MAONI YA MHARIRI: Kwa hili la malori Waziri Mwijage umeteleza

Waziri wa Viwanda, Biashara na Uwekezaji, Charles Mwijage

Muktasari:

Miongoni mwa mambo waliyojadili katika mkutano huo ni upungufu wa mizigo ulivyoanza kuathiri biashara yao, suala ambalo lilimuibua Waziri wa Viwanda, Biashara na Uwekezaji, Charles Mwijage aliyeufungua mkutano huo kuwajibu.

Mwishoni mwa wiki iliyopita wamiliki wa malori kupitia chama chao cha Tatoa, walifanya mkutano wao mkuu ambao waliutumia kujadili mambo mbalimbali yanayoihusu sekta ya usafirishaji kwa ujumla wake.

Miongoni mwa mambo waliyojadili katika mkutano huo ni upungufu wa mizigo ulivyoanza kuathiri biashara yao, suala ambalo lilimuibua Waziri wa Viwanda, Biashara na Uwekezaji, Charles Mwijage aliyeufungua mkutano huo kuwajibu.

Kauli hiyo ya upungufu wa mizigo bandarini na ile ya baadhi yao kuhamia bandari za Mombasa nchini Kenya na Beira ya nchini Msumbiji, ilifafanuliwa na Waziri Mwijage kuwa kupungua kwa mizigo ni suala la dunia nzima na muda si mrefu litarekebishika.

Hata hivyo, mmoja wa wanachama wa Tatoa ambaye pia ni Mkurugenzi Mtendaji wa Kampuni ya NMC Tracking, Natal Charles alimwambia itachukua muda mrefu kuwarejesha watumiaji wa Bandari ya Dar es Salaam kwa sababu waliondoka kutokana na ushindani wa kibiashara uliopo kwenye bandari nyingine.

Kutokana na hali hiyo, mfanyabiashara huyo alisema imesababisha wenye malori waliokopa mikopo benki ili kununua magari hayo kuwa katika hatari ya kufilisiwa na pia wapo baadhi yao ambao wamefilisika kwa kukosa mizigo ya kusafirisha.

Lakini, Waziri Mwijage alienda mbali zaidi kwa kuwashauri wamiliki hao kwamba kama hakuna mizigo ya kubeba ni vema wakayaegesha malori yao hadi hali itakapokuwa nzuri.

Majibu ya Waziri Mwijage ya kutaka wenye malori wayaegeshe, tena kwa kuwasisitiza wayapake vilainishi kwa wingi ili yasipate kutu, yameacha ukakasi ambao haukuwa na sababu ya kuwapo.

Hatuoni sababu ya kauli hiyo ya Waziri Mwijage, ilhali wenye malori ni sehemu ya uchocheaji wa ongezeko la ajira na ukuaji wa uchumi wa nchi? Kama alivyosema mkurugenzi wa NMC Tracking, baadhi yao wana mikopo na benki zinataka marejesho yao. Hizo fedha za mikopo watazipata wapi kama hawazalishi? Je, benki zitaendelea kuwavumilia wakati nazo zinafanya biashara?

Pili, hivi katika kipindi cha kusubiri mwaka mmoja au zaidi ya hapo alichosema waziri kuwa ndiyo ambacho anatarajia ongezeko la mizigo bandarini watakuwa wanafanya shughuli gani?

Ni kweli kwamba wote walioathiriwa na hali hiyo wanaweza kujenga viwanda vidogo kama alivyosema na kumudu kuviendesha hata kama hawana uzoefu na shughuli hiyo?

Tunasema waziri alikuwa na sababu ya kujadiliana na wadau hao umuhimu wa namna gani ya kuendesha shughuli zao ili mwisho wa siku pande zote, yaani wao, Serikali na hata jamii inayotegemea shughuli zao ziweze kunufaika kwa kuendesha maisha na kuchangia katika pato la Taifa.

Tunaamini kwamba wamiliki hao wa malori ni wawekezaji muhimu kwenye sekta ya usafirishaji kutokana na mchango wake kiuchumi, lakini hawapaswi kupatiwa majibu hayo katika hali inayotafsirika kama kejeli, wakati Serikali ndiyo yenye jukumu la kuwaandalia mazingira bora ya uendeshaji wa shughuli zao.

Kama ilivyo kaulimbiu ya mpango mkakati wa Serikali ya Awamu ya Tano ya uanzishaji wa viwanda vingi nchini, lakini haiwezi kufanikiwa bila sekta ya usafirishaji kuwa imara. Uimara wa sekta hiyo utakuwapo kutokana na uboreshaji wa mazingira unaopaswa kufanywa na Serikali na siyo wawekezaji.

Waziri Mwijage hapaswi kukwepa jukumu hilo kwa kuwa ndilo aliloapa kulitekeleza. Kwetu sisi bado tunaamini kwamba wamiliki wa malori wana fursa ya kuendelea na shughuli zao na Serikali inawajibika kuwezesha mazingira yatakayowaweza kupata mizigo ya kusafirisha.