Kumlea mtoto bila viboko inawezekana

Muktasari:

  • Zifuatazo ni nyenzo kuu nne za kujenga msingi bora wa malezi yenye uadabishaji chanya na ambayo hufikia malengo endelevu ya mzazi kwa mtoto wake.

Malezi bora huhitaji msingi imara kama ilivyo kwa ujenzi wa nyumba. Leo tunaangazia swala la viboko katika malezi na kujielimisha kama inawezekana kulea bila viboko. Haishangazi kuwaona wazazi katika jamii yetu wakichapa fimbo, kwenzi, kumkaripia kwa sauti ya juu (kufoka) na hata kumtusi mtoto wao. Tofauti na dhana iliyojengeka kuwa namna hii mtoto anapata kujifunza utii, watalaamu wa makuzi wanatwambia kuwa mtoto anaweza kutii bila viboko. Hii inajulikana kama uadabishaji chanya unaojengwa kupitia mahusiano mazuri baina ya mtoto na mlezi wake.

Zifuatazo ni nyenzo kuu nne za kujenga msingi bora wa malezi yenye uadabishaji chanya na ambayo hufikia malengo endelevu ya mzazi kwa mtoto wake.

Kuwa na malengo ya muda mrefu juu ya mtoto wako. Kufanikisha kumkuza mtoto tangu anapozaliwa hadi utu-uzima ni kazi ya kujivunia, lakini wazazi wengi huianza safari hii bila kufikiria ni upi mwisho wa safari hii? Ukifanikiwa kujua malengo ya muda mrefu kwa mtoto wako, wewe mwenyewe utakuwa mfano wa kuigwa. Kama unataka mtoto wako awe mwema na mwenye msaada kwa jamii, anayeweza kufikiri, msikivu, asiye mkorofi, mwenye upendo kwa watu wote na mengine kama hayo lazima utembee katika nyayo hizo. Akuige. Ukipanda mahindi huvuni viazi.

Mtengenzee mtoto mazingira ya upendo na mawasiliano. Upendo na mawasiliano kati ya mzazi na mtoto kwa jamii yetu huishia mara nyingi umri wa kuhudhuria kliniki (miaka5). Ili kumkuza mtoto mwema unatakiwa kumuonyesha upendo wakati wote na kumpatia taarifa muhimu hasa kuhusu mabadiliko ya kimwili pale anapoelekea balehe, mfanye mtoto awe rafiki na kwamba kuwa mzazi sio lazima mtoto akuogope bali akuheshimu na kukuthamini.

Elewa watoto wanavyofikiri na kuhisi juu ya mambo mbalimbali. Jipe muda kuelewa hisia na fikra za watoto juu ya mambo mbalimbali kulingana na umri wao. Utakuta mzazi anampiga mtoto mchanga/mdogo kisa analia pasi kikomo usiku na mchana bila ya kujiuliza iwapo mtoto anaelewa hata sababu ya kupigwa? Yapo makosa mengi watoto wanayofanya katika umri tofauti na wazazi hutumia vipigo kama namna ya kuwaadabisha bila ya kujua sababu za watoto (kiumri) kufanya wafanyayo. Vipigo namna hii vinawatengenezea tabia ya kuwa wakorofi na kuamini kuwa matatizo hutatuliwa kwa njia ya ugomvi. Usugu!

Adhabu ni malengo ya muda mfupi. Uelewa juu ya changamoto mbalimbali zitokanazo na hatua za makuzi ya mtoto na namna ya kuzikabili kwa kutumia mbinu rafiki na si viboko ni muhimu kwa mzazi. Utakubaliana nasi kuwa viboko vinamneemesha mzazi/mlezi zaidi hata ya mtoto kwani anapata kutuliza hasira zake huku mtoto akiambulia mafunzo hafifu mno. Kutumia adhabu katika kumuadabisha mtoto hutimiza malengo ya muda mfupi na hulenga katika kutimiza matakwa ya mzazi ya muda huo na si malengo endelevu.

Adhabu za viboko na nyinginezo hugusa zaidi mwili tu na husahaulika kwa muda mfupi wakati kuadabisha kwa njia rafiki hugusa ubongo moja kwa moja na humpa mtoto nafasi ya kufikiri na kujifunza kutokana na makosa. Malezi yanayolenga kukuza mtoto ambaye mzazi anategemea aje kuwa mtu mzima muwajibikaji na anayekubalika kwenye jamii hayana budi kuzingatia nyenzo hizi.