Kuna haja ya kufundisha ujasiriamali shuleni, vyuoni

Mwanafunzi akitengeneza Kompyuta. Picha ya Maktaba

Muktasari:

  • Hii ni kutokana na historia ya nchi yetu hasa baada ya kupata uhuru, kwani tuliamua kufuata siasa ya ujamaa na kujitegemea kupitia Azimio la Arusha.
  • Siasa ya ujamaa na kujitegemea haikushadidia ujasiriamali kwa vile ulifananishwa na ubepari ambao ulichukuliwa kama unyama na wale wote waliokuwa wanajihusisha na shughuli za kijasiriamali hasa biashara katika kipindi hicho walionekana kama “wanyama” au watu walikuwa waliochepuka njia kuu ambayo ilikuwa inaaminiwa na jamii ya wakati huo.

Elimu ya ujasiriamali katika nchi yetu haina umri mkubwa kama zilivyo taaluma nyingine kama vile lugha, historia, siasa na sayansi.

Hii ni kutokana na historia ya nchi yetu hasa baada ya kupata uhuru, kwani tuliamua kufuata siasa ya ujamaa na kujitegemea kupitia Azimio la Arusha.

Siasa ya ujamaa na kujitegemea haikushadidia ujasiriamali kwa vile ulifananishwa na ubepari ambao ulichukuliwa kama unyama na wale wote waliokuwa wanajihusisha na shughuli za kijasiriamali hasa biashara katika kipindi hicho walionekana kama “wanyama” au watu walikuwa waliochepuka njia kuu ambayo ilikuwa inaaminiwa na jamii ya wakati huo.

Wafanyakazi serikalini walikuwa hawaruhusiwi kujihusisha na biashara. Shughuli za ujasiriamali zilionekana kufanywa na watu ambao hawakuwa na elimu ya kutosha kupata ajira na wageni hasa kutoka bara la Asia kama vile Wahindi.

Hata hivyo, kutokana na hali halisi ya maisha katika nchi yetu na dunia kwa jumla, kuanzia miaka ya katikati ya 2000, nchi ilianza taratibu kuingiza elimu ya ujasiriamali katika elimu ingawa haikuwekewa kipaumbele.

Kwa sasa elimu ya ujasiriamali imekuwa kama wimbo wa taifa si shuleni na vyuoni, bali hata katika sekta ambazo si rasmi kama ambavyo tumekuwa tukishuhudia matangazo mbalimbali yanayopigia debe uendeshaji wa elimu ya ujasiriamli katika makundi mbalimbali ya jamii yetu.

Kutokana na wanajamii na taifa kwa jumla kuanza kuona elimu ya ujasiriamali kama mwarobaini wa matatizo yanayowakabili, lengo la makala haya ni kuelezea umuhimu wa elimu ya ujasiriamali katika shule na vyuo kama njia mojawapo yenye kuonyesha jinsi elimu ya ujasiriamali inavyoweza kusaidia jamii na taifa kwa katika kuleta maendeleo endelevu.

Ujasirimali ni mchakato au hali waliyo nayo baadhi ya watu ya kutaka mafanikio yanayoshadidiwa na moyo wa ushindani, kujiamini, uwezo binafsi wa kukabiliana na kutatua changamoto zilizopo ikiwa ni pamoja na uthubutu wa kukabiliana na changamoto ambazo wakati mwingine huweza kuathiri maisha yao katika kipindi cha mpito.

Kumekuwa na mjadala wa muda mrefu kuhusu kama ujasiriamali hufundishwa au mtu huzaliwa nao, ingawa si lengo la makala haya kujikita katika mjadala huu kwa kuwa tunaelewa nguvu iliyonayo elimu katika kuyatengeneza maisha ya mwanadamu.

Elimu ya ujasiriamali ni muhimu katika ngazi zote za elimu kwa ajili ya kuwatayarisha vijana juu ya maisha yao ya baadaye, kwani tunaamini vijana wana maono na matamanio yao katika maisha kama walivyo watu wazima, ingawa watu hawa wawili wanaweza kutofautiana hapa na pale kutokana na sababu za umri, mazingira, wakati na uzoefu katika maisha.

Elimu ya ujasiriamali katika shule na vyuo hujenga msingi mzuri wa kujiamini miongoni mwa vijana na hivyo kuwafanya wayakabili maisha bila uoga jambo ambalo litawafanya kufanya kazi zao wanazozipenda kwa umahiri, weledi na kujiamini zaidi.

Vijana wanapofundishwa elimu ya ujasiriamali wanaepukana na suala la kusoma kwa kukariri kwa kuogopa kushindwa mtihani ambao kwa sasa kufaulu mtihani huchukuliwa kama tiketi ya mafanikio katika maisha.

Kwa kuwa tumekuwa tukisisitiza zaidi kuhusu ufaulu wa mtihani na kushindwa kuwajengea wanafunzi uwezo wa kujiamini katika maisha yao ya baadaye, udanganyifu wa mitihani umekuwa ukifanyika shuleni na vyuoni kama njia mojawapo ya kukidhi matarajio ya jamii yao ambayo inaona kufaulu mtihani tena kwa alama za juu ndio mafanikio na kushindwa mtihani ndiyo tiketi ya kushindwa maisha!

Badala ya kuwafanya vijana wajiamini katika yale wanayoyafanya na wanayoyapenda kulingana na uwezo na vipawa vyao, tumekuwa tukiwatia hofu ya maisha kwa njia ya mitihani kiasi hata cha kutoa mikopo ya elimu kwa kuzingatia madaraja ya ufaulu jambo ambalo linajenga taifa la watu wasiojiamini katika kazi ambazo si lazima ziwe za kukaa ofisini.

Kama elimu ya ujasiriamali itatiliwa mkazo na kutekelezwa ipasavyo, itasaidia vijana wengi kugundua fursa mbalimbali zilizopo na kuzifanyia kazi kwa manufaa yao na jamii yao.

Vijana wengi wanashindwa kugundua fursa zilizopo kwa kuwa hawana msingi mzuri wa kufanya hivyo, matokeo yake wamekuwa watu wa kusubiri kuambiwa kuwa hapa kuna fursa, pale kuna fursa.

Kitendo hiki kinawafanya baadhi yao kuzivamia fursa hizo pasina kutumia mbinu za kijasiriamali, jambo linalosababisha wengi kushindwa na kukata tamaa.

Elimu ya ujasiriamali humfanya mtu kuwa mbunifu na mgunduzi wa mambo mbalimbali ambayo ni faida kwake na jamii kwa jumla, kwani ugunduzi au ubunifu huo husaidia kutatua changamoto zilizopo katika maisha ya kila siku na hivyo kujenga maendeleo endelevu, kutengeneza ajira, kufufua uchumi na kuboresha maisha ya watu.

Elimu ya ujasiriamali husaidia kubadili mtazamo na fikra za mtu juu ya mambo mbalimbali yanayomzunguka na anayoyaona katika ulimwengu.

Ukweli ni kuwa jamii zilizoamini katika ujasiriamali zimepiga hatua kubwa sana katika kupunguza umaskini ambao ni kikwazo cha ustawi wa mwanadamu.

Elimu ya ujasiriamali ni chachu ya mabadiliko ya jamii kwa kuwa ni mwezeshaji mkubwa wa sekta zote katika maisha ya mendeleo ya mwanadamu.

Hii ni kutokana na ukweli kuwa si kila mmoja wetu anatakiwa kuwa mfanyabiashara mjasiriamali ndipo afaidike na elimu ya ujasiriamali, bali jamii nzima inatakiwa kuishi au kufanya kazi kijasiriamali.