Kujisomea vitabu kutapunguza makelele

Muktasari:

Umeshatazama filamu hasa inapofika vipande vya msutano au maombezi. Kama ni mfuatiliaji, basi inabidi tu ujichagulie mtu mmoja wa kumsikiliza ikiwa unataka walau kuambulia kitu, kwa sababu wote wanaongea tena ovyo.

Maisha yameshakuwa kelele tupu na kimya imeshakuwa bidhaa adimu hasa katika maeneo ya mijini.
Ukiangalia muvi kelele, nyimbo kelele,  vyombo vya usafiri kelele tu…dah tuanze kupiga kelele, haya makelele yapungue.
Umeshatazama filamu hasa inapofika vipande vya msutano au maombezi. Kama ni mfuatiliaji, basi inabidi tu ujichagulie mtu mmoja wa kumsikiliza ikiwa unataka walau kuambulia kitu, kwa sababu wote wanaongea tena ovyo.
Kuna wakati mimi huwabeza wazee wanaosema muziki ulikuwa zamani siku hizi kelele tu, lakini kuna wakati nahisi kama kuna ukweli hivi.
Umesimama kwenye kituo cha daladala, kuna kila aina ya kelele, makondakta wakishindana kupiga debe, huku wanakuzonga huku na kule. Muuza juisi na maji naye anaitisha wateja wake, pembeni kuna bonge la spika la muuza dawa za kuua kunguni na mende.
Huku unatoka jasho na uchovu tele, unaamua kupanda moja kati ya daladala ili angalau upumzike, ingawa limejaa unaamua tu kupanda hivyo hivyo.
Unaingia ndani ya daladala moja, dereva amefungulia redio mpaka mwisho na nyimbo zinazopigwa humo ni za kuumiza kichwa kwani mabati yanagonga ile mbaya.
Daladala linaondoka, lakini barabara yenyewe ni makorongo matupu na kwa kuwa hilo daladala ni mkweche, vyuma vinagongana, haifai. Kama hiyo siyo mbaya sana, jirani yako anapokea simu, naye inambidi azungumze kwa sauti ya juu kwa sababu ndani utulivu ziro.
Mwingine naye anampigia simu mfanyakazi wake nyumbani, anaanza kumpa maelekezo ya kupika mboga siku hiyo.
Mwingine anakumbuka dakika zake alizojiunga jana yake, muda unakaribia kuisha hivyo anaangalia kwenye orodha ampigie yoyote ili dakika zisipotee bure.
Ataongea hapo kwa sauti ya juu hata nusu saa na maongezi yenyewe ni ya kuchefua. Mwingine anampigia mwenzake kumweleza kuhusu nyumba yake anayoijenga huko Goba.
Siyo ajabu, unaweza kumsikia mtu kwenye simu akisema: “Kwa kweli hawa wenye nyumba wamenichosha ntahamia tu hata kama haina madirisha.”  
Umeshachoshwa na makelele, unajiuliza kuna umuhimu gani wa kuzungumza mambo kama hayo ndani ya vyombo vya usafiri wa umma kama siyo kupigiana kelele tu.
Kwa wenzetu, muda unapokuwa katika usafiri wa umma ndiyo wa kujisomea magazeti au kitabu