La Mayanja linaibua maswali kibao

Muktasari:

  • Kuna mahali wameharibu? Huku tulio nje tunajijibu, hapana, kuna mgogoro Simba? Tunaoangalia jibu hapana wakati ligi ikiingia mzunguko wa saba, hatuoni tatizo.

Unajiuliza, kabla ya mechi na Njombe Mji juzi, Simba ilikuwa nafasi ya ngapi, jibu, ni ya kwanza.

Kuna mahali wameharibu? Huku tulio nje tunajijibu, hapana, kuna mgogoro Simba? Tunaoangalia jibu hapana wakati ligi ikiingia mzunguko wa saba, hatuoni tatizo.

Simba iko nafasi ya kwanza ikiwa na pointi 15 na mabao 19, kocha mkuu ni Joseph Omog, inakuwaje msaidizi anakuwa bomu zaidi ya mkuu? Maswali mengi yanayotokana na Mayanja yanazalisha majibu mchanganyiko.

Juzi kocha msaidizi wa