Kwanini Rais Kim amekubali kukaa mezani na Trump

Muktasari:

  • Ni kwa sababu Korea Kaskazini inasema imefikia malengo yake ya kuwa na uwezo wa kutengeneza silaha za nyuklia

Viongozi wote duniani wanaelekeza macho na masikio yao katika mkutano wa kihistoria Ijumaa ijayo kati ya Rais wa Korea Kusini Moon Jae-in na mwenzake wa Korea Kaskazini Kim Jong Un. Kikubwa dunia itataka kujua matokeo ya majadiliano ya ajenda yao: Marufuku silaha za nyuklia.

Mkutano huo unaweza kutoa mwanga muhimu kuhusu kuwepo au kutokuwepo mkutano mwingine wa kihitoria kati ya Rais wa Marekani Donald Trump na wa Korea Kaskazini Kim Jong Un.

Suala la silaha za nyuklia limetajwa sana wiki za hivi karibuni, kutoka Seoul hadi Washington na Beijing, lakini bado kuna shaka kuhusu kinachomaanishwa ‘marufuku ya silaha za nyuklia’, na kuchanganyana kunaweza kuzua matatizo katika mkutano wa Ijumaa na uliopangwa baadaye kati ya Trump na Kim.

Habari zilizotolewa na maofisa wa Korea Kusini na vyombo vya habari vya China ni kwamba Kim yu radhi kuingia katika majadiliano ya kuondoa silaha za nyuklia katika rasi ya Korea.

Alhamisi iliyopita, Rais Moon alisema Korea Kaskazini haikupendekeza sharti lake la muda mrefu la kutaka vikosi vya ulinzi vya Marekani viondolewe kwanza ili nayo iweze kuachana na silaha za nyuklia, suala ambalo wachambuzi wametilia shaka.

Machi 27 Kim alipokuwa amefanya ziara nchini China, shirika la habari la Xinhua lilimnukuu kiongozi huyo akisema, “Msimamo wetu wa siku zote ni kwamba tumedhamiria kuhakikisha hakuna silaha za nyuklia katika rasi, kwa mujibu wa matakwa ya hayati Kim Il Sung na hayati Katibu Mkuu Kim Jong Il.”

Kauli hiyo ilivutia majibu chanya kutoka kwa Trump, ambaye alisema kulikuwa na “fursa nzuri” kwa Korea Kaskazini kuondokana na silaha za nyuklia. Lakini kiuhalisia Trump, Kim na Moon akilini wana maana tofauti ya marufuku ya silaha za nyuklia.

Marekani, Korea Kusini

Katika kipindi cha zaidi ya muongo mmoja, Marekani na Korea Kusini zimekuwa na maana moja tu kuhusu marufuku ya silaha za nyuklia za Korea Kaskazini. Ni kuwepo mkakati usiobadilika wa kuharibu kabisa programu ya silaha na kufanya uhakiki wa kina.

Lugha hiyo ndiyo inatumiwa wakati wote na Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa katika maazimio yake ya kulaani Korea Kaskazini yaliyotolewa Oktoba 2006. Mkakati usiobadilika kiuhalisia unalenga kuhakikisha hauwezi kufanyika tena urutubishaji wa madini ya urani baada ya kubomoa programu.

Ukaguzi unaweza kufanywa na shirika la kimataifa kama vile Shirika la Kimataifa la Nishati ya Atomiki (IAEA) ambalo wakaguzi wake walifukuzwa na Korea ya Kaskazini mwaka 2002.

Kwa miongo kadhaa, Marekani na Korea Kusini zimejaribu kusukuma ajenda ya marufuku ya silaha za nyuklia katika Korea ya Kaskazini.

Mwaka 1991, Korea Kaskazini ilijiunga na Korea Kusini kutia saini “tamko la pamoja la kuacha utengenezaji silaha za nyuklia katika Rasi ya Korea.” Miaka miwili baadaye, Korea Kaskazini iliahidi kuwa itaharibu programu zake za nyuklia ili kubadilishana na misaada ya kimataifa.

