UCHAMBUZI: Kukua kwa uchumi, maendeleo ya kiuchumi ni dhana mbili tofauti

Muktasari:

Hilo linawezekana endapo kukua huko kunawanufaisha wachache na kuwaacha wengi wakiishi kwenye lindi la umaskini. Hili pia linaweza likasababishwa na kuimarika kwa sekta moja tu ambayo haigusi maisha ya wengi, mfano utalii kwa hapa nchini. Hilo likitokea, hata uchumi ukisemwa unakua kwa kasi ya kupaa, wananchi wataendelea kuwa maskini.

Ni vigumu kwa maendeleo ya kiuchumi kutokea bila ya kukua kwa uchumi. Ni lazima uchumi uongezeke kwanza ndipo maendeleo ya kiuchumi yapatikane. Lakini, kukua kwa uchumi siyo lazima kulete maendeleo. Uchumi unaweza kukua lakini usiambatane na maendeleo ya kiuchumi.

Hilo linawezekana endapo kukua huko kunawanufaisha wachache na kuwaacha wengi wakiishi kwenye lindi la umaskini. Hili pia linaweza likasababishwa na kuimarika kwa sekta moja tu ambayo haigusi maisha ya wengi, mfano utalii kwa hapa nchini. Hilo likitokea, hata uchumi ukisemwa unakua kwa kasi ya kupaa, wananchi wataendelea kuwa maskini.

Ninachomaanisha hapa ni kwamba, takwimu za kukua kwa uchumi peke yake, siyo kitu muhimu kwa walalahoi walio wengi, japo ni muhimu. Cha msingi ni matokeo ya kukua huko kwa wananchi. Kiasi cha maendeleo ya kiuchumi yaliyotokana na kukua huko katika kipindi kinachozungumzwa ndilo suala muhimu zaidi.

Kukua kwa uchumi kunahusishwa zaidi na ongezeko la Pato la Taifa (GDP) au kipimo cha uzalishaji mali, bidhaa na huduma katika nchi nzima kwa kila mwaka.

Maendeleo ya kiuchumi yana uhusiano na ubora wa maisha ya watu katika nyanja mbalimbali; huduma za afya na kupungua kwa maradhi, elimu na kupungua kwa kiwango cha ujinga na kupungua kwa umasikini.

Uchumi wa nchi unaweza kuwa unakua kwa kiwango cha juu lakini wananchi bado ni masikini. Siyo jambo la ajabu, inatokea. Hilo litatokana na ukuaji huo ulimnufaisha nani katika nchi husika au ulitokana na sekta zipi na idadi ya wananchi wanaojishughulisha nayo.

Pamoja na mambo mengine, kipimo cha maendeleo ya kiuchumi kinaangalia mafanikio yaliyopatikana kwenye pato la mtu mmoja kwa mwaka (per capital income), ubora wa elimu au kiwango cha kujua kusoma, kuandika na kuhesabu, ubora wa huduma za afya, makazi bora, utunzaji wa mazingira na umri wa kuishi.

Kipimo kingine Human Development Index (HDI), ambacho hulinganisha maendeleo baina ya mataifa duniani hutumika pia. Kwa mfano, kwa mwaka 2014, Tanzania ilishika nafasi ya 151 miongoni mwa nchi 188 wanachama wa Umoja wa Mataifa (UN). Kipimo hiki kinaangalia mambo matatu muhimu; umri wa mtu kuishi duniani, ubora wa elimu na pato la mtu kwa mwaka.

Kwa upana huo, suala la maendeleo ya kiuchumi huibua mijadala mikali katika ulingo wa kisiasa, hususani miongoni mwa vyama shindani kila linapokuja suala la kuuza sera za kiuchumi.

Kwa upande mwingine, uchumi unaweza kukua, lakini watu wengi bado wasione ongezeko lolote halikugusa wala kuboresha maisha yao ya kila siku. Kama takwimu zitatokana na uchumi unaoshikiliwa na watu wachache au kukithiri kwa vitendo vya rushwa, wananchi hawawezi kuona chochote.

Inaweza ikatokea pia kuwa sekta inayochangia zaidi inamilikiwa na wawekezaji wa nje ambao kwa kutumia sheria dhaifu zilizopo kwenye mataifa mengi ya Afrika wanalipa kodi ndogo na kupeleka fedha nyingi kwenye nchi zao.

Inaweza ikatokea, uchumi unakua, lakini kiasi kikubwa cha fedha kinatumika kwenye shughuli za ulinzi na usalama. Kwa sababu bidhaa na huduma nyingi za majeshi zinawahusu wananchi wachache bado maisha ya wananchi yataendelea kuw amagumu. Kwa hiyo, wakati ukuaji wa uchumi unahusisha zaidi takwimu za GDP kwa upande mwingine, maendeleo ya kiuchumi, yanahusiana zaidi na uboreshaji wa hali ya maisha ya watu katika nyanja mbalimbali.