Friday, July 21, 2017

TUONGEE KIUME : Kusomesha kimada ni sawa na kujivika mabomu

 

By Kelvin Kagambo

Ulishawahi kukutana na stori za kuhuzunisha lakini unapozisikia unashidwa kujizua kucheka? Mjini kuna stori nyingi za namna hiyo, ukitaka kuzisikia jitahidi kuwa karibu na vyanzo vyake na niamini mimi, hazitakuwa stori tu, bali zitakuachia funzo fulani.

Kuna moja niliisikia majuzi— nakukumbusha tu ni ya kuhuzinisha lakini hakuna namna, inabidi tuizungumzie hapa.

Kuna jamaa ni jirani yetu, hivi tunavyozungumza hata saa 24 hajamaliza tangu arejeshwe nyumbani kutoka hospitali alikokuwa amelazwa kwa siku mbili baada ya jaribio lake la kutaka kujiua kwa kunywa sumu kushindikana.

Kabla hatujafika mbali niweke sawa kitu kimoja, ninaposema jamaa simaanishi kijana, ni mwanaume mtu mzima tu, ana mke mzuri na watoto watatu, na mwanaye wa mwisho anasoma kidato cha pili— sasa vuta picha tunayemzungumzia yukoje.

Binafsi nilivyosikia jirani kalazwa kwa kunywa sumu niliingiwa wasiwasi mno, nikajua inawezekana baada ya yeye mimi nitafuata kwa sababu nilichokuwa nikiamani ni kwamba, mtu mzima namna ile hawezi kufikia hatua ya kutaka kujiua kwa sababu za kijingajinga tu, lazima jaribio lake lilikuwa ni sehemu ya matokeo ya mabadiliko ya hali ya hewa mjini tangu mfumo wa maisha uwe ‘Kazi Tu’.

Lakini baadaye nikapata habari za uhakika kuwa kumbe jirani alitaka kujiua baada ya kuletewa kadi ya mwaliko wa harusi ya kimada wake wa miaka mingi ambaye inasemekeana alimlipia ada ya miaka mitatu wakati binti anatafuta shahada yake chuo kikuu, kwahiyo kwa kweli ile taarifa ya kwamba anaoelewa ilikuwa ni nzito kwa jirani.

Ukijaribu kujivisha viatu vya jirani utagundua nyakati ngumu alizopitia baada ya taarifa ile. Utagundua ni kweli alikuwa na kila sababu ya kujaribu kujitoa roho ili kuepukana na machungu— ada ya miaka mitatu sio kitu kidogo bwana, ni ‘vimilioni’ kadhaa hapo, ukijumlisha na mizinga ya hapa na pale, inaweza kusoma milioni kumi kwa hesabu za haraka.

Ila ukijaribu kujivisha ujirani kwa jirani yangu utagundua kuwa kweli stori yake ilikuwa inahuzunisha lakini ndani kwa ndani inafurahisha kwa sababu imejaa ujinga.

Hivi kweli mwanaume mwenye akili timamu, umeoa na una watoto, unapata habari kuwa kimada wako uliyemsomesha anaolewa unakasirika hadi kutaka kujiua, unataka kutwambia kuwa ulivyokuwa unajivisha majukumu ya baba yake ulikuwa unaamini kwamba atakuwa kimada wako miaka nenda rudi, kwamba hatakaa awaze kuolewa, kuwa na familia kama wewe.

Haki ya mungu huo ni ujinga, tena nadhani kama ingewezekana hospitali ziwe zinahoji sababu ya mtu kutaka kujiua kabla ya kumpokea na kumpa matibabu, mtu akija na sababu za kijinga namna hii hakuna haja ya kumsaidia kwa sababu huko ni kufuja muda na nguvu kazi kumuhudumia mjinga mmoja ambaye anayachokonoa matatizo yakiamka anatafuta kichaka kwa kuyakimbia.

-->