Kuna jambo la kujifunza kutoka Mtwara kuhusu elimu yetu

Shule za msingi nyingi katika Mkoa wa Mtwara zina mwonekano kama huu wa Wanafunzi kusoma kwenye mazingira yasiyo rafiki kwa utoaji wa taaluma. Picha na mtandao wa kusini wordpress.com

Muktasari:

  • Katika matokeo hayo kati ya shule 10 zilizoongoza kufanya vibaya kitaifa, shule tisa zilitoka katika mkoa huo ulioko Kusini mwa Tanzania.
  • Tukio hilo lilitibua nyongo za watu wengi, hususan viongozi wa mkoa huo, walioona kuwa matokeo hayo yamewadhalilisha na kuufedhehesha mkoa. Nadhani walijiapiza kuwa hawataliachia tukio hilo lipite hivihivi. Lazima watu wote waliosababisha aibu hii wachukuliwe hatua!

Mtwara imechafuka. Mtwara inanuka Mtwara haitamaniki! Hii inatokana na matokeo mabaya ya mtihani wa kumaliza elimu ya msingi mwaka 2016.

Katika matokeo hayo kati ya shule 10 zilizoongoza kufanya vibaya kitaifa, shule tisa zilitoka katika mkoa huo ulioko Kusini mwa Tanzania.

Tukio hilo lilitibua nyongo za watu wengi, hususan viongozi wa mkoa huo, walioona kuwa matokeo hayo yamewadhalilisha na kuufedhehesha mkoa. Nadhani walijiapiza kuwa hawataliachia tukio hilo lipite hivihivi. Lazima watu wote waliosababisha aibu hii wachukuliwe hatua!

Kweli kiongozi wa kwanza kuchukua hatua alikuwa ni Mkuu wa Mkoa huo, Halima Dendegu, aliyewawajibisha walimu wakuu wa shule 63 pamoja na maofisa elimu wa shule za msingi wawili kwa kile alichodai ni kushindwa kutimiza majukumu.

Kama kweli mtu anashindwa kutimiza wajibu wake kwa uzembe ni sahihi kabisa kumchukulia hatua za kumrekebisha au hata kumuwajibisha.

Ni uzembe?

Suala la kujiuliza, ni kama kulikuwa na uzembe dhahiri ambao umewafanya maofisa elimu na walimu wakuu hao wastahili kuchukuliwa hatua.

Uongozi wa mkoa unaonekana kuamini pasipo shaka yoyote kuwa walimu wakuu na maofisa elimu hawa wamevuna walichopanda na pengine walistahili hatua kali zaidi!

Kuna baadhi ya watu, taasisi na mitandao kama vile TenMet waliopaza sauti zao na kusema kuwa hata kama walimu wakuu na maofisa elimu hawa wamechangia kuleta matokeo mabaya katika mkoa huo, zipo sababu nyingine ambazo kama hazikuangaliwa zitaendelea kuutafuna mkoa huo kielimu.

Miongoni mwa sababu hizo ni pamoja na mazingira duni ya kujifunzia na kufundishia, uhaba wa vifaa vya kufundishia, uwiano mbaya wa walimu na wanafunzi.

Baadhi ya wadau wanainyooshea kidole hata Serikali yenyewe kuwa inachangia kuzorotesha elimu, si katika Mkoa wa Mtwara pekee lakini nchi nzima.

Mathalan, kwa miaka mingi walimu wamekuwa wakiidai Serikali mabilioni ya stahili zao kama vile nauli za uhamisho bila mafanikio. Ni dhahiri masuala kama haya yamekuwa yakiwavunja moyo walimu wengi na hivyo kufanya kazi kwa shingo upande.

Pia ni shule chache zina zokaguliwa ili kubaini changamoto zilizopo na hivyo kuzirekebisha mapema.

Aidha, ni kwa kiasi gani wazazi na jamii nzima ya Mtwara wanasaidia na kuhamasisha au uboresha elimu katika mkoa? Mathalan, ni kwa kiasi gani wanaitikia miito ya walimu inayowataka kuchangia chakula kwa watoto wao shuleni?

Hivyo wadau wa elimu wamesisitiza kuwa mambo haya ni vizuri yakatiliwa maanani kama kweli tunataka kutatua tatizo la matokeo mabaya ya elimu katika Mkoa wa Mtwara na mikoa mingineyo.

Pia, wakati wananchi wa Mtwara bado wameduwaa na kugubikwa na wingu zito la simanzi pengine lililochanganyika na hasira kutokana na matokeo mabaya ya watoto wao sina hakika kama wao na sisi tumejipa muda wa kutakafakari zaidi nini kifanyike. Ni kwa kiasi gani tumeuangalia na upande wa pili wa sarafu kuhusu matokeo haya.

Inaelekea kuwa tumeamini kuwa wanafunzi wote wa Mkoa wa Mtwara wamefeli mtihani huo. Je, hii ni kweli? Hakuna wanafunzi wengine mkoani humo na pengine kutoka shule hizo tisa waliofanya vizuri mtihani huo? Maana yangu ni kuwa hivi tumejiuliza imekuwaje wanafunzi hawa wachache wamefaulu licha ya kuishi katika mazingira hayahaya duni, kusoma na kufundishwa na walimu hao hao?

Ni wangapi tumeutazama pia upande huu wa pili wa sarafu? Wengi wetu tumewakazia macho wale watoto waliofanya vibaya katika mitihani yao na kujiimanisha kuwa watoto wote mkoani Mtwara walifanya vibaya katika mitihani yao! Je, ni kwa kiasi gani tumefanya uchunguzi uliotuthibishia kuwa wanafunzi wote katika shule zilizofanya vibaya, walifanya vibaya?

Je, hakuna watoto wawili au hata mmoja katika shule hizo aliyefanya vizuri? Kama yupo tumejipa muda wa kumfuatilia ili kujua alitumia mbinu zipi kufanya vizuri wakati wenzake wengi wamefeli?

Yatupasa tufahamu kuwa katika jamii yoyote iwe familia, kijiji, au hata shule huwa kuna watu ambao vitendo au tabia zao si za kawaida lakini zinazowawezesha kupata mafanikio au mikakati ya kuwawezesha kupata ufumbuzi wa changamoto zinazowakabili kuliko wenzao, licha ya kukabiliwa na changamoto zile zile.

Kama tutagundua kuwa wapo watoto watano au hata watatu waliofanya vizuri licha ya kusomea na kuishi katika mazingira duni kama yaleyale ya wenzao waliofeli, hawa wanapaswa kuwa ‘shamba darasa’ kwetu.

Itatupasa tujifunze kutoka kwao ili tujue ni kipi walichokifanya tofauti na wenzao hadi wakafanikiwa kufanya vizuri katika mitihani yao ilhali wenzao walifeli.

Somo hili litatusaidia baadaye kubuni mbinu zitakazotusaidia kukabiliana na changamoto zinazowakwamisha wanafunzi wengi katika mitihani yao.

Lazima tuangalie mbinu mbadala za kukabiliana na changamoto zinazotukabili katika sekta ya elimu. Tunaweza kuanza kujifunza kutoka Mtwara.

Robert Mihayo ni mratibu wa uhakiki wa ubora Shirika la HakiElimu. Baruapepe [email protected] au [email protected]