Klabu za usalama shuleni kinga ajali za wanafunzi

Wanafunzi wakivuka barabara ya Kawawa jijini Dar es Salaam. Kuwapo kwa klabu za usalama kwa wanafunzi shuleni, kunaelezwa kama chachu ya kupunguza ajali zinazowakabili wanafunzi barabarani. Picha na Beatrice Moses

Muktasari:

  • Wanafunzi hao waliokuwa wanakwenda kufanya mtihani katika shule ya Tumaini Junior ya Karatu, walifariki dunia wakiwa wamebakiza miezi minne kumaliza darasa la saba.

Ajali iliyosabisha vifo vya wanafunzi 32 na walimu wao wawili wa shule ya Lucky Vicent ya Arusha mwanzoni mwa Mei mwaka huu ilishtua na kuhuzunisha wengi.

Wanafunzi hao waliokuwa wanakwenda kufanya mtihani katika shule ya Tumaini Junior ya Karatu, walifariki dunia wakiwa wamebakiza miezi minne kumaliza darasa la saba.

Mengi yalisemwa kuhusu chanzo cha ajali hiyo, ikiwamo mwendo kasi wa dereva na hali mbaya ya hewa. Wengine walidai kuwa breki za gari zilishindwa kufanya kazi.

Takwimu za ajali kutoka Kikosi cha Usalama Barabarani, zinaonyesha kuwa mwaka 2015 jumla ya watoto 135 wenye umri wa kati ya miaka 7 hadi 19 walikufa kwa ajali.

Kati ya hao wavulana walikuwa ni 88 na wasichana 47. Waliojeruhiwa walikuwa ni 351 ambapo wavulana walikuwa ni 131 na wasichana 120.

Mwaka 2016, taarifa inaonyesha kuanzia Januari hadi Septemba watoto 99 wenye umri wa kati ya miaka 7 hadi 19 walikufa kwa ajali wavulana wakiwa 61 na wasichana 38. Waliojeruhiwa ni 229 wasichana 69 na wavulana 160.

Inawezekana ni kweli ajali haizuiliki lakini chanzo cha ajali kinaweza kuzuilika iwapo umakini utaongezeka kwa watumiaji wote wa vyombo vya moto.

Ni kwa sababu hiyo, tangu mwaka 2014 Baraza la ushauri la watumiaji wa Mamlaka ya usafiri wa nchi kavu na Majini (Sumatra CCC), limekuwa likisimamia klabu za usalama shuleni ili kutengeneza wajumbe wa kujitolea kutoa elimu hiyo kwa jamii.

Ofisa elimu kwa umma wa Sumatra CCC, Nicholous Kinyariri anasema klabu hizo zinashirikisha wanafunzi ambao wanasaidia kufikisha ujumbe kwa njia rahisi kwa wazazi wao, wanafunzi wenzao, ndugu jamaa na marafiki.

Anasema kuwa tayari klabu zimeanza kuonyesha mafanikio kwa kuwa wanafunzi wanachama wamekuwa, wakiongoza kwa kutoa taarifa zinazosaidia magari yanayooendeshwa kwa kuhatarisha maisha, kukamatwa na kuchukuliwa hatua.

“ Pamoja na kwamba wengi wao hawamiliki simu, lakini wamekuwa wakitumia njia ya kuomba walezi waliopo kwenye shule zao au wazazi na wasafiri wengine kuhakikisha ujumbe unafika haraka mahali husika kwa hatua mara wanapoona viashiria hatarishi vya safari,” anasema Kinyariri.

Mpaka sasa anasema kuna wanachama 2,550 katika mikoa tisa, huku mpango uliopo ukiwa ni kuongeza mkoa mwingine hivi karibuni.

Anasema klabu hizo zinakuwa na wanafunzi 50 katika kila shule iliyochaguliwa kuwa kwenye mpango huo. Wanachukua idadi hiyo ili kuhakikisha wanafikisha elimu husika kwa kiwango cha uelewa uliokusudiwa.

“Kuna gharama katika kuanzisha klabu hizi ikiwa ni pamoja na kuwezesha mafunzo husika, kugharimia shughuli zinazofanywa ikiwamo kurekodi nyimbo za kuelimisha jamii zinazopigwa kwenye radio. Lakini sisi hatujali gharama hizo, tunachotaka ni kuona elimu hii inasaidia jamii,’’ anasema.

Anabainisha mwaka jana wanafunzi wanachama 700 walihitimu masomo yao, mwaka huu watahitimu 666. Ni wanafunzi anaosema watakuwa na muda mzuri wa kuelimisha jamii.

“ Tumekusudia pia wakati wa likizo kila mwanafunzi mwanachama atoe elimu na kipeperushi kwa watu 10 na atuletee namba za simu za aliozungumza nao. Hapo unaweza kuona tutakuwa tumefikia watu wengi,” anaeleza.

Matokeo chanya

Kamanda wa Kikosi cha Usalama Barabarani, Fortunatus Muslim akizungumzia kuhusu vilabu hivyo, anasema vinasaidia katika kutoa elimu ambayo inachangia katika kupunguza ajali ambazo zimesababisha wananchi wengi kupoteza maisha, huku wengine wakipata ulemavu na hivyo kuongeza idadi ya watu tegemezi.

Anasema kikosi chake kinaendelea kujiimarisha kwa kupambana na kuwadhibiti kwa mujibu wa sheria, madereva wazembe na wanaoendesha magari mabovu.

Mkaguzi wa magari na madereva, Inspekta Yohana Mjema,anasema klabu hizo ni suala jema kwa kuwa linasaidia wanafunzi kuwa makini wanapotembea kwa miguu au wakiwa ndani ya vyombo vya usafiri.

“ Nikiwa mmoja wa askari wa kikosi cha usalama barabarani, natambua kuna maeneo ambayo ni changamoto kwa watoto hasa katika kuvuka, maana mengine bado hayajawekwa alama,” anasema na kuongeza:.

“ Hali hiyo ni hatari kwa sababu kuna madereva wazembe wanaendesha bila tahadhari yoyote hata kwenye maeneo ya shule, hivyo kugonga wanafunzi. ‘’

Othman Juma ni mwanafunzi wa kidato cha sita katika Shuke ya Sekondari ya Benjamini Mkapa ambaye ni miongoni mwa wanachama wa klabu ya usalama wa barabarani. Anaeleza kuwa vinawasaidia kujengea uelewa mzuri wa alama za barabarani na haki za msingi za vyombo vya moto.

“ Ajali zimezima ndoto za wanafunzi wenzetu wengi kwa kuwasababishia vifo na wengine ulemavu, Nani ajuae wangeendelea kuishi wangekuwa kina nani na wangesaidia kwa namna gani maendeleo ya Taifa letu,”anasema.

Juma anasema kuwa amewahi kushuhudia ajali iliyosababisha kifo cha mwanafunzi katika eneo la Mbagala Mission aliyekuwa anavuka kwenye kivuko chenye cha pundamilia. Dereva alipita kwa kasi bila tahadhari na kusababisha ajali.