Kuna tafakuri nyingi za kiuchumi kufutwa leseni za benki tano nchini

Muktasari:

  • Kuna mambo mengi ya kujadili kuhusu kilichofanywa na Benki Kuu yenye majukumu mengi katika usimamizi wa sekta ya fedha nchini ikiwamo kuhakikisha kunakuwa na utulivu wa bei katika uchumi.

        Kati ya habari kubwa juma la kwanza Januari ni kitendo cha Benki Kuu kufuta leseni za biashara za benki tano na kuziweka tatu nyingine katika uangalizi. Mijadala mingi imezuka kiasi cha kuleta hofu kwa baadhi ya watu.

Kuna mambo mengi ya kujadili kuhusu kilichofanywa na Benki Kuu yenye majukumu mengi katika usimamizi wa sekta ya fedha nchini ikiwamo kuhakikisha kunakuwa na utulivu wa bei katika uchumi.

Pamoja na mambo mengine, Benki Kuu pia ina jukumu la kuziangalia na kuzisimamia benki zote za biashara na taasisi za fedha. Usimamizi huu ni pamoja na kuhakikisha benki zinatimiza vigezo vya msingi vya kujiendesha sokoni kwa mujibu wa sheria.

Vigezo hivi vinajumuisha vya kitaifa na kimataifa. Benki Kuu ni lazima isimamie matakwa na viwango vya udhibiti kama inavyotakiwa katika makubaliano ya Basel kuhusu mabenki. Ni muhimu kuhakikisha benki zinakidhi vigezo vilivyowekwa ikiwamo kiasi cha mtaji kinachokubalika.

Kufuta leseni

Kufutiwa leseni kwa benki tano kunatokana na kutotimiza kiwango cha chini cha mtaji kinachotakiwa kwa mujibu wa sheria. Kiwango hiki ni Sh2 bilioni kwa kila benki. Lengo la kuzifutia benki leseni ni kumlinda mteja na uchumi kwa ujumla.

Kati ya maswali ya kimjadala ni kwanini benki hizi zilishindwa kufikia kiasi cha mtaji kinachotakiwa? Kama zilisajiliwa tafsiri ni kuwa zilikuwa na mtaji unaotakiwa ambao ulipungua. Kama ndivyo; kwa nini mtaji ulipungua?

Maswali yote mawili majibu yake yanaweza kupatikana katika sekta zisizo za fedha walipo wateja wa benki. Hii ni kwa sababu afya ya benki kibiashara ikiwamo mtaji na mikopo isiyolipika inaakisi hali ya uchumi. Benki zinaweza kushindwa kufikia kiwango cha mtaji unaotakiwa kama haifanyi biashara vizuri. Biashara kuu ya benki ni kukopesha fedha. Kama hazikopeshi kwa sababu wakopaji hawataki au hawawezi kukopa mtaji utapungua. Vilevile, kama zinakopesha lakini waliokopa hawataki au hawawezi kulipa mtaji utapungua pia.

Kimsingi, kama uchumi wa wakopaji ni nzuri watakopa na kufanya marejesho vizuri hivyo mtaji utakua salama. Kwa hiyo kisababishi kikuu cha kuwapo au kutokuwapo kwa mtaji ya kutosha ni hali ya wateja. Kama kuna haja ya kuokoa hali basi ni kufanyia kazi matatizo ya msingi yanayosababisha wateja kushindwa kukopa au kushindwa kulipa wanapokopa.

Uangalizi

Pamoja na benki tano kufutiwa leseni, kuna zilizowekwa chini ya uangalizi wa Benki Kuu kwa kipindi cha miezi sita hivi. Hii inaashiria kuwa hali sio nzuri katika benki husika. Hali nzuri au mbaya katika sekta ya fedha inaweza kuwa ishira kwa sekta nyingine za uchumi.

Nadharia na uhalisia wa uchumi vinaonyesha kuna mwingiliano wa kisekta. Katika ujumla wake, sekta zote huwa na muelekeo mmoja. Muelekeo wa sekta mtambuka kama ya fedha huweza kuashiria muelekeo wa uchumi kiujumla.

Kati ya zilizojadiliwa zaidi ni kujua hatma ya benki zinazowekwa katika uangaluzi wa Benki Kuu. Kuna hatari ya wateja wake kuzikimbia kwa kuhofia kuwa zinaweza kufutiwa leseni kama zitashindwa kukidhi vigezo katika kipindi cha uangalizi.

Hoja nyingine ni umuhimu wa kuwa wazi kwa Benki Kuu. Wapo wanaofikiri kuwa Benki Kuu imefanya vyema kuweka wazi kuwa benki husika zitakuwa chini ya unagalizi wake. Wapo wanaofikiri uwazi huu ni kiama kwa benki husika kwa maana wateja wenye amana watazikimbia.

Athari

Mjadala mkubwa kuhusu kufutiwa leseni kwa benki husika ni athari zake kwa muda mfupi hasa kwa wateja wenye amana katika benki husika. Athari za moja kwa moja ni kutoweza kupata amana zao kwa wingi wanaotaka.

Taarifa zinaonyesha Bodi ya Bima za Amana itawajibika kulipa hadi Sh1.5 milioni katika awamu ya kwanza wakati wateja hao wakiendelea kusubiri tathmini itakayobainisha hasara iliyopo kwa benki nzima na kuona nani anastahili kiasi.

Wenye kiasi kikubwa zaidi ndiyo wenye hofu kutokana na hili. Wenye zaidi ya Sh10 milioni kwa mfano, wanajiuliza kama watalipwa fedha zao au. Athari nyingine ipo kwenye shughuli za uchumi zinazotegemea benki husika kama vile mjati wa wajasiriamali unaokuwamo kwenye benki hizo pindi zinapofungwa.

Linapotokea hilo, biashara husika huathirika kiasi cha kuweza kuugusa uchumi kwa ujumla. Hata hivyo kuna hoja kuwa kama benki hizi hazikushughulikiwa athari za muda wa kati na mrefu katika uchumi zingeweza kuwa kubwa zaidi.

Elimu

Katika hali kama hii, ni muhimu Benki Kuu kulihakikishia soko kuwa hali ni shwari kwa ujumla. Ni lazima kurudisha imani ya wateja kwa kuonyesha kuwa benki zilizobaki zipo imara na zinaendelea vizuri kwa kutumia vigezo visivyo na shaka.

Vigezo hivi ni pamoja na kiasi cha mtaji kwa aina ya benki mfano benki za jamii, benki za biashara na benki za uwekezaji. Kigezo kingine ni kiasi cha mikopo chechefu. Kama mikopo isiyolipika ni juu ya kiwango cha matakwa ya kisheria na kiudhibiti, Benki Kuu inaweza kuhatarisha sekta hiyo.

Pamoja na Benki Kuu kulihakikishia soko kuwa hali ni shwari ni muhimu kwa benki husika kufanya hivyo pia. Muhimu zaidi ni kwa wataalamu na taasisi huru, mfano Shirika la Fedha Duniani (IMF) kutoa uhakika unaohitajika.