Kwa nini wanaume wanachepuka zaidi kuliko wanawake

Muktasari:

  • Hii huongezeka zaidi pale ambapo kuna misuguano ndani ya nyumba na kwa hiyo wanandoa hawawezi kuweka hisia na mawazo yao katika tendo la ndoa, mume hata kama ana kiu kiasi gani anawaza anamuanzaje mkewe, maana anajua fika kwamba atakataliwa.

Kwa sababu wanaume ni watu wanaopenda tendo la ndoa mara kwa mara, na kwa sababu wake zao hawako tayari kutimiza kiu hii mara kwa mara kulingana na uhitaji, wanaume wengi huchangamkia fursa pale wanapokutana na uwezekano wa kupata tendo la ndoa kirahisi na kwa wepesi.

Hii huongezeka zaidi pale ambapo kuna misuguano ndani ya nyumba na kwa hiyo wanandoa hawawezi kuweka hisia na mawazo yao katika tendo la ndoa, mume hata kama ana kiu kiasi gani anawaza anamuanzaje mkewe, maana anajua fika kwamba atakataliwa.

Wengine kutokana na ukaribu baina yao kuwa mbaya, mwanaume anaona ugumu kumtongoza mkewe ampe tendo la ndoa, akiwaza kuanza mchakato huu anaona ni jukumu zito kama kujenga nyumba sasa mtu wa hivi anapopata fursa rahisi na nyepesi kutoka kwa kiumbe yeyote wa kike ukweli ni kwamba hataiacha.

Hapa ndipo panapochochea biashara ya umalaya, kwa sababu mwanaume anaona ngoja nitumie shilingi elfu tano au kumi au ishirini ili nimalizane na hii hamu mara moja nirudi nyumbani. Ndio maana pia wanawake walio rahisi au wanaojirahisisha kingono hutumiwa na wanaume hususan na waume za watu maana kiu yao ni kuitumia fursa hiyo kiufasaha na kuondoka.

Kisasi

Mara nyingi wanaume hutumia kitendo cha kutoka nje ya ndoa au nje ya uhusiano kama fimbo ya kulipiza kisasi kwa maumivu au hasira yoyote waliyokuwa nayo dhidi ya mpenzi au mke.

Kwa mfano, wanaume wengi nilioongea nao binafsi, hususan wale ambao walikuwa wanalalamika kuwa mke wangu haniheshimu, mke wangu ananidharau, mke wangu hanisikilizi, mke wangu anafanya hivi au anafanya vile baada ya kuongea au kulalamika kwa muda mrefu pasipo kuona mabadiliko baadaye waliamua kuchepuka.

Kisaikolojia, mwanaume anapochepuka kwa sababu ya kisasi huwa inamwondolea ile hali ya kujishtaki au kushtakiwa nafsini kwamba amefanya kosa na hiyo inaweza kumfanya aendelee kuchepuka kwa muda mrefu tofauti na mwanamke.

Ni vyema ukachukua tahadhari hii pale unapoona mume wako analalamika sana kuwa haumheshimu, unamdharau, haumsikilizi, haushuki au kunyenyekea, basi fahamu kwamba kuna uwezekano mkubwa ameshaanza kuchepuka au yuko kwenye kuisoma ramani ili aanze.

Kama kuna uwezekano wa kubadili tabia na kushughulikia hayo malalamiko yake ni bora ukafanya hivyo maana kifuatacho chaweza kuhatarisha uhusiano wenu.

Mkanganyiko wa matarajio

Wapo wanaume wengi ambao kabla hawajaoa walikuwa na shauku kubwa kwa wake zao, walikuwa na matamanio au matarajio makubwa kwa wake zao.

Wengine walioa wake zao kwa sababu ya maumbo mazuri na ya kuvutia, wengine ni aina ya familia wanawake hao walizotoka, wengine walioa wakitegemea huyu mwanamke ni mcha Mungu sana, au aliwahi kusikia habari zake nzuri kwa watu na akatamani sana kuwa naye maishani na mara baada ya kuingia kwenye ndoa bahati mbaya yale mambo aliyokuwa ana kiu nayo sana na kuyatarajia anakuta sivyo yalivyo.

Wapo ambao nimeongea nao sana, wanasema walipooa lile umbo zuri la mke wake alidhania ndio ustadi wa kitandani baadaye akakuta ujuzi wa tendo la ndoa ni mdogo kuliko matarajio yake.

Wengine baada ya ndoa wamekuja kugundua tabia zilizojificha kwa mke ambazo hawakuzijua awali, wengine wameibua udhaifu kedekede kwa wake zao ambao mwanzoni hawakuufikiria.

Hii hali ya matarajio ya mwanaume kufukiwa na uhalisia huua kabisa hamasa ya tendo la ndoa na hapo inakuwa rahisi mwanaume kuanza kutafuta uhusiano mwngine nje.

Pamoja na kwamba wanaume huonekana wakiwa jasiri kwa nje, ieleweke kwamba ni viumbe dhaifu ndani, ni viumbe wasioweza kuvumilia upweke ndani yao, wakati wote hutamani kuwa karibu na mwanamke hata kama akiwepo karibu hawaelewani mara kwa mara.

Mara nyingi kwenye uhusiano unakuta mwanaume ameoa au ana mpenzi na kuna mambo yanaendelea ambayo yanasumbua uhusiano wao.

Ukaribu unapokosekana mwanaume huanza kujihisi upweke ndani yake na hapo inanyanyuka kiu ya kutafuta mtu wa kuuondoa.

Inasemekana kwamba wanaume wengi huchepuka au kuanza mchakato wa kuchepuka kunapokuwa na tafrani kwenye mapenzi au ndoa, ni kwa nini? Sababu ni kwamba ule ugomvi umeleta baridi moyoni na nafsini kwa mwanaume na hawezi kustahimili upweke huo ndani yake kwa hiyo anatafuta faraja haraka sana.