MAONI: Kosa la nani, mtumbuaji au mtumbuliwa?

Waziri Mkuu wa zamani, Edward Lowassa

Muktasari:

Kweli, baada ya kuanza kazi, Rais Magufuli aliwaengua baadhi ya watendaji ambao inasemekana hawakwenda na kasi yake. Baadhi yao walikuwa na kashfa za ufisadi na wakafikishwa mahakamani, huku wengine wakiwekwa pembeni.

Tangu alipoingia madarakani mwishoni mwa mwaka 2015, Rais John Magufuli alijitambulisha kama mtumbua majipu. Alianza kutoa kauli hiyo alipokuwa akilihutubia Bunge kwa mara ya kwanza mjini Dodoma akitanabaisha kuwapo kwa uozo mwingi nchini akiufananisha na majipu.

Kweli, baada ya kuanza kazi, Rais Magufuli aliwaengua baadhi ya watendaji ambao inasemekana hawakwenda na kasi yake. Baadhi yao walikuwa na kashfa za ufisadi na wakafikishwa mahakamani, huku wengine wakiwekwa pembeni.

Basi ikawa ni utumbuaji kila kukicha, watu wakawa roho juu juu. Kimsingi tuliridhika kwamba Rais anaisafisha nchi na uchafu mwingi alioukuta.

Nakumbuka siku Rais Magufuli alipozungumza na wazee wa Dar es Salaam Februari 13, 2016 katika Ukumbi wa Diamon Jubilee, alizungumza kwa uchungu kuwa nchi imeoza kila mahali na akasisitiza azma yake ya kuendelea kuisafisha.

Hata katika mkutano wa Bodi ya Makandarasi uliofanyika Mei 26, 2016 Rais pia alirudia kauli zake hizo za uozo serikalini. Uozo katika elimu, uozo katika sekta ya ujenzi, uozo katika uajiri na mengineyo mengi.

Lakini pamoja na yote hayo, kulikuwa na utata ukiendelea chini kwa chini. Siku Rais anawahutubia wazee wa mkoa wa Dar es Salaam, alieleza mkakati wake wa uteuzi wa wakuu wa mikoa na kumsifia aliyekuwa mkuu wa wilaya ya Kinondoni wakati huo, Paul Makonda huku akisema watu wasishangae akipanda cheo.

Kweli, baada ya mwezi mmoja, Makonda akawa Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam. Ili kuonyesha kuwa cheo hicho hakikuwa kwa bahati mbaya, Rais Magufuli alinukuliwa akieleza sababu ya kumweka Makonda katika nafasi hiyo, siku alipozindua mitambo ya Kinyerezi II Machi 16, 2016.

Kwanza alimpongeza Waziri wa Nishati na Madini, Profesa Sospeter Muhongo akisema ndiyo maana amemrudisha kwenye wizara hiyo.

“Ndiyo maana Profesa Muhongo niliamua kukurudisha hapa; na saa nyingine vitu vizuri vinapigwa vita, hata Makonda alikuwa anapigwa vita nikamwambia anabaki hapa hapa Dar es Salaam, ili mbaya wao wamwone yuko hapo, tena akiwa bosi zaidi,” alisema Rais Magufuli.

Kauli hiyo pamoja na nyingine nyingi za Rais Magufuli kuhusu Makonda zinafanya watu wajiulize mambo mengi. Hivi Rais anateua mtu fulani ili kuwakomoa baadhi ya watu? Je, alijiridhisha na sifa za elimu, uzoefu na weledi, au ni kukomoa watu tu?

Kwanza tujikumbushe, jinsi Makonda alivyopanda vyeo hadi akafikia hapo alipo. Akiwa mmoja wa viongozi wa Shirikisho la Vyuo Vikuu (Tahliso) na Umoja wa Vijana wa CCM, Makonda alionekana kuwa shupavu kwa kutoa matamko makali.

Wakati uchaguzi mkuu wa 2015 ukikaribia kulikuwa na makundi ya wagombea. Makonda alijitanabaisha kwamba hapatani na kundi la Waziri Mkuu wa zamani, Edward Lowassa, kwa hiyo alitoa matamko ya kumponda wazi wazi.

Makonda pia alishiriki kwenye Bunge Maalumu la Katiba mwaka 2014 na alikuwa mstari wa mbele katika kupinga Rasimu ya Mabadiliko ya Katiba, maarufu kama Rasimu ya Warioba.

Tunajua jinsi ambavyo Bunge lile lilivyogawanyika baada ya wajumbe wa kambi ya upinzani kususa na kuunda Umoja wa Katiba ya Wananchi (Ukawa) huku wajumbe wa CCM na baadhi ya taasisi wakiunda Katiba Inayopendekezwa.

Baada ya pale, wajumbe wa iliyokuwa Tume ya Mabadiliko ya Katiba wakiongozwa na aliyekuwa Mwenyekiti wao, Jaji Joseph Warioba walipoanza kutoa mihadhara ya Katiba hiyo.

Katika moja ya mihadhara iliyofanyika Dar es Salaam, vurugu zilizuka baada ya baadhi ya vijana wanaodhaniwa kuwa wa CCM wakiongozwa na Makonda kunyanyua mabango ya kuupinga.

Makonda alionekana kwenye picha za magazeti wakati Jaji Warioba akishambuliwa. Watu wakalalamika, wakitaka achukuliwe hatua kwa kitendo kile. Lakini wakubwa wakaziba masikio, tena kwa jeuri kabisa, akateuliwa kuwa mkuu wa wilaya.

Makeke yakaendelea. Makonda akiwa DC alianza kujitutumia kwa kutoa ahadi hizi na zile ambazo mpaka leo hazijatekelezwa. Watu wakaendelea kumnyooshea kidole, lakini wakubwa wakaziba masikio, hadi Rais Magufuli alipoingia madarakani na kumwona Makonda kama jembe lake. Kila analofanya linapata sifa za Rais.

Hata hivyo, ndege mjanja hunasa kwenye tundu bovu. Watu wameibua kashfa ya vyeti vya Makonda wakidai alitumia jina la mtu mwingine katika safari yake ya masomo. Ni zaidi ya mwezi sasa, Makonda amepata kigugumizi. Je, anasingiziwa? Kama anasingiziwa, mbona wasingiziaji hawakamatwi na kushtakiwa?

Watu wameshtakiwa kwa kughushi vyeti, watumishi wa umma wamefukuzwa kazi na wengine wamekimbia kazi kwa kuhofia adhabu baada ya uhakiki wa vyeti, lakini huyu anadunda.

0754 897 287