Kutambua pekee haitoshi, suluhu itafutwe kufungwa kwa biashara

Waziri wa Fedha na Mipango, Dk Philip Mpango akizungumza wakati wa mkutano na waandishi wa habari jana jijini Dar es Salaam. Picha na Omar Fungo

Muktasari:

Alisema kati ya Agosti na Oktoba 2016; Wilaya ya Ilala ilifunga biashara 1,076, Kinondoni 443 na Temeke 222 na Jiji la Arusha zikifungwa 131.

Mwishoni mwa Desemba 2016, Waziri wa Fedha na Mipango, Dk Philip Mpango alitoa taarifa ya utekelezaji wa bajeti kwa kipindi cha nusu mwaka. Pamoja na mambo mengine, alieleza kuwa baadhi ya wajasiriamali walifunga biashara zao.

Alisema kati ya Agosti na Oktoba 2016; Wilaya ya Ilala ilifunga biashara 1,076, Kinondoni 443 na Temeke 222 na Jiji la Arusha zikifungwa 131.

Ni jambo linalohitaji mjadala na kazi zaidi ikiwemo kutafuta kiini cha tatizo na suluhu yake. Waziri Mpango alisema wafanyabaishara hao hawakuweka wazi kilichowafanya waamue kusitisha shughuli zao. Alitoa sababu za jumla ambazo zinaweza kuchangia hilo.

Kwa kadri ya takwimu za waziri, jumla ya biashara zilizofungwa katika kipindi husika kwa Dar es Salaam ni 1,741. Hii ni sawa na biashara 580 kwa mwezi au biashara 19 kwa siku.

Arusha zilifungwa biashara 74 kwa mwezi yaani wastani wa biashara mbili kwa siku. Kwa vigezo vyovyote vile idadi hii ya kufunga biashara siyo ndogo. Vilevile, hizi ni takwimu za Dar es Salaam na Arusha pekee.

Sampuli hii ya mikoa miwili ni ndogo kwa nchi nzima. Hata hivyo, ikiongezwa mikoa kama vile Mwanza, Mbeya na Tanga takwimu kwa nchi nzima zitaonyesha uhalisia wa kufungwa kwa biashara.

Kwa uchumi wa nchi, kaya na mwananchi mmoja mmoja, siyo afya biashara kufungwa kwa sababu yeyote ile. Hii ni kutokana na athari nyingi ambazo zinawagusa wengi na kufikia mbali katika kufungwa kwa miradi hiyo.

Athari

Kufungwa kwa biashara kwa sababu yeyote ile kuna athari kwa watu na taasisi kadhaa. Zipo athari za moja kwa moja na zisizo za moja kwa moja, muda mfupi, wa kati na mrefu.

Ndiyo maana ni muhimu kuchambua na kujadili hali hii kwa ajili ya kutafuta chanzo cha msingi na suluhu ya tatizo hili.

Athari za awali ni kwa wenye biashara husika. Kufungwa kwa biashara maana yake ni pamoja na kupoteza au ajira na kipato kwa wenye biashara hizi na wasaidizi wao.

Kwa upande wa Serikali Kuu na zile za mitaa kuna kupoteza mapato yatokanayo na kodi na yasiyo ya kodi. Kiasi cha mapato haya kitategemea pamoja na mambo mengine aina ya biashara na ukubwa wake.

Kwa taasisi za fedha hasa zinazodai madeni kwenye biashara hizo kutakuwapo na changamoto ya kutorejeshwa mikopo iliyochukuliwa kwa wakati. Kutegemea na ukubwa wa mikopo husika, taasisi hizi zinaweza kutikisika.

Hii ni kwa sababu biashara ya taasisi hizi ni kutoa mikopo na mapato yake ni riba inayolipwa na wakopaji. Kama biashara zimefungwa, uwezekano wa kulipa mitaji iliyochukuliwa na wamiliki ni mdogo.

Hii ni kweli pia kwa watu na taasisi nyingine zinazokuwa zikizidai biashara zilizofungwa. Siyo afya kiuchumi kwa sababu licha ya taasisi za fedha, wafanyabiashara wengine waliokuwa wanazitegemea watalazimika kutafuta sehemu nyingine.

