kuiona nchi ambayo yeye alisimama mstari wa mbele kupambana na wakoloni ili iwe huru kama jehanamu. Chiluba alimtesa Kaunda, alimfanya aonekane si lolote wala chochote.

Chiluba alipomaliza uongozi wake na kumkabidhi mrithi wake, marehemu Levy Mwanawasa, mambo yaligeuka. Mwanawasa alitambua kiu ya wananchi wa Zambia, kumuona baba yao wa taifa akiwa huru.

Alijua ili kuujengea imani na hadhi uongozi wake lazima awe mtetezi wa Kaunda. Hivyo, akatangaza kumuweka huru. Mwanawasa alimwomba radhi Kaunda kwa yote aliyofanyiwa kipindi cha uongozi wa Chiluba.

Mwanawasa hakuishia hapo, alimthibitisha Kaunda kama mwasisi wa Taifa la Zambia. Na tangu hapo Kaunda amekuwa akibeba hadhi ya Baba wa Taifa la Zambia.

Kama Jumbe, jifunze pia kuhusu Kaunda. Ni kwamba wananchi walimpenda na walimwona anaonewa, ndiyo maana kipindi anafanyiwa ghasia nyingi na Chiluba, walikuwepo watu ambao walikuwa tayari kumpigania.

Haikuwa ajabu kwa Mwanawasa kubatilisha kila adhabu ambayo Kaunda alikuwa anapewa na Chiluba. Ni kwamba Kaunda hakuishi kwenye vichwa vya wananchi wa Zambia tu, aliishi kwenye nyoyo za Wazambia.

Turudi kwa Alhaji Jumbe

Jumbe hakubaki tu mtu wa kukumbukwa na kusahaulika ndani ya vichwa vya Wazanzibari na Watanzania kwa jumla, bali dhati yake ilituama kwenye mioyo yao. Kwa kila alichofanyiwa, wananchi walizidi kumuweka moyoni.

Alikuwa hazungumzwi kwa sauti kubwa lakini minong’ono ilisikika kutoka muongo mmoja kwenda mwingine mpaka ikazidi mitatu. Utastaajabu vijana ambao walizaliwa baada ya mwaka 1984 lakini wanamjua Jumbe. Hawakuwa wakimwona mara kwa mara kutokana na mtindo wa maisha aliopangiwa lakini historia yake iliteka nyoyo zao.

Kama wewe ni kiongozi, hakikisha unawekeza uongozi wako na tabia zako kwenye mioyo ya watu. Maana uongozi ni jambo la kupita tu. Kwa kumaliza muda wako au kuondolewa, amini kuwa nje ya uongozi utatetewa na kupendwa na watu kama ulikuwa ndani ya nyoyo zao. Na utapuuzwa au kuchukiwa, ikiwa uliishi kwenye fikra tu.

Unapokuwa kiongozi hakikisha unawaongoza watu vizuri ili wakuhifadhi ndani ya mioyo yao. Muhimu kutambua ni kuwa ukishatoka madarakani lazima urudi kuishi nao kama raia mwenzao.

Viongozi wengi baada ya kutoka madarakani huyaona maisha magumu kutokana na uwekezaji wao walipokuwa kwenye uongozi. Ukiwa kiongozi kwa cheo cha kuteuliwa au kuchaguliwa, tambua kwamba uongozi ni wakati wa uwekezaji, fainali ni baada ya kuachia ngazi.

Elimika na Valentine Strasser

Valentine Strasser alipata kuwa Rais wa Sierra Leone. Wakati akiingia madarakani, aliweka rekodi ya kuwa kiongozi mwenye umri mdogo kuwahi kutokea. Hata sasa, hakuna Taifa ambalo limewahi kupata mkuu wa nchi mwenye umri chini ya miaka 25 ili avunje rekodi ya Strasser.

Aprili 29, 1992 Strasser akiwa kijana mwanajeshi mwenye umri wa miaka 25, aliwaongoza wanajeshi wenzake kuvamia Ikulu ya Sierra Leone, wakamteka aliyekuwa Rais wa nchi hiyo, Joseph Saidu Momoh wakamlazimisha kukimbia naye akatorokea Conakry, Guinea.

Baada ya Momoh kutorokea Conakry, Strasser alijitangaza kuwa Rais wa Sierra Leone. Maisha yakabadilika, alishakuwa mkuu wa nchi. Kwa hiyo hakutaka kuishi kwenye nyoyo za Wasierra Leone.

Hakulipa malimbikizo ya mishahara ya wanajeshi na watumishi wengine wa umma. Alifuja almasi ya Sierra Leone, kwa vile jina lake ni Valentine, basi sikukuu ya ‘Valentine’s Day’ akaifanya kuwa sherehe ya kitaifa yenye mapumziko.

Alikuwa mtu wa starehe, vurugu nyingi kwa wanawake, aliua watu wasio na hatia. Strasser alisahau kuwa ipo siku uongozi hautakuwa kwenye mikono yake na ambacho kinaweza kumfaa ni kuishi ndani ya mioyo ya watu ili wamtetee na kumpigania baadaye.

Januari 16, 1996, Strasser alipinduliwa na msaidizi wake, Brigedia Jenerali Julius Maada Bio. Strasser alikimbilia Uingereza, akajiunga na Chuo Kikuu cha Warwick, kilichopo mjini Coventry, akaanza masomo ya sheria, akasema anataka awe wakili ili awatetee Waafrika.

Mwaka mmoja wa masomo, Strasser aliishiwa fedha, akaacha chuo. Maisha Uingereza yakawa magumu, akakimbilia Gambia nako kukawa pagumu mwisho akarudi Sierra Leone mjini Grafton, Mashariki ya Mji Mkuu wa nchi hiyo, Freetown.

Kazi ya kwanza ambayo Strasser aliifanya ikawa kuanzisha chuo kidogo cha kufundisha kompyuta na Teknolojia ya Habari na Mawasiliano (Tehama). Maisha ya chuo yakamshinda.

Baada ya kila kitu kwenda kombo, Strasser alirudi nyumbani kwa mama yake mzazi na kuishi kwenye banda la uani. Hata sasa akiwa na umri wa miaka 49, anakunywa pombe za kienyeji mtaani. Hana hadhi yoyote kama kiongozi mkuu wa nchi mstaafu.

Strasser anaishi kama mtu tu mtaani. Mlevi na hakuna anayemjali. Hana mtu wa kumtetea wala kumpigania kwa sababu hakuishi kwenye nyoyo za watu. Strasser ndiye mkuu wa nchi wa zamani, anayeishi kimaskini kuliko wote duniani.

Ukiwa kiongozi na kugeuka kituko kama Strasser inawezekana kabisa. Ishi vibaya na watu wasikupende, akija mtawala ambaye hatakutambua kama mkuu uliyepita, unaweza kuishi maisha ya hovyo kama ombaomba mtaani au mnywa gongo uliyeshindikana.

Luqman Maloto ni mwandishi wa habari, mchambuzi na mshauri wa masuala ya kijamii, siasa na sanaa. Ni mmiliki wa tovuti ya Maandishi Genius inayopatikana kwa anwani ya mtandao www.luqmanmaloto.com