Kweli, haki inapocheleweshwa ni sawa na kutopewa

Mashehe wa kundi la Uamsho wanaotuhumiwa kujihusisha na vitendo vya ugaidi wakiwa chini ya ulinzi wa askari Magereza walipofikishwa katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu jijini Dar es Salaam. Picha na Maktaba

Muktasari:

Mwanaharakati maarufu wa haki za Wamarekani wenye asili ya Kiafrika, Martin Luther King alieleza katika barua aliyoitoa kwa siri mwaka 1963 kutoka jela ya Birmingham kwamba, “haki ikichukua muda mrefu kutolewa, ni sawa na kutotolewa.”

Katika mfumo wa utawala wa kidemokrasia yapo mambo ambayo ni vigezo muhimu katika kupima kuwapo au kutokuwapo kwa utawala bora, wa haki na sheria.

Vipimo hivyo vikionekana havipo au kuna udhaifu katika utekelezaji wake, basi huo unaoitwa utawala bora huwa na mashaka na kuelezwa kuwa ni wa maneno na si vitendo.

Vipimo vikuu vya mfumo huo ni uhuru, usawa na haki ambavyo kusisitizwa kwa umuhimu wake kuna historia ya zaidi ya karne mbili na imekuwa ikielezwa kwamba amani ya kweli hupatikana pale haki inapotolewa kwa vitendo badala ya maneno matupu.

Katika suala hili ipo misemo inayosikika kila siku katika mahakama, mikutano ya wanasheria na katika makongamano na semina mbalimbali juu ya umuhimu wa haki wakati wote kuonekana inatolewa tena kwa wakati.

Orodha ndefu ya misemo hii ni pamoja na, “haki ikikawia kutolewa ni sawa na kutotolewa” na “kukawia kuitoa haki sio haki.”

Mwanaharakati maarufu wa haki za Wamarekani wenye asili ya Kiafrika, Martin Luther King alieleza katika barua aliyoitoa kwa siri mwaka 1963 kutoka jela ya Birmingham kwamba, “haki ikichukua muda mrefu kutolewa, ni sawa na kutotolewa.”

Maelezo yote haya yanasisitiza umuhimu wa haki kupatikana kwa haraka, hasa watu waponyimwa uhuru wao na kuletewa bughudha katika maisha yao na kuziacha familia zao zikiteseka na kuathirika kwa shida za maisha.

Nilifurahishwa na wajumbe wa Baraza la Wawakilishi walipozungumzia suala hili katika mkutano wa bajeti ya mwaka 2017/18 kwa kulalamikia kutolewa haki kwa washtakiwa katika kesi nyingi ziliofunguliwa Zanzibar.

Zipo kesi zilizotolewa mfano na kuelezwa kuwa zinawasononesha watuhumiwa. Watu hawa, wengine kwa zaidi ya miaka saba wamenyimwa dhamana kama vile sio haki ya mshtakiwa kupata dhamana na kesi zao huwa kila siku hazisikilizwi, bali hupangiwa tarehe za kutajwa.

Kesi zilizogusiwa ni pamoja na za wafanyakazi na watu wengine waliodaiwa kuhusika kwa njia moja au nyingine na zinazowahusu kwa njia moja au nyingine kuzama meli za abiria na watu wengi kupoteza maisha yao.

Wawakilishi walitaka kesi hizi sikilizwe haraka na washtakiwa kupewa dhamana. Kinachoshangaza ni kwamba wawakilishi hawakugusia hata kidogo kesi ya viongozi wa Jumuiya ya Kiislamu ya Uamsho ambayo mara nyingi huwaona washtakiwa wanafikishwa katika Mahakama  ya Zanzibar na mara nyingine Dar es Salaam.

Sasa ni miaka minne na kesi hii haionekani kuendelea na la ajabu kusikia hivi karibuni jaji mmoja wa Zanzibar akihoji kwa nini washtakiwa hao waliondolewa Zanzibar na kupelekwa Dar es Salaam wakati wanadaiwa kufanya kosa linalowakabili Zanzibar.

Kwanza sielewi kwa nini imechukua miaka minne kwa kauli kama hii kusikika katika mahakama ya Zanzibar.

Lakini kubwa zaidi ambalo ningelitarajia kulisikia kutoka kwa wawakilishi ni kwamba hawa viongozi wa dini waliwahi kutoa shutuma nzito za kudhalilishwa wakati wakiwa katika mikono ya vyombo vya sheria.

