Kuhama vyama na fikra sahihi za wanasiasa

Muktasari:

Chini ya maneno hayo, aliweka mwongozo wenye sehemu tatu kwa wanasiasa kuhusu vyama vyao.

Gwiji wa siasa za Canada na Waziri Mkuu kwa vipindi vingi zaidi nusu ya kwanza ya Karne ya 20, William King maarufu kama Mackenzie King, alipata kuandika kanuni kuhusu wanasiasa na vyama vyao, aliandika; “My political party is not my religion and it shouldn’t be yours either”, yaani chama changu cha siasa si dini yangu na hakipaswi kuwa dini yako pia.

Chini ya maneno hayo, aliweka mwongozo wenye sehemu tatu kwa wanasiasa kuhusu vyama vyao.

Mosi, alisema “chama changu cha siasa si mwokozi wangu”. Wakristo huamini uwepo wa mwokozi ambaye ni Yesu Kristo. King anataka wanasiasa wasivichukulie vyama vyao sawa na Yesu Kristo.

Pili, “chama changu cha siasa hakinipendi”. Hili ni darasa kuwa hakuna chama cha siasa chenye kumpenda mtu. Vyama huhitaji watu ili vijijenge kuwa vikubwa lakini pale inapobidi chama kinaweza kumjeruhi yeyote kwa ajili ya kutimiza malengo yake.

Tatu; Chama changu hakina uzima wa milele. Hakuna chama ambacho kinatoa uhakika wa uzima wa milele kwa mwanachama wake. Hivyo, kila mtu kwenye chama ni wa kupita tu, leo upo kesho haupo. Hayupo ambaye uhai wake duniani utarefushwa na chama chake.

Mwongozo huo wa King ukibebwa na kila mwanasiasa kama kanuni, utaokoa kundi kubwa la watu ambao kwao huwa waaminifu kwa vyama na kujenga chuki na watu wengine kwa kudhani kwamba pumzi zao za uhai zinafungamana na kadi zao za uanachama.

Kila mwanachama, hasa kijana ambaye ndiye yupo kwenye kundi lililo na idadi pana ya watu wenye deni kubwa la kuishi, hupaswa kufahamu kuwa kadi ya uanachama haitoi oksijeni, hivyo wanapoielekea siasa lolote linaweza kutokea kwenye vyama vyao, ama kutimuliwa au kuhama.

Katika vyama inaweza pia kutokea kukimbiwa na watu ambao inaaminika ndiyo uhai wa chama au kuwa na viongozi ambao hukubaliani na mitazamo, hivyo ukajikuta huna furaha. Ukifika hapo kumbuka mambo manne; chama cha siasa yo dini wala mwokozi, hakina uzima wa milele na hakimpendi mtu.

Hiyo ndiyo sababu kati mwaka 1975 mpaka 1980 kiliundwa chama cha Zanu Zimbabwe na baadaye Zanu-PF kutoka mwaka 1980 mpaka Novemba 2017, Robert Mugabe ndiye aliyeaminika kuwa ni uhai wa chama, lakini sasa Zanu-PF wanamuona Mugabe sawa na kifo cha chama na wamemtimua.

Siasa ni malisho mema

Mwanasiasa anapopata wazo au kushiriki wazo la kuasisi chama, moja kwa moja huamini kuwa chama hicho kwake kitakuwa malisho mema. Sawasawa na ambaye hujiunga na chama hai ni baada ya kuvutiwa na sera pamoja na falsafa zake kuwa ndani yake malisho mema yatapatikana.

Mjadala wa malisho mema upo katika makundi mawili; kwanza ni mvuto wa kiitikadi, kisera na kifalsafa kwamba chama kinaweza kujibu matatizo ya watu, hivyo mwanachama anakiasisi au anajiunga nacho ili kushiriki kuyaendea matarajio yake.

