Kuwa na nguvu za kiume si kigezo cha uwezo wa kutungisha mimba

Muktasari:

  • Sababu ya kwanza ni aina ya maisha ya mwanaume husika na historia ya utumiaji wa baadhi ya madawa. Madawa haya yanaweza kuwa ya kimatibabu au hata ya kulevya.

Kitu muhimu wanaume wanachopaswa kukijua ni hiki, pamoja na kuwa na nguvu za kiume na uwezo wa kushiriki tendo la ndoa kikamilifu, lakini bado wanaweza kupatwa na tatizo hili linalosababisha kushindwa kuzaa au utasa kutokana na sababu mbalimbali zinachangia tatizo hili kama nitakavyoeleza.

Hivyo kabla sijaendelea nawashauri wanaume wote waliopo kwenye mahusiano na ndoa ambao kwa kipindi kirefu wamekua wakipatwa na kasumba hii, kabla ya kuwatupia lawama wanawake wao, wanapaswa kupata vipimo vya afya kutoka kwa madaktari ili kutatua tatizo kwanza, na nikumbushe tu kuwa kwa enzi enzi tulizo nazo sasa, kumlaumu mwanamke kuwa hazai bila mwanaume naye kupata vipimo vya afya, kijamii inachukuliwa kama ni unyanyasaji wa kijinsia na ni kuendekeza utamaduni wa kizamani.

Sababu ya kwanza ni aina ya maisha ya mwanaume husika na historia ya utumiaji wa baadhi ya madawa. Madawa haya yanaweza kuwa ya kimatibabu au hata ya kulevya. Kati ya wanaume walio hatarini kupoteza uwezo wa kuzaa ni wale wenye tabia ya ulevi. Ulevi sio tu unaathiri nguvu za kiume lakini pia unadhoofisha uzalishwaji stahiki wa mbegu za kiume na hata hicho kiasi hafifu cha mbegu zinazozalishwa bado zinakosa afya ya kuweza kurutubishwa.

Uvutaji wa sigara na bangi, unywaji wa pombe na hasa wa kupindukia, utumiaji wa madawa mengine haramu ya kulevya unaathiri moja kwa moja uwezo wa kutungisha mimba. Lakini hata uzito uliopitiliza pia unaathiri utungishwaji wa mimba. Mwanaume anashauriwa kudhibiti uzito wa mwili unaoashiria kupita kiasi kwani kufanya hivyo atasaidia kudhibiti uwepo wa mafuta ya ziada ambayo kwa kawaida yanaathiri uzalishwaji wa mbegu za kiume.

Matatizo katika utokaji wa mbegu za kiume ni sababu nyingine iliyopo nyuma ya tatizo hili ambayo wanaume wengi wanashindwa kuitambua. Haijalishi kama mwanaume ana nguvu za jinsia kwa kiasi gani lakini pia kiasi cha ujazo wa mbegu za kiume pia ni muhimu katika kufanikisha utungishwaji wa mimba. Lakini hata hivyo, wanaume wachache wanasumbuliwa na tatizo ambalo ile mirija inayosafirisha

mbegu za kiume kutoka kwenye korodani ambako ndiko zinakotengenezwa na kuchujwa na kuja kwenye uume huziba kutokana na matatizo mengine ya kiafya kama vile kuwa na mafuta yaliyozidi mwilini, matatizo ya kisukari na hata maambukizi mengine kwenye mfumo wa uzazi na ikitokea hivyo basi inatengeneza tatizo lingine ambalo kitaalamu linaitwa sperm motility problem.

Kama kiwango cha mbegu za kiume ni hafifu hawezi kuwa rahisi kuzifanya mbegu hizo zisafiri kwa kasi inayohitajika hadi kwenye yai la mwanamke kwa ajili ya urutubishwaji, kwa sababu ili mbegu ziweze kurutubishwa zinahitaji uwingi na kasi pia.

Baadhi ya matatizo yanayoweza kuchangia ni kama vile kutokua na uwiano wa mfumo wa homoni mwilini, magonjwa au maambukizi kwenye via vya uzazi na mfumo wa uzazi kwa ujumla, baadhi ya magonjwa ya kurithi, na utumiaji wa baadhi ya madawa ambayo yana mchanganyiko mkubwa na kemikali.

Ili kuzitambua sababu nyingine nyingi zaidi mwanaume anapaswa kupata kuwaona wataalamu wa afya ili kupewa msaada zaidi na kutatua tatizo linalomkabili pasipo yeye kujua badala ya kuendelea kuwatupia lawama wanawake.