TUJADILI UCHUMI: Kipimo cha mafanikio kwenye uchumi ni zaidi ya idadi ya viwanda

Thursday November 9 2017

 

By Profesa Honest Ngowi; [email protected]

Kati ya mambo makuu yanayosisitizwa na serikali ya awamu ya tano katika maendeleo ni kuwa na uchumi wa viwanda. Hili ni jambo zuri kwa sababu ya faida zake ambazo ni pamoja na uwezekano wa kuongeza ajira, mapato ya kodi na yasiyo ya kodi, fedha za kigeni na kukuza sekta nyingine zinazofungamana na sekta ya viwanda.

Kwa uujumla uchumi wa viwanda unaongeza uwezekano wa kukua kwa pato la taifa na kuchangia kupunguza umasikini hasa uliokithiri.

Katika azma ya kuwa na uchumi wa viwanda suala la idadi ya viwanda limejitokeza na litajitokeza kwa namna mbalimbali. Linaweza kujitokeza katika malengo yanayotakiwa kufikiwa katika muda fulani, kwa mfano kila mkoa kuwa na viwanda 100 ndani ya mwaka mmoja.

Pia idadi itatajwa katika tathmini mbalimbali kwa mfano ya idadi ya viwanda vilivyojengwa au kufufuliwa katika muda fulani kama vile mwaka mmoja au miwili hata mitano tangu azma hiyo kutangazwa.

Kiutaalamu na kiuchambuzi ni vizuri kuelewa kuwa idadi ya viwanda ni muhimu sana. Mambo mengine yote yakikaa sawa, idadi kubwa zaidi ya viwanda inapaswa kuwa neema zaidi.

Hata hivyo idadi ya viwanda pekee si kipimo tosha cha mafanikio ya uchumi wa viwanda. Kuna mambo mengine mengi ya kuzingatia. Inapendeza kuainisha na kujadili mambo haya kitaalamu ili azma ifanikiwe vizuri zaidi.

Azma ya viwanda

Azma ya uchumi wa viwanda Tanzania imejadiliwa na kuandikwa sehemu nyingi. Kuna aina tatu za viwanda vinavyofikiriwa na serikali ya awamu ya tano. Hivi ni viwanda vinavyoweza kuajiri watu wengi, vinavyoweza kuzalisha bidhaa kwa walaji wengi na vitakavyozalisha ili kuuza nje ya nchi.

Pamoja na mambo mengine serikali inalenga kuimarisha viwanda vilivyopo na kuongeza mchango wa sekta hii katika pato la taifa ifikapo mwaka 2020. Inalenga kuzalisha asilimia 40 ya ajira zote nchini ifikapo mwaka 2020. Lengo jingine ni kuuza katika masoko ya upendeleo ya kikanda duniani.

Idadi ya viwanda

Idadi ya viwanda ni moja kati ya mambo muhimu kupima mafanikio ya kuwa na uchumi wa viwanda popote duniani. Katika muktadha wa kutaka idadi fulani ya viwanda ndani ya muda fulani ni muhimu kwa wadau wote wakiwamo wanaotoa na kupokea maagizo na ushauri kuelewa yaendanayo na idadi ya viwanda.

Haya ni pamoja na rasirimali watu ambayo lazima iandaliwe katika ngazi mbalimbali. Kutegemea aina ya rasilimali watu, kuna itakayohitajika kuandaliwa miaka kadhaa kabla ya kuwa na idadi inayotakiwa na kuagizwa. Mahitaji mengine ni rasilimali fedha zilizopo kwa ajili ya kuwekeza katika sekta hii.

Nyingine ni malighafi za kufanikisha ulishaji kwenye viwanda husika, miundombinu ya aina zote, umeme na maji kwa matumizi ya viwanda na shughuli nyingine muhimu zinazoambatana navyo.

Mambo mengine muhimu ni suala la mazingira kwa maana ya athari zinazoweza kuletwa na idadi kubwa ya viwanda. Ni mambo yanayohusu uchumi wa kijani kwa maana ya uwezo wa nchi na dunia kwa ujumla kubeba viwanda na yatokanayo na viwanda. Idadi ya viwanda tunavyotaka lazima iendane na uwezo wa mazingira kuzalisha mahitaji ya viwanda hivi na kuhimili uchafu utakaotokana navyo.

Soko

Idadi ya viwanda katika uchumi shindani wa soko inatakiwa kuamuliwa kwa kiasi kikubwa na mwingiliano huru wa nguvu za ugavi na utashi sokoni. Viwanda 100 kwa kila mkoa kwa mwaka kwa mfano vinaweza kuwa vingi au vichache mno kutegemea na hali halisi ya soko.

Kiutaalamu idadi ya viwanda huamriwa na matokeo ya upembuzi yakinifu unaozingatia mambo mengi. Pamoja na soko, idadi ya viwanda lazima iendane na mtaji uliopo, maendeleo ya sekta nyingine zinazotegemeza na kutegemewa na viwanda katika mwingiliano wa kisekta.

Hali halisi ya teknolojia nayo ni muhimu kuamua idadi ya viwanda. Teknolojia ya hali ya juu sana inaweza kufanya viwanda vichache tuu kuzalisha bidhaa ambazo zingezalishwa na viwanda vingi vitumiavyo teknolojia ya zamani. Tukitaka viwanda 100 ndani ya miezi 12 kila mkoa, ni lazima pia kuongeza haya yanayoendana na idadi hii katika kila mkoa na nchi kwa uwiano unaotakiwa.

Vigezo zaidi

Taarifa na mijadala ya idadi ya viwanda ni lazima iangazie aina za viwanda vinavyotakiwa. Tunapotaja idadi ya viwanda lazima tutaje vimezalisha ajira kiasi gani za moja wa moja na zisizo za moja kwa moja. Walioajiriwa wamepata kazi zenye staha kiasi gani ikiwamo ujira na namna ujira huu unavyowasaidia kuondokana na umasikini.

Pia, lazima kusema idadi hiyo ya viwanda imetumia vipi na kwa kiasi gani malighafi ya ndani na kilichotokea katika uchumi wa waliozitoa. Lazima kujadili viwanda hivi vimeingiza kiasi gani cha fedha za kigeni kwa mauzo ya nje.

Pia vimeokoa kiasi gani cha fedha za kigeni zilizokuwa zitumike kununua bidhaa ambazo sasa zinazalishwa ndani. Kwa kifupi, viwanda vinatakiwa si tu kwa lengo la kuwa na idadi kubwa bali viwe na mchango katika uchumi.

Mawasiliano: 0754 653 740

Advertisement