Pili ni fursa binafsi, kwamba mwanachama anajiunga na chama kwa sababu ameona mwanya wa uongozi, kwamba atapata fursa ya kugombea cheo anachokitaka au ataweza kukitumia chama kwa vyovyote vile kutimiza malengo yake binafsi. Hayo ni malisho mema katika sura ya masilahi binafsi.

Ufafanuzi wa makundi hayo mawili unakuleta kwenye ukweli huu, kwamba watu wanajiunga au wanaasisi vyama vya siasa kwa sababu mbili kuu, ama kuviendeleza vyama ili vifikie malengo mazuri yaliyomo kwenye maandishi au kutafuta fursa za kuongoza au kutimiza matarajio binafsi.

Mantiki ya hapo ni kuwa mtu anaweza kubaki kwenye chama, kuondoka na kuhamia kwingine kwa sababu za malisho mema. Mwanachama anabaki kwa imani kwamba ama chama chake ndicho chenye majibu ya watu au bado anaona fursa ndani yake, hivyo aondoke azipoteze?

Kumbe sasa anaweza kuwapo mtu anashambulia wenzake wenye kuhama vyama kwa sababu yeye yupo pazuri au imani yake ni kamili kwamba chama chake ndicho chenye majibu ya msingi juu ya matatizo ya watu na nchi kwa jumla. Na anayehama anakuwa anaona aendako ndiko pazuri.

Yule anayeachana na siasa labda awe mzee aliyeshiriki muda mrefu lakini kama umri wake bado unadai, huyo anakuwa amekata tamaa ya kuendelea, kwamba ama haoni chama chenye matarajio ya utumishi wa watu (kama anatafsiri siasa ni huduma) au hakuna chama chenye masilahi yake (kwa tafsiri ya siasa masilahi).

Wimbi la sasa

Hivi sasa kuna wimbi kubwa la wanachama na viongozi wa kisiasa kuhama vyama, wengi zaidi wakitoka upinzani kujiunga CCM. Ukishiba nadharia ya malisho mema kwenye siasa, hutawabeza, maana nao wanaangalia kilicho bora kwao.

Waliokuwa wanachama na viongozi wa ACT-Wazalendo waliohamia CCM ni Profesa Kitila Mkumbo, Samson Mwigamba, Albert Msando na Edna Sunga, wakati kutoka Chadema kwenda CCM ni Lawrence Masha, David Kafulila na Patrobas Katambi ambaye alikuwa mwenyekiti wa Baraza la Vijana Chadema (Bavicha).

Sawa tu na aliyekuwa Mbunge wa Singida Kaskazini (CCM), Lazaro Nyalandu ambaye alipata kuwa Waziri wa Maliasili na Utalii, aliyeamua kuhamia Chadema hivi karibuni na kujiuzulu ubunge, alitoa sababu zake kuhusu umuhimu wa nchi kuwa na Katiba Mpya ili kuimarisha utawala bora.

Tuchambue; Nyalandu ameona CCM, ambacho ni chama kilichomwezesha kupata ubunge, hakina malisho mema upande wa utawala bora, demokrasia na upatikanaji wa Katiba mpya, hivyo ameona ahame. Kama kuna sababu za ndani hizo ni zake binafsi.

Masha alisema amehama Chadema kwa sababu ameona upinzani hakuna mipango mahsusi ya kushika dola. Tafsiri yake ni kuwa yeye kwake malisho mema ni kushika dola, hivyo amerejea CCM ambacho kipo madarakani ili kuyaelekea matarajio yake kisiasa.

Kafulila alisema anajivua uanachama wa Chadema kwa kuwa wapinzani wamepoteza shabaha ya kukabiliana na ufisadi. Bila kusema kama atajiunga na CCM au la, alisema anaungana na Rais John Magufuli kwa sababu anapambana na ufisadi. Kumbe kwa Kafulila malisho mema ni kupigana vita dhidi ya ufisadi?

