Kuna ulazima Rais Magufuli kuwa mwenyekiti wa CCM?

Rais John Magufuli

Muktasari:

Taarifa iliyotolewa na msemaji wa chama hicho, Christopher Ole Sendeka inaeleza kuwa mkutano huo utatumika kwa Kikwete kukabidhi madaraka ya chama hicho kwa Rais John Magufuli kama ilivyo utamaduni wa chama hicho. Utamaduni huo ni wa muda mrefu kwamba mtu anayechaguliwa kuwa Rais wa nchi kupitia chama hicho, ndiye hufanywa mwenyekiti wa chama.

Jumamosi ya Julai 23, mwaka huu Chama cha Mapinduzi (CCM) kitafanya mkutano mkuu wa kumchagua mwenyekiti mpya wa chama hicho baada ya mwenyekiti wa sasa Jakaya Kikwete kumaliza muda wake kikatiba.

Taarifa iliyotolewa na msemaji wa chama hicho, Christopher Ole Sendeka inaeleza kuwa mkutano huo utatumika kwa Kikwete kukabidhi madaraka ya chama hicho kwa Rais John Magufuli kama ilivyo utamaduni wa chama hicho. Utamaduni huo ni wa muda mrefu kwamba mtu anayechaguliwa kuwa Rais wa nchi kupitia chama hicho, ndiye hufanywa mwenyekiti wa chama.

Wapo wanaounga mkono Rais Magufuli kuwa mwenyekiti wa Taifa wa CCM kwa hoja kwamba atakuwa na mamlaka kamili ndani ya chama chake na ndani ya Serikali. Lakini wapo wanaoona uamuzi huo utampunguzia mamlaka yake.

Swali la msingi ni je, kuna ulazima kwa Rais Magufuli kuwa mwenyekiti wa Taifa wa CCM kwa sasa? Kuna faida au hasara gani kwa nchi ikiwa Rais wa nchi ni mwenyekiti wa chama cha siasa?

Suala hili linaweza kuibua mjadala mpana kwa wachambuzi wa masuala ya kisiasa na wananchi kwa ujumla. Rais wa nchi kuwa mwenyekiti wa chama cha siasa itamzuia kuwa huru kiutendaji.

Baada ya Rais Magufuli kusimikwa rasmi kuwa mwenyekiti wa CCM atakua amefungamanishwa na chama hicho moja kwa moja. Hii itamfanya kuwajibika kwa jambo lolote ndani ya CCM kama ilivyo ndani ya Serikali.

Hii inaweza kutengeneza mgogoro wa kimasilahi kati ya chama chake na Serikali. Kwa hiyo, likitokea jambo ndani ya chama ambalo linagusa pia Serikali itampa Rais wakati mgumu kufanya uamuzi kwa kuwa atakuwa anawajibika ndani ya chama na Serikali kwa wakati mmoja.

Hii ina maana kwamba ikiwa Rais ataletewa suala ambalo linagusa chama chake na Serikali kwa wakati mmoja na akatakiwa kufanya uamuzi ataingia kwenye mgogoro mkubwa wa kimasilahi ili asiathiri upande wowote kati ya pande hizo mbili.

Maana yake ni kwamba atapima katika mizani ya usawa nafasi ya chama chake na nafasi ya nchi. Ikitokea hivi itakuwa si sahihi.

Nionavyo mimi, Rais Magufuli kuwa mwenyekiti wa CCM Taifa siyo kumfanya kuwa na mamlaka kamili kama wengi wadhaniavyo, bali ni kumfunga minyororo katika uamuzi yake.

Uamuzi atakaofanya Rais Magufuli baada ya Julai 23 atapaswa kukifikiria chama chake na Serikali yake kwa wakati mmoja. Kuna wakati atalazimika kukisaidia chama chake kwa gharama ya urais wake. Hii si dalili nzuri katika ukuaji wa demokrasia.

Pia, si dalili nzuri kwa CCM wala kwa vyama vya upinzani. Kwa CCM ni dhahiri hawatakuwa na fursa ya kumfaidi mwenyekiti wao maana muda mwingi atabanwa na majukumu ya nafasi yake ya urais.

CCM itastawi au itadumaa?

Maana yake ni kwamba CCM haitakuwa na mwenyekiti mtendaji, bali wa heshima (ceremonial). Kwa hali hii ni ngumu chama kukua na kustawi.

Kwa hiyo, CCM isipokuwa makini inaweza kudumaa kwa miaka mingine 10 kutoka sasa kwa sababu haitakuwa na mwenyekiti mtendaji.

Hii ina maanisha kuwa kama CCM inahitaji kukua, itapaswa kuwa na mwenyekiti mtendaji. Mwenye muda wa kutosha wa kufanya shughuli za chama chake na kufanya ubunifu mbalimbali wa kukisaidia chama chake kukua kama ilivyo kwa vyama vya upinzani. Vinginevyo CCM itazidi kudumaa kama ilivyokwishadumaa kwa muda mrefu sasa.

