Kukaimu muda mrefu kunapunguza ufanisi wa watumishi serikalini

Thursday October 19 2017

Joseph Alphonce  ni Mtakwimu na Ofisa Mipango.

Joseph Alphonce  ni Mtakwimu na Ofisa Mipango. Anapatikana kwa 0685214949/0744782880. 

By Joseph Alphonce

Kila iitwapo leo watumishi kadhaa wa umma wanaondoka katika nafasi zao za utendaji kwa sababu mbalimbali. Ama kwa kustaafu, kufariki, kusimamishwa, kufukuzwa au ugonjwa wa muda mrefu.

Kati ya wanaoachia nafasi baadhi ni watoa maamuzi ya mwisho au washiriki kwenye mfumo wa kutoa maamuzi ya serikali ili kuwaletea wananchi maendeleo. Mtumishi wa umma anapoondoka Serikali huteua mtu mwingine kujaza nafasi iliyoachwa wazi.

Kama mtumishi aliyetueliwa hajafikia cheo cha anayeondoka hukabidhiwa ofisi kwa masharti ya kukaimu kwa muda usiozidi miezi sita au vinginevyo kutegemea na nafasi husika.

Ndani ya kipindi hicho kama mtumishi atakidhi vigezo na masharti hupewa barua ya kuthibitishwa vinginevyo huondolewa na anayekidhi kuletwa kuendele ana majukumu ya nafasi husika.

Tatizo si mtumishi kukaimu bali kufanya hivyo kwa muda mrefu bila kuthibitishwa. Ripoti kadhaa za Mkaguzi na Mdhibiti wa Hesabu za Serikali (CAG) zimekuwa zikihoji na kuonyesha utendaji dhaifu unaofanywa na watumishi wanaokaimu kwa muda mrefu.

Kuna faida za kuwathibitisha wanaokaimu ndani ya muda mfupi ikiwamo kuongeza ufanisi katika utekelezaji wa majukumu, uwajibikaji na uzalendo.

Kuthibitishwa kunaendana na mabadiliko ya mshahara na marurupu, mtumishi anapolipwa stahiki zinazoendana na majukumu yake humfanya awekeze maarifa na nguvu kufikiri namna bora ya kutatua changamoto za wananchi.

Maamuzi anayochukua mtumishi aliyethibitishwa na kaimu ni tofauti. Anayekaimu bado ana hofu na hajui hatima yake. Hivyo wakati mwingine hujikuta akitenda kuwafurahisha watu fulani ili iwe rahisi kuthibitishwa.

Kwa sasa Serikali imezuia kwa muda ajira mpya, uteuzi na kupanda madaraja ili ‘kusafisha taarifa’ za watumishi. Kusafisha huko ni kuzuri kwani kumebaini watumishi wasio na sifa na vigezo vinavyostahili.

Haya ni mafanikio yanayostahili kupongezwa kwa sababu mchakato mzimma umeokoa fedha za Serikali ambazo zitaelekezwa kutatua changamoto za wananchi.

Wakati upande mmoja ajira mpya, uteuzi na kupanda madaraja kumesimamishwa kwa muda upande mwingine watumishi wanastaafu, wanafariki, wanasimamishwa, wanafukuzwa na wengine wanaugua kwa muda mrefu.

Hii inasababisha nafasi nyingi za maamuzi hasa katika Serikali za Mitaa kukaimiwa na watu ambao wakati mwingine hawakidhi kuwapo kwenye nafasi hizo hivyo kukwamisha utekelezaji wa miradi ya maendeleo kwa ufanisi na kiwango kinachotarajiwa.

Kila shughuli au mradi una muda wa kuanza na kuisha. Ni vyema Serikali kwa muda muafaka ikaondoa zuio ililoliweka la kuajiri, kuteua na kupanda madaraja. Kuzuia matukio haya kwa muda mrefu kuna faida chache na hasara nyingi.

Hasara kadhaa zinazotokana na zuio hilo ni pamoja na kuongezeka kwa vijana wasio na ajira nchini maana kila mwaka vijana wanahitimu. Ukosefu wa ajira kwa zuio ambalo haijulikani litaisha lini lina madhara kisiasa, kiuchumi na kijamii.

Pia uwajibikaji, ufanisi na motisha vinapungua kwa kuzuia kupanda madaraja kwa watumishi ambao ni watekelezaji wakuu wa maagizo na maelekezo yote ya Serikali.

Watumishi hujitahidi kufanya kazi kwa bidii na uaminifu wakiamini siku moja watateuliwa kushika wadhifa fulani ikiwemo ukuu wa idara au ukurugenzi hivyo kuzuia uteuzi kunapunguza morali na ufanisi kwa wengi.

Watumishi waliopo Serikali za Mitaa (Tamisemi) ndio watekelezaji wakuu wa shughuli za Serikali ikiwemo afya, elimu, maji, barabara za mikoa na wilaya, kilimo, mifugo, uvuvi na ardhi.

Unapokuwa na mkuu anayekaimu kwa muda mrefu huku akitekeleza majukumu kwa mshahara na marupurupu yasiyolighana na nafasi husika inadhorotesha ufanisi na ubora wa kazi.

Bila ya kuapo kwa kada ya watumishi wa umma wenye weledi stahiki, uteuzi unaozingatia sifa za utendaji na wanaolipwa vizuri matumizi ya takriban Sh600 bilioni za mishahara kila mwezi hayatakuwa na tija.

Kada pekee inayoweza kuondoa suala la watumishi hewa na wasio na sifa wala vigezo Serikalini ni ofisi ya rasilimaliwatu. Kimsingi hii ndio kazi yao, haiwezekani taasisi ya umma ikawa na watumishi hewa halafu ofisa utumishi asifahamu lolote.

Ndio kada inayohusika na kusafisha taarifa wa watumishi kila wakati. Ni lazima kuwekeza vya kutosha kwa kada hii ili kupata matunda stahiki.

Mfumo wa taarifa za watumishi ‘Lawson’ kwa kiasi kikubwa unasaidia kudhibiti watumishi wasio na sifa kuingia kwenye utendaji wa Serikali. Mifumo hii inategemea uadilifu na uzalendo wa waingiza taarifa kutoka idara ya utumishi.

Hawa, kwa kushirikiana na idara nyingine, huwa na maslahi binafsi kufanikisha udanganyifu huo unaolitia taifa hasara bila sababu za msingi.

Mwandishi ni Mtakwimu na Ofisa Mipango. Anapatikana kwa namba 0685214949/0744782880.

Advertisement