Kutoa maoni, kuandamana kwa amani si uhaini kisheria

Muktasari:

  • Serikali imetamka kwa nguvu kubwa kwamba watakaojaribu kuandamana “Watakiona cha mtema kuni.“ Wananchi wametahadharishwa kwamba kutokana na katazo la maandamano, kufanya hivyo ni sawa na kufanya uhaini.

Kwa muda wa wiki mbili hivi kumekuwapo na maoni mengi katika vyombo vya habari kuhusu maandamano. Kwa upande mmoja wako wanaopigania uhalali wa kuandamana; na huku upande wa Serikali ukiwaonya wote wanaopanga kuandamana.

Serikali imetamka kwa nguvu kubwa kwamba watakaojaribu kuandamana “Watakiona cha mtema kuni.“ Wananchi wametahadharishwa kwamba kutokana na katazo la maandamano, kufanya hivyo ni sawa na kufanya uhaini.

Lugha hii ya uhaini ndiyo iliyonisukuma niandike maoni yangu haya. Ni lugha kali na yenye kutia hofu. Inapofikia hatua kwamba lugha ya uhaini inatumika katika kuzuia haki ya wananchi kueleza maoni yao, suala hilo halipaswi kunyamaziwa. Tunahitaji tafakari ya kina kutoka kwa wadau mbalimbali kwa ajili ya ustawi wa nchi yetu.

Tatizo kubwa ambalo linawasumbua watu wengi na hasa wanazuoni ni hili, wakitambua fika kwamba uhuru wa kutoa maoni na kufanya maandamano ya amani ni haki yao ya kibinadamu na ya kikatiba, wanabaki kujiuliza, je, zuio la mikutano ya kisiasa kwa wanasiasa nje ya majimbo yao, na zuio la maandamano ya kisiasa yanachangia vipi katika kukuza haki na umoja wa kitaifa?

Hili ni swali la msingi. Kwa sababu kwa upande mmoja kipo chama tawala ambacho licha ya makatazo hayo mwenyekiti wake ambaye ni rais wa nchi, na katibu mwenezi wa chama hicho wanaonekana wakizunguka nchi nzima kukutana na watu na kukinadi chama tawala, na kwa upande mwingine viko vyama vya upinzani vinavyokumbana na ukali wa makatazo hayo. Wenyeviti wa vyama hivyo na makatibu wao waenezi hawana ruhusa kufanya siasa katika sehemu nyingine za nchi yetu. Uwanja wa kisiasa katika hali hii hauko sawa.

Jambo la pili linalowatatiza wanazuoni ni hili, Kama nia ya zuio hilo ni kuwafanya watu kufanya kazi na kushughulika na maendeleo badala ya kupiga siasa, kinachosahaulika hapa ni kuwa kufanya siasa kwa misingi ya kisheria ni sehemu ya sayansi na tafsiri ya kazi. Tusiporuhusu haki ya kutoa maoni, tukaongozwa na sera ya “hapa kazi tu“ bila kuhoji - kazi hugeuka kuwa shuruti na shuruba” The tyrany of work“. Tujipe muda tujifunze kutokana wasia ya kitume kutoka Papa aliyelitembelea Bara la Afrika mara nyingi, Mtakatifu Yohane Paulo II.

Kulingana na Hati ya Kitume ya Papa Yohane Paulo II, Kanisa katika Bara la Afrika (Nairobi, 1995), makatazo dhidi ya uhuru wa kutoa maoni, uhuru wa vyombo vya habari na maandamano yanakandamiza dhamiri za watu; yanachezea haki yao na pia kudumaza utu wao.

Papa Yohane Paulo II alikuwa mmoja walioandaa Mtaguso wa Pili wa Vatikani (1962-1965), ambao tayari hapo awali ulishatamka kuwa uhuru wa kujieleza na kuabudu ni mambo ya msingi katika utu wa mwanadamu.

Mtaguso katika Tamko lake kuhusu uhuru wa kuabudu, unatamka wazi kwamba “Kila mwanadamu kwa kusikiliza dhamiri yake anayo kinga ya kidhamiri bila kutakiwa kuwa na woga kujieleza hadharani, na kueleza imani yake hadharani ili mradi haingilii uhuru wa wenzake.“

Ni katika mwanga huo, Mtakatifu Yohane Paulo II anapolitazama Bara la Afrika anasikitishwa kutokana na maelekezo ya Serikali nyingi za Kiafrika. Anasema na ninamnukuu, “Nalazimika kuandika kwa huzuni nyingi kwamba mataifa mengi ya Kiafrika yangali yanaishi katika utawala wa kiimla na dhuluma ambazo zinawanyima wanaotawaliwa uhuru wa kibinafsi na haki muhimu za binadamu hasa uhuru wa kuchangamana pamoja na wa kisiasa, na vile vile haki ya kufanya uchaguzi wa serikali ulio wa haki“ (Kanisa Katika Afrika 1995, no. 112).

Kwa kadiri ya maoni ya Papa huyu, amani haitapatikana kwa njia ya kuminya haki ya demokrasia na uhuru wa raia kujieleza, bali kwa kuruhusu haki zao za msingi.

Ni kwa sababu hiyo Papa Yohane Paulo II anafundisha kwa kusema: “Pamoja na mababa wa Sinodi ningependa kusisitiza kuendelezwa kwa harakati za kutetea haki ya jamii na uongozi bora kama njia ya lazima katika kutengeneza uwanja mzuri wa amani. Ukitaka amani shughulikia haki. Ni vizuri sana-na pia ni vema –kuzuia machafuko kuliko kujaribu kuyachochea. Ni wakati ambapo watu wafue panga zao ziwe majembe na mikuki iwe miundu (Isa 2:4),“ mwisho wa kumnukulu. Anachotaka kutuambia Papa ni kwamba ni bora kabisa kwa viongozi na raia kusikilizana ili kudumisha amani na maelewano. Jambo la muhimu ni viongozi kutambua msingi wa malalamiko ya wananchi ili wajikite katika kutatua kero zao.

Mazungumzo na majadiliano ni jambo la kuzingatiwa badala ya umwagaji wa damu. Ni muhimu kutambua kwamba umwagaji wa damu ni aibu kwa mwanadamu mwenyewe.

Haki ya kuishi ni moja kati ya mambo muhimu yanayotetea utu wa mwanadamu. Mambo mengine ni haki ya kuabudu, ya kutoa maoni na ya kwenda mahali popote ili mradi mtu havunji sheria.

Kumbe, iwapo umwagaji wa damu ni aibu kwa mwanadamu mwenyewe, basi kuzuia uhuru wa kutoa maoni ni kama kuuweka rehani utu wa mwanadamu.

Ili huo uhuru wa kutoa maoni uweze kufanya kazi barabara, Papa Yohane Paulo II anawaagiza Wakristo walei wasimame imara kupigania na kutetea demokrasia ya vyama vingi.

“Hii ndiyo sababu Sinodi imegusia kwamba demokrasia ya haki na yenye kuheshimu vyama vingi vya kisiasa, ni mojawapo ya majukumu ambayo yanalionyesha Kanisa kusafiri na watu“ (Kanisa Barani Afrika, no. 112).

Kwenye nchi yoyote ile yenye Katiba inayoruhusu mfumo wa vyama vingi; upo wajibu na wajihi wa kutekelezwa matakwa ya demokrasia ya vyama vingi.

Hiyo ni pamoja na uhuru wa kutoa maoni na kufanya maandamano ya amani. Maandamano ya amani kwa mujibu wa katiba hayawezi kuwa ni uhaini hata kidogo. Kadiri ya mahimizo ya kitume ya Papa huyu, ni wajibu wa Wakristo walei kuhakikisha utawala wa sheria unashamiri barani Afrika.

Papa mwenyewe anaagiza, “Wakristo wanaoshughulika katika jitihada za kidemokrasia kulingana na ujumbe wa Injili, ni kielelezo cha Kanisa ambalo linashiriki katika kuendeleza utawala wa sheria kila mahali barani Afrika. (Kanisa Barani Afrika, no. 112).

Mtumishi huyo wa Mungu analitaka Kanisa liwe jasiri katika kuishi utume wake wa kinabii barani Afrika katika kutetea haki. “Jukumu la Kanisa katika kutetea haki na hasa la kulinda haki za binadamu, haliwezi kuchukuliwa kimzaha“ (Kanisa Barani Afrika, no. 106).

Unabii wa Kanisa unajikita katika mambo matatu; kutangaza habari njema ya Ufalme wa Mungu, kukemea maovu, na kupinga kwa vitendo maovu katika jamii.

Hivyo, kanisa litakamea wakati watu wengi wananyamaza kwa hofu, Kanisa litashauri wanasiasa hata wakati watu wengi wakiogopa, na Kanisa linaweza hata kuhamasisha maandamano ya amani likiwa limejisadikisha kuwa hiyo ni njia ya lazima kama viongozi walioko madarakani hawasikilizi.

Mwaka 2004 huko Austria Kardinal Christoph Schonborn pamoja na maaskofu wa Austria waliongoza maandamano kupinga uvamizi wa Marekani huko Iraq. Mwaka 1998 Kardinali wa New Delhi India pamoja na masista waliaandamana katika Jiji hilo kupinga madhulumu waliyofanyiwa masista. Na hivi karibuni huko Jamhuri ya Congo, Kardinali Laurenti Mosengwo Askofu Mkuu wa Kinshasa alihamasisha maandamano dhidi ya utawala wa Rais Kabila katika jaribio lake la kuendelea kubaki madarakani.

Maandamano ya amani ni muhimu sana kama hatua ya watu kueleza malalamiko yao ambayo hayakushughulikiwa kwa muda mrefu. Hivi ndivyo Papa Yohane Paulo II anavyofundisha kuhusu wajibu wa Kanisa Barani Afrika anasema hivi: “Kanisa...lazima liendelee na unabii wake na kuwa sauti kwa wasiokuwa na sauti, ili kila mahali utu wa binadamu uheshimiwe na kila mtu na watu kwa ujumla wawe kiini cha mipango ya Serikali“. (Kanisa Barani Afrika, no. 70).

Mwishowe, nimnukuu tena Papa anaposema, „Uenezaji wa Injili lazima ukatae na kuzuia kudunishwa na kuharibiwa kwa mwanadamu. Kulaani maovu na unyanyasaji ni mojawapo ya utumishi wa uenezaji Injili katika uwanja wa kijamii ambao ni kipengele cha unabii wa Kanisa (Kanisa Barani Afrika, no. 70).

Kwa vyovyote vile, mustakabali mzuri wa taifa letu utategemea sana jinsi viongozi waliopo madarakani wanavyoheshimu haki za msingi za raia wao; na upatikanaji wa Katiba Mpya itakayopanua wigo wa kidemokrasi na kuwapatia raia wenyewe mamlaka zaidi katika kuchangia mustakabali wa nchi yao.

Mungu Ibariki Tanzania, dumisha uhuru na umoja.

Mwandishi ni Padri wa Jimbo Katoliki la Mbinga na Mhadhiri katika Chuo Kikuu Katoliki -CUEA–Kampasi ya Gaba, Kenya