Kombe la Chalenji 1981-Ilikuwa akiingia Mogella tu, kapiga bao

Muktasari:

  • Iko hivi, kulifanyika mashindano mengi, Tanzania Bara ikawa mwenyeji baada ya 1981, mwaka 1992, 2002, 2007, 2010 na 2011. Hata mwaka 2010 wakati inatwaa ubingwa, moto wake haukuwa kama ilivyokuwa mwaka 1981.

Achana na mwaka 2010 Tanzania Bara ilipotwaa ubingwa wa Chalenji kwa bao la beki wake, Shadrack Nsajigwa, shughuli ilikuwa mwaka 1981.

Iko hivi, kulifanyika mashindano mengi, Tanzania Bara ikawa mwenyeji baada ya 1981, mwaka 1992, 2002, 2007, 2010 na 2011. Hata mwaka 2010 wakati inatwaa ubingwa, moto wake haukuwa kama ilivyokuwa mwaka 1981.

Kuna mchezaji anaitwa Zamoyoni Mogella ‘Golden Boy’ anasema: “Nilipewa hilo jina mwaka 1981 nikiwa miongoni mwa wachezaji wa timu ya Taifa (Taifa Stars) kwenye mechi za Chalenji na ilikuwa zaidi dhidi ya Malawi.

“Tulikuwa tumefungwa magoli 2-1 katika ile mechi na Malawi, niliingia dakika ya 75, zikiwa zimesalia dakika mbili mpira kwisha, nilifunga goli la kusawazisha na kufanya matokeo kuwa sare ya 2-2.

“Pale ndipo nikapewa jina la Golden Boy, ilifikia mahali nikawaaminisha mashabiki kutokana na uwezo wangu kwamba, nikiingia tu lazima nifunge na kweli ilikuwa hivyo kutokana na kujitunza na kulinda kiwango changu hadi nilipostaafu,” anasimulia.

Tanzania Bara wakati huo ikiwa chini ya kocha Mjerumani, Rudi Gutendorf, na kati ya wachezaji wake, alikuwa Zamoyoni Mogella. Tanzania ikifungwa, akiingia tu lazima atikise nyavu, licha ya kuwa Wakenya walimbana tukalala 1-0 katika fainali.

Ilikuwa dakika kama 10 au 15 kabla mpira kwisha, Gutendorf alikuwa anamwinua Mogella basi uwanja mzima kelele.

Mashindano yale yalikuwa na msisimko wa aina yake, kila mmoja alikuwa nyuma ya timu ya Tanzania Bara hadi fainali dhidi ya Kenya tuliyolala kwa bao la Ouma.

Hata hivyo, mwendo wa mashindano haya umekuwa wa kusuasua kutokana na udhamini, lakini sasa kuanzia jana Desemba 3 hadi 17, mwaka huu Kenya ndiye mwenyeji wake na Tanzania Bara imepangwa Kundi A pamoja na Zanzibar, Libya, Kenya na Rwanda.

Bara jana ilikuwa ikicheza na Libya mechi ya ufunguzi wakati Kenya ilikuwa ikikwaruzana na Rwanda.

Lilikoanzia Kombe la Chalenji

Hicho kilikuwa kibwagizo cha 1981, lakini Chalenji ilianzia wapi hasa?

Tunaelezwa katika historia kuwa hii ndiyo michuano mikongwe Afrika. Ilianza mwaka 1926 wakati huo ikiitwa Gossage ambayo sasa inatimiza miaka 91.

Gossage lilikuwa jina la tajiri mmoja akimiliki kiwanda cha sabuni na ndiye alikuwa mdhamini na alikuwa akipenda soka.

Baada ya kumaliza kuizunguka Afrika Mashariki kwa usafiri wa reli enzi hizo ikiitwa, Uganda-Kenya Railways mwanzoni mwa miaka ya 1900, katika safari yake alikuwa akikutana na makundi ya watu waliokuwa wakikaakaa bila kujishughulisha baada ya kumaliza kujenga reli na shughuli nyingine.

Wengi wao walikuwa Waafrika, Waasia na Wanubi ambao ndiyo waliokuwa wakijenga reli. Gossage aliona kwamba njia pekee ya kuwafanya wafurahi ni kuwawekea michezo (mashindano).

Kwa hiyo, mwaka 1927, alianzisha michuano iliyoshirikisha mataifa ya Kenya na Uganda na alianzisha Kombe lililoitwa Gossage. Mashindano yalishindaniwa katika miji ya Kampala na Nairobi kwa miaka mingi na kuwa moja ya mashindano maarufu.

Tanganyika (sasa Tanzania) ilijiunga 1944 na kushiriki mashindano hayo kwa mara ya kwanza kuanzia 1945.

Kwa upande wa Zanzibar, iliyokuwa chini ya utawala wa Waarabu, mwaka 1948 baadaye iliingizwa na kufanya mashindano ya mataifa manne.

Mashindano yaliendelea na jina la Gossage hadi mwaka 1963 na kubadilishwa jina na kuitwa Mashindano ya Chalenji Afrika Mashariki.

Mataifa hayo manne yalishindana hadi 1973 walipokaribisha mataifa mengine.

Katika mkutano maalum uliofanyika Nairobi, Kenya wanachama hao walikubaliana kuiingiza Somalia, Zambia na Ethiopia na wakati huo sasa ndipo Cecafa ikazaliwa.

Sasa kuna mataifa saba yaliyoingia. Wakati huo na Makao Makuu ya Cecafa yalikuwa Mogadishu, Somalia kabla ya kuhamishiwa Nairobi. Michuano hiyo inaitwa Kombe la Cecafa.

Mwaka 1974, nchi wanachama walianzisha mashindano mengine, lakini haya yalikuwa katika ngazi ya klabu, uzinduzi ulifanyika Dar es Salaam na ndiyo hiyo Kombe la Kagame.

Sudan na Malawi zilijiunga Cecafa mwaka 1975. Baadaye 1981, Zimbabwe, baada ya kupata uhuru wake 1980, ikajiunga na familia ya Cecafa.

Hata hivyo, 1994 baada ya kuanguka utawala wa kidhalimu Afrika Kusini, kulianzishwa Baraza kama Cecafa la Cosafa lililokuwa likiunganisha mataifa ya Kusini mwa Afrika.

Kutokana na hali hiyo, mataifa ya Malawi, Zambia na Zimbabwe yakajiondoa Cecafa na kuanza maisha mapya ya Cosafa.

Kuondoka kwa mataifa hayo, kulifungua mlango kwa Rwanda, Burundi na Eritrea, pamoja na Djibouti kuingia Cecafa mwaka 1995.

Hiyo ilifanya mataifa ya Cecafa kufikia 11 ambayo ni: Kenya, Sudan, Uganda, Tanzania, Ethiopia, Eritrea, Zanzibar, Somalia, Rwanda, Djibouti na Burundi.

Waliotwaa mara nyingi

Mpaka sasa, Uganda Cranes imetwaa mara nyingi, 1973, 1976, 1977, 1989, 1990, 1992, 1996, 2000, 2003, 2008, 2009, 2011, 2012 na 2015.

Kenya inafuatia, 1975, 1981, 1982, 1983, 2002 na 2013 wakati Tanzania Bara imetwaa mara tatu, 1974, 1994 na 2010 sawa na Malawi 1978, 1979, na 1988 na Sudan 1980, 2006 na 2007.