Wateja wa bidhaa na huduma hizo watalazimika kutafuta muuzaji mwingine, hii inaweza kuongeza gharama. Waliokuwa wanauza malighafi kwa ajili ya uzalishaji wa bidhaa husika nao watakosa soko, watoa huduma na ushauri vilevile.

Sababu

Ingawa waziri alisema wamiliki hawakutoa sababu za kufungwa kwa biashara za, alieleza inawezekana kushindwa kuingiza bidhaa nchini bila kulipa kodi stahiki ni miongoni mwa changamoto zilizochangia suala hilo.

Kiuchambuzi, mfumo wa kodi una mambo mengi. Kuna haja ya kujua ni nini hasa katika mfumo wa kodi kinacholeta ugumu kwa wafanyabiashara hao kiasi cha kufunga biashara zao.

Utafiti wa mradi unaoitwa Taxation, Institutions and Participation (TIP) ambao mwandishi wa makala hii ni mtafiti mkuu kwa Tanzania umebaini kuwa mifumo ya kodi ina mambo mengi.

Yapo mambo mengi yanayolalamikiwa na walipa kodi. Haya ni pamoja na wingi na viwango vikubwa vya kodi, namna za ukusanyaji kodi, ukokotozi wa makadirio ya kodi na ukiritimba katika marejesho inapolipwa nyingi kuliko inayostahili.

Mengine ni ushirikishwaji katika maamuzi ya msingi ya kodi, matumizi ya mashine za EFD, namna kodi inavyotumiwa, makundi fulani kupata misamaha ya kodi na mengine kutopata, ukwepaji wa kodi kwa baadhi ya wanaopaswa kulipa na kadhalika.

Nadharia

Katika nadharia za biashara na uchumi, biasara zinaweza kufungwa kwa sababu mbalimbali. Kimsingi biashara zitaweza kufungwa katika muktadha wa makala haya kwa sababu hazifanyi vizuri.

Vipimo na vigezo vya biashara kufanya au kutofanya vizuri ni vingi. Hivi ni pamoja na kutokuwa na mauzo mazuri. Kutokuwa na mauzo mazuri kunasababisha kutopata fedha za mauzo na faida inayotarajiwa.

Ina maana kuwa muhusika atashindwa kulipa gharama za uendeshaji wa biashara ikiwemo pango, mishahara ya wafanyakazi, madeni ya taasisi za fedha kama benki na kodi mbalimbali. Hata hivyo, ni lazima kwenda ndani zaidi ili kubaini kiini cha tatizo.

Biashara kutofanya vizuri kwa vigezo na viashiria tajwa hapa ni dalili ya matatizo ya msingi zaidi. Kutoweza kuuza bidhaa na huduma kama ilivyokuwa awali ni dalili ya tatizo la msingi zaidi ambalo lazima litafutwe.

Vivyo hivyo kutoweza kufanya biashara kwa sababu ya mfumo wa kodi ni dalili ya matatizo ya msingi zaidi yanayopaswa kufanyiwa kazi.

Jambo la kufanya

Ili kutatua tatizo la biashara kufungwa ni lazima kujua chanzo cha kufungwa kwake. Ili kujua chanzo ni azima utafiti wa kina ufanyike. Sababu ya mfumo mgumu wa kodi iliyoelezwa na waziri lazima ifanyiwe utafiti wa kina zaidi.

Pamoja na mambo mengine ni lazima kujua ni nini hasa katika mfumo wa kodi kinaleta tatizo na kusababisha biashara kufungwa. Pamoja na mambo mengine, masuala yanayolalamikiwa katika mfumo wa kodi kwa kadri ya wa TIP lazima yafanyiwe kazi.

Vilevile, sababu za kinadharia zilizoainishwa lazima zifanyiwe kazi pia ili kujua kinachochochea biashara kufungwa na muhimu zaidi, kinachotakiwa kufanyika ili kuzuia hali hii na kuzirejesha biashara zilizofungwa sokoni.

Ili kupata uhalisia wa tatizo husika, waliofunga biashara wanatakiwa kuhusishwa zaidi. Itapendeza endapo biashara zilizofungwa zitabainishwa na kutafuta suluhu ili kuzikomboa. Nadharia inatutaka kuchochea hizi biashara kwa kuzipa mazingira safi, rafiki na wezeshi.