Lakini kila wakati maagano hayahhufikiwa lakini ahadi hazikufuatwa na pande zote mbili.

Bado serikali ya Marekani inaonekana kuwa na matumaini ya mazungumzo ya hivi karibuni kwamba yatakuwa tofauti.

Jumatano Trump alitoa mtazamo wake akisisitiza kuwa hayuko katika nafasi ya kutekeleza kile ambacho watangulizi wake hawakuweza.

Hata hivyo, alisema kuwa angependa kusimama tayari akisubiri kuona kitakachotokea katika mkutano huo unaosubiriwa sana ikiwa hautakidhi matarajio yake.

Kwa upande wa Korea Kusini, Moon alikanusha Alhamisi kuwepo madai ya mgawanyiko kati ya kile Kaskazini na Kusini walichomaanisha kuhusu marufuku ya silaha za nyuklia. “Sidhani kama kuna tofauti yoyote katika dhana,” alisema Moon.

Korea Kaskazini

Akiwa Beijing Kim aliahidi mazungumzo kuhusu kuachana na silaha za nyuklia, lakini hakuzungumzia utayari wa nchi yake kusitisha programu zake. Bali alizungumzia kuondolewa silaha za nyuklia katika Rasi (Korea).

Wataalamu walisema Korea Kaskazini kwa muda mrefu imekuwa ikitarajiwa kuingiza uwepo wa vikosi vya Marekani kwenye mpaka kuwa sehemu ya majadiliano.

Ingawa Marekani haijaweka silaha za nyuklia nchini Korea Kusini tangu mwaka 1992, Korea Kaskazini inaona kuwa uwepo tu wa Marekani katika rasi ni kitishio cha nyuklia.

Korea Kaskazini inaona inatishiwa na nguvu ya kijeshi za Marekani na Korea Kusini hivyo yenyewe inahitaji silaha za nyuklia kujaribu kuzuia uvamizi kwa mtazamo wowote.

Pia inataka kulinganisha programu yake ya nyuklia na ya jeshi la muungano (Marekani na Korea Kusini) ambalo inadai ni kitisho cha nyuklia katika rasi.

Wataalamu walisema mabadiliko ya dhahiri ya Korea Kaskazini kuhusu uwepo wa jeshi la Marekani katika Korea Kusini ilionekana kama chaguo bora la muda mfupi au kwa namna nyingine ni jaribio la kusukuma jambo dogo linaloelekea kuzaa jambo kubwa kwa Marekani na Korea Kusini.

Msimamo mpya

Jumamosi Korea Kaskazini ilitoa taarifa nyingine ya matumaini kabla ya mkutano wake na jirani yake Korea Kusini kuhusu marufuku ya silaha za nyuklia.

Vyombo vya habari vya Korea Kaskazini vimetangaza kuwa serikali itasitisha majaribio ya silaha za nyuklia na itafunga maeneo yanayotumika kurushia na itasitisha programu ya makombora ya masafa marefu.

“Kuanzia Aprili 21, Korea Kaskazini inasitisha majaribio ya nyuklia pamoja na urushaji wa makombora ya masafa marefu,” lilisema shirika la habari la serikali la KCNA.

Kim amesisitiza: “Hatutatumia silaha za nyuklia isipokuwa ikiwa kuna kitisho au uchokozi wa kinyuklia kwa nchi yetu, na kwa namna yoyote hatutasafirisha silaha za nyuklia wala teknolojia ya nyuklia.”

Kwa nini Kim anasema watasitisha majaribio ya nyuklia? Jibu; kwa sababu nchi yake ya Korea Kaskazini imefikia malengo yake ya kuwa na uwezo wa kutengeneza silaha za nyuklia. Hii ndiyo sababu ya Kim sasa kukubali mazungumzo na Moon na Trump.

Chama cha Wafanyakazi Korea Kaskazini kimesema serikali yao itaonyesha ushirikiano na kufanya majadiliano na nchi jirani kuhakikisha hali ya amani na uthabiti katika Rasi ya Korea.

Lakini Trump anasema ikiwa mwelekeo hautaridhisha ataondoka kwenye kikao.

acidel et