KUTOKA MEZA YA MHARIRI WA JAMII: Kunahitajika muda kujadili Muswada wa Habari

Muktasari:

Ni kweli kwamba wananchi wote na hata wadau wote nchini hawawezi na hawajawahi kushiriki maandalizi ya muswada huu. Kuna “wachache” waliowahi kushiriki kujadili hatua za awali za kuandaa muswada.

Hapa kuna muswada wa Sheria ya Huduma za Habari wa mwaka 2016. Wadau wa habari wanasema wameuona, wameusoma na wameutafakari. Wanataka kuujadili kwa ‘manufaa ya nchi.’

Ni kweli kwamba wananchi wote na hata wadau wote nchini hawawezi na hawajawahi kushiriki maandalizi ya muswada huu. Kuna “wachache” waliowahi kushiriki kujadili hatua za awali za kuandaa muswada.

Hata hivyo, kushiriki mijadala ya awali siyo kuandika muswada. Baada ya kupokea maoni ya washiriki, Serikali ambayo huwa na nia ya dhati ya kufanya inachotaka, hupeleka maoni yake kwa mwandishi wa sheria ambaye “hunyoosha na kupinda kama alivyoelekezwa.”

Kilichonyooshwa na kupindwa na kunyooshwa kama mtaalamu alivyoelekezwa na Serikali, ndicho kilichopo katika muswada huu.

Sasa kuna wanaosema walijadili mambo kadhaa lakini siyo katika mwelekeo huu. Kuna wanaosema hawajawahi kushiriki kwa njia yoyote ile katika hatua za awali za kuandaa muswada. Kuna waliosema lakini hawakusikika.

Ni katika makundi haya inatoka sauti: “Tunahitaji muda kujadili muswada huu.” Hawa ni wale wanaotaka kujadili nia, lengo la muswada na kinachoweza kutokea huko tuendako endapo muswada utapitishwa kama ulivyo na kuwa sheria.

Wanaiomba Serikali kusitisha hatua ya kupeleka bungeni kwa shabaha ya kusomwa kwa mara ya pili na kujadiliwa, muswada wa Sheria ya Huduma za Habari.

Ni bahati mbaya kwamba katika hatua ya sasa, baadhi ya waandishi wa habari ambao wangekuwa mstari wa mbele kupigania kupatikana kwa sheria bora wamegawanyika.

Kuna wanaosema kile ambacho Serikali imeleta katika muswada ni “sawa, sahihi na kinatosha. “ Kuna wanaosema “muswada ni kitanzi.” Kuna wanaosema “twende tu” na kwamba hii ni hatua moja; “tutadai mabadiliko huko tuendako.”

Hapa inaonekana wazi kuwa kuna baadhi ya waandishi wana mchoko wa mwili na akili; kuna wenye jicho la masilahi la “huenda nikapandia hapo; kuna wanaofikiri hakuna haja ya kupigania mabadiliko; lakini pia kuna wanaosema hawatakaa kimya katika kutetea taaluma yao.

Kutosikilizana, kuchoka na kutafuta masilahi binafsi katika kipindi hiki ni kukataa kuona na hata kupuuza hatari inayowazengea waandishi wa habari.

Hii siyo ishara nzuri katika tasnia ya habari. Huu ni mgawanyiko unaoelekeza kwenye kupoteza fursa katikati ya kipindi cha kupigania uhuru wa kufikiri kuwa na maoni na kutoa maoni hayo bila woga wa kukemewa, kutishwa au kufungwa.

Ni kupoteza uhuru wa mwandishi wa kutafuta na kuandika habari; uhuru na haki ya mwananchi ya kutafuta na kupewa taarifa na habari; na uhuru wa vyombo vya habari wa kukusanya na kusambaza taarifa na habari.

Kwa mfano, mgawanyiko utasababisha waandishi wa habari kushindwa kuona kuwa muswada huu, siyo tu unaweza kutafsiriwa kulenga kumiliki habari, bali hata waandishi wa habari wenyewe. Kifungu cha 10 na kile cha 18 (2) vya muswada vinaeleza hilo kinagaubaga.

Miliki inapatikana katika kuomba “kufungwa”, kuomba kuwa mwandishi wa habari. Huwi mwandishi wa habari mpaka usajiliwe, uorodheshwe na kutambuliwa na bodi inayoundwa chini ya muswada wa sheria hii ya Serikali.

Ukiishasajiliwa, kutambuliwa na kuorodheshwa, ukae tayari kusimamishwa au kufukuzwa wakati wowote bodi itakapokukuta na dosari.

Bodi itatumia kanuni “kama zitakavyoainishwa.” Hazimo katika muswada huu.

Kifungu cha 18, kwa mfano, kinasema mtu yeyote hataruhusiwa “kufanya kazi ya uandishi wa habari, isipokuwa kama mtu huyo amethibitishwa na sheria hiyo”- siyo kuthibitishwa na mwajiri wako anayejua uwezo na umuhimu wako.

Ni mambo kama haya ndiyo waandishi wa habari na wadau wa habari wanapaswa kukaa pamoja na kujadili na kutolea maoni.

Chunga hili: aliyeachishwa au kufukuzwa kazi kwa mkono wa Bodi, “hataruhusiwa kufanya kazi ya uandishi wa habari kwa namna yoyote ile” (Kifungu 20 (2). Angalia kifungu 20 (3) – yule ambaye amefutwa “hataruhusiwa kuajiriwa au kushughulika kwa namna yoyote ile katika kazi au taaluma inayohusiana na habari.”

Si haya tu, muswada umejaa vitanzi kwa mwandishi wa habari na wananchi wote. Unagusa haki ya watu wote ya kufikiri, kuwa na maoni, kutafuta na kupewa taarifa; na uhuru wa kutoa maoni.

Muswada huu unagusa hata wabunge na rais. Hawatapata taarifa za kweli na sahihi. Kuna heshima gani katika kujiundia kitanzi?

Huu basi ndiyo msingi wa waandishi wa habari na wadau wa habari kutaka muda zaidi kujadili muswada huu. Tujadili.