Kutoka kuwa dansa na sasa ni mwanamuziki wa injili

Sunday February 18 2018

 

By Tumaini Msowoya, Mwananchi [email protected]

Jesca Gazuko sio jina geni kwa wapenzi wa muziki wa injili hasa kutokana na mwanadada huyo kuonekana kwenye video za waimbaji wengi.

Jesca amewahi kucheza kwenye video nyingi zikiwamo: ‘Surprise’ ya Goodluck Gozebert, Jesca Honore na Miriam Lukindo.

Akizungumza na mwandishi wa makala haya amesema muziki ndio maisha yake na kucheza ilikuwa njia tu ya kufikia mafanikio yake.

Binti huyo anayechipuki katika muziki huo ameachia kibao chake kipya kinachoitwa ‘Bwana Amefanya’.

“Bwana Amefanya ni wimbo wangu mpya unaonitambulisha kama Jesca mwimbaji, sio mcheza shoo tu. Namshukuru Mungu kwa siku chache tu nilizoachia wimbo huu, umeanza kupata maarufu,” anasema.

Anasema wakati wake umefika kuonyesha kipaji chake cha uimbaji japo wengi wamezoea kumuona kwenye kucheza tu.

“Nimecheza kwa waimbaji wengi sana sasa nimeamua kuimba mwenyewe ninachoomba mashabiki wangu wanipokee kama mwanamuziki. Wapokee nyimbo zangu ,” anasema na kuongeza;

“Kaa tayari kumpokea Jesca akiwa mwimbaji na sio dansa kama wengi walivyozoea, sio kwamba nitaacha kucheza hapana, lazima niendelee kumchezea Mungu wangu lakini, nitacheza zaidi kwangu mwenyewe”.

Tayari wimbo wake huo umeanza kusikika kwenye vituo mbalimbali vya redio na yupo mbioni kuachia video yake.

Anasema yupo kwenye hatua za awali za kuandaa video yake huku mkakati wake mkubwa ukiwa kuachia wimbo baada ya wimbo.

Waimbaji wengi wa muziki wa Injili hawana uongozi na hilo linawafanya washindwe kufikia ndoto ya mafanikio yao.

“Nipo chini ya uongozi kwa hiyo kila ninachokifanya sasa naelekezwa tu na nina uhakika nitafika mbali,,” anasema.

Mbali na muziki, Jesca amekuwa akijishughulisha na kazi mbalimbali ikiwamo biashara.

“Nafanya kazi nyingine za kujiingizia kipato na nimeajiriwa kwa hiyo natumia muda wangu wa ziada kutekeleza yote,” anasema.

Akizungumzia changamoto kwenye kucheza anasema kuna baadhi wamekuwa wakimdhulumu lakini, hayo yote huwa hayampi shida kwa sababu mwisho wa siku, anakuwa amefanya kwa ajili ya Mungu.

“Wengine wakiona Jesca dansa wanadharau, hilo huwa halinipi shida kwa hiyo niwashauri tu wadada wenzangu kutobabaishwa na maneno ya watu, kutochagua kazi na kujituma kwa sababu bila hivyo, sio rahisi kufikia ndoto za mafanikio yetu,” anasema.

Akielezea mikakati yake, mwanadada huyo anasema kiu yake ni kuja kuwa mwanamuziki mkubwa.

Anaamini moja ya njia ya kufikia mafanikio yake ni kutumia vyombo vya habari.

Advertisement