Profesa Kitila alisema sababu ya kwenda CCM ni baada ya kuona chama kimekuwa cha wanachama, vilevile kinamvutia kiitikadi na sera za kiuchumi. Ukifika hapo unajua kuwa tafsiri ya malisho mema kisiasa kwa Kitila ni chama kuwa na itikadi, vilevile sera bora za kiuchumi.

Kitila ni mmoja wa waasisi wa ACT-Wazalendo, hivyo kwa tafsiri hiyo unaweza kujiuliza je, chama hicho ambacho alishiriki kukijengea misingi hakina itikadi bora ambazo zingembakisha? Hakuna sera nzuri za kiuchumi? Au vyote vipo ila aliona giza kwa chama kushika dola hivi karibuni?

Katambi alisema amehama kwa sababu kijana ukiwa upinzani unatumiwa kama karai, kwamba umuhimu wake huonekana wakati wa ujenzi tu, baada ya ujenzi kukamilika karai hutelekezwa. Hapo ni sawa na kusema malisho mema ya Katambi ni kijana kuthaminiwa.

Msando na Mwigamba walijielekeza kulekule kwenye utawala bora na namna Rais Magufuli anavyopambana na ufisadi. Unaweza pia kutafsiri eneo hilo kuwa ndilo lenye kubeba mtazamo wa malisho mema kisiasa ambayo Msando na Mwigamba wanaamini.

Tutanue fikra

Rejea tafsiri ya malisho mema kisiasa kwamba yupo mwenye kutazama misingi ya chama kuelekea kuihudumia jamii, mwingine anatazama fursa ya kuongoza. Hapohapo elewa kuwa yupo anaweza kuhama chama kwa kuona chama kina misingi lakini hakina msuli wa kupambana kushika dola.

Ukisogea mbele ya hapo unapata jawabu kwamba yupo ambaye anakuwa na fursa nzuri kwenye chama alichopo lakini anaamua kwenda kubanana na watu wengine kwa sababu anaona kwamba chama anachohamia kina msuli wa kupambana na anaweza kupata fursa.

Rejea tena kwenye mwongozo wa Mackenzie King kuwa chama si dini, mwokozi wa maisha, hakimpendi mtu wala hakitoi uzima wa milele, kwa hiyo ukiona mtu anahama ujue anatafuta malisho mema. Hupaswi kumshambulia kuwa ni msaliti kwa sababu kila mmoja anatazama mambo kivyake.

Mbunge wa zamani jimbo la Kasulu Mjini (NCCR-Mageuzi), Moses Machali alipohamia CCM mwaka jana kutokea ACT-Wazalendo, Kafulila alisema Machali hakuwa mpinzani halisi, hivyo bora alivyojiunga CCM, kisha akasema safari ya ukombozi ni ngumu, kwamba wachache tu watafika mwisho.

Katika maelezo yake, Kafulila alijitabiria kuwa mmoja wa wanasiasa ambao wangefika mwisho katika kile alichokiita ni safari ya ukombozi. Hata alipohama NCCR-Mageuzi kujiunga na Chadema alisema chama hicho ndicho chenye uhakika wa kushika dola.

Hoja za Machali alipojiunga CCM ni sawa na alizotoa Kafulila, kwamba Rais Magufuli ndiye mpambanaji wa ufisadi. Ulinganisho huo usikufanye umuone Kafulila sawa na aliyemcheka mlevi kilabuni kisha naye akavuta kiti na kuagiza kinywaji, bali ukutanue kifikra.

Kwamba kwenye siasa kila mmoja huangalia matarajio anayoyapa kipaumbele. Ni vizuri kumheshimu mtu na uamuzi wake. Baba wa Taifa Mwalimu Julius Nyerere alisema CCM si mama yake, hivyo angeweza kuhama.

Hata hivyo hili si la kuacha kulisema, maana lina msisitizo wake, kwamba ni vigumu mno mtu kukiri kuwa amehama kwa sababu ya maslahi binafsi, yaani malisho mema ya tumbo lake, isipokuwa atasingizia hoja nyingine. Siri ni yake.