Madai ya viongozi hawa wa dini ni pamoja na kuteswa na kufanyiwa unyama. Hizi si shutuma ndogo na hazistahili katika nchi ya kidemokrasia kufumbiwa macho wala kuzibiwa masikio.

Ningetarajia wawakilishi sio tu kuzungumzi suala hili katika malalamiko yao ya watu kusota magerezani kwa muda mrefu bila ya kesi zao kusikilizwa, bali hata kutaka iundwe tume ya uchunguzi kuutafuta ukweli wa madai ya hawa viongozi wa dini.

Kwa vyovyote vile lazima tukubali madai waliyotoa vongozi hao yanazipaka matope Serikali za Zanzibar na ya Jamhuri ya Muungano na Serikali yoyote makini na inayojali utawala wa haki na sheria ingeunda tume kuchunguza shutuma hizi.

Lakini hata mahakama ilikaa kimya baada ya tuhuma hizi nzito kutolewa na kutotoa amri ya kutaka jambo hili lichunguzwe na mahakama kupelekewa ripoti juu ya ukweli au uzushi wa jambo hili.

Serikali zote mbili; ya Zanzibar na Muungano, ziliwaahidi wapigakura na zimekuwa zikisisitiza kuongoza nchi kwa mfumo wa sheria na haki.

Lakini tujiulize haki ipo wapi kama watu wanakaa miaka saba gerezani wananyimwa dhamana na kesi zao hazisikilizwi na kumalizika?

Ni vizuri kwa viongozi wa Serikali na vyombo vya sheria wakalitupia macho suala hili ambalo limeonekana sasa kuwakera hata wajumbe wa Baraza la Wawakilishi.

Ukimya hautoi tafsiri yoyote ile isipokuwa kumfanya raia kuona Serikali haijali uhuru wa wananchi wake na kumuona mtu hana kosa mpaka pale anapotiwa hatiani na mahakama kutokana na ushahidi uliowasilishwa mahakamani.

Kwa muda mrefu pamekuwapo na madai katika jamii juu ya kuwapo kesi za kutunga na za kisiasa ili kuwakomoa watu badala ya kesi kufunguliwa kwa kosa la uhalifu.

Panapotokea kusuasua kwa kesi kuchukua miaka saba hadi 10 bila kusikilizwa na hukumu kutolewa panasababisha madai ya kwamba utawala wa haki na sheria nchini una upungufu mkubwa.

Hali hii pia haiipi nchi yetu taswira nzuri katika jumuiya ya kimataifa mbali ya kuzitesa familia za washtakiwa.

Ni vyema ikatafutwa njia muafaka, kama Katiba inavyoeleza na sheria zetu kuelekeza, kwa utawala wa haki na sheria kufuata mkondo wake na watu kuona haki inatendeka kwa vitendo na si maneno huku tukiimba kwamba nchi yetu ni ya amani, utulivu na yenye kuendeshwa kisheria.

Katika miaka ya nyuma tulikaripia sana mwenendo wa kuwaweka watu kuzuizini uliokuwa ukifanywa na makaburu wa Afrika Kusini kwa kuwafungulia kesi zilizokuwa kila siku zinapigwa tarehe na hazimaliziki.

Sio vizuri sasa na sisi kuanza kuwa na mwendo kama huo ambao hauendi sambamba na mfumo wa utawala wa kidemokrasia.

Katiba yetu ambayo inamhakikishia kila raia uhuru wake wa kuishi na kutawaliwa kwa misingi ya haki na sheria lazima iheshimiwe na wale wanaokiuka mwenendo huu kwa kuwadhalilisha wenzao wanaopaswa kuwajibishwa.

Tumerithi magereza kutoka kwa wakoloni na tumejenga mengine kwa ajili ya kuwaweka na kuwapa adhabu watu wanaovunja sheria za nchi na kuonekana wahalifu na mahakama na si kuwa kama nyumba za kufikia wageni ili kutumika kwa ajili ya kuwapeleka watu kuteseka na kuwadhalilisha wao na familia zao.

Tukumbuke ukweli, hekima na busara zilizomo katika ile misemo ya “haki ikikawia kutolewa ni sawa na kutotolewa” na “kukawia kuitoa haki sio haki”.