Mwaka 2005 kwenye Uchaguzi Mkuu, CCM ilipata kura milioni 8 na wapinzani kura milioni 2. Miaka 10 baadaye (2015) CCM wakatangazwa kupata kura zilezile milioni 8 huku wapinzani wakipata kura milioni 6 kutoka milioni 2.

Hii ni dalili kuwa vyama vya upinzani vinakua, lakini CCM imedumaa. Kwa hiyo, kumfanya Rais Magufuli kuwa mwenyekiti ni kuifanya CCM izidi kudumaa, kwa sababu Rais hawezi kuwa mwenyekiti mtendaji wa chama cha siasa na kila kitu kikaenda sawa.

Nafasi ya kukua kwa demokrasia

Kwa upande wa vyama vya upinzani ni dhahiri Rais Magufuli akiwa mwenyekiti wa CCM vyama hivyo vitaathirika hasa katika ukuaji wa demokrasia. Hii ni kwa sababu mfumo utampa Rais fursa ya kutumia mamlaka yake ya nchi kwa faida ya chama chake.

Kwa mfano, Rais akishiriki shughuli za chama chake, ataendelea kulindwa kama Rais na kauli zake zitabebwa kwa uzito kuwa ni kauli za Rais japo atakua akizungumza kama mwenyekiti wa chama.Rais pia, aweza kutumia jukwaa la chama chake kutoa maagizo ya Serikali na yakatekelezwa.

Hii itakifanya chama chake kuwa ‘chama dola’ badala ya chama kinachoongoza dola. Hii itaviathiri sana vyama vingine kwa sababu wenyeviti wao hawatakuwa na fursa katika Serikali kama atakayokuwa nayo mwenyekiti wa CCM (Rais Magufuli).

Vilevile, uzoefu unaonyesha kwamba katika nchi zilizopiga hatua kidemokrasia duniani, hutenganisha cheo cha mkuu wa nchi na uongozi ndani ya chama. Hii inasaidia kuepusha mgogoro wa kimasilahi unaoweza kujitokeza.

Kuna wakati Rais atapaswa kuchukua uamuzi unaoweza kukiathiri chama chama chake. Lakini ndiye mwenyekiti atawezaje kujikwamisha?

Nchini Marekani, Rais Barrack Obama anatokana na Chama cha Democratic, lakini hajawahi kuwa kiongozi ndani ya chama hicho mathalan uenyekiti. Mwenyekiti wa sasa wa chama hicho ni Debbie Wasserman Schultz. Hii inampa fursa nzuri Rais Obama kufanya uamuzi kwa uhuru na haki bila kufungwa moja kwa moja na itifaki za chama chake.

Sasa kwa nini na hapa kwetu tusifanye hivyo pia? Ikiwa demokrasia tuliyonayo tumerithi kutoka nchi za magharibi, kwa nini tusirithi na misingi yake yote? Mbona tumerithi nusunusu? Kwa nini tusifanye kama Marekani kuruhusu Rais awe huru na chama kiwe na utaratibu mwingine wa kuwapata viongozi wake nje ya taasisi ya urais?

Pengine wapo watakaosema kuwa hatupaswi kuiga kila wanalofanya wamagharibi kwa kuwa mazingira yetu na yao ni tofauti. Ni sawa, lakini mbona hata Kenya wametushinda? Je, Kenya nao ni wamagharibi? Chama cha TNA kimemtoa Rais Uhuru Kenyatta, lakini Kenyatta siyo Mwenyekiti wa chama hicho. Mwenyekiti ni Johnson Sakaja.

Huyu anayeshughulika na masuala yote ya kisiasa ndani ya TNA na hivyo kumpa fursa Rais Kenyatta kushughulikia zaidi masuala ya kitaifa kuliko ya chama chake. Kwa nini CCM wasiige hata kwa Wakenya kama hawataki kuiga Marekani?

Magufuli ana uzoefu?

Hata hivyo, ndani ya CCM Rais Magufuli hana uzoefu mkubwa unaoweza kumfanya kuwa mwenyekiti hodari wa chama hicho kitaifa. Kwa mujibu wa aliyekuwa Mwenyekiti wa CCM Mkoa wa Shinyanga, Hamis Mgeja ni kuwa Rais Magufuli hajawahi kushika wadhifa wowote ndani ya chama chake zaidi ya kuwa mwanachama wa kawaida.

Maana yake ni kwamba, hajawahi kushiriki vikao vyovyote vikubwa vya uamuzi ndani ya chama chake. Hajawahi kushiriki vikao vya chama chake ngazi ya wilaya, mkoa wala vya kitaifa.

Ameanza kushiriki vikao hivyo baada ya kuwa Rais. Kwa hiyo, hana uzoefu mkubwa ndani ya chama chake. Je, ataweza kuimudu nafasi ya mwenyekiti wa chama hicho ngazi ya Taifa? Hili ni swali wanalojiuliza watu wengi nje na ndani ya CCM.

Mwandishi ni mchambuzi wa masuala la siasa na jamii, anapatikana kwa barua pepe: [email protected] na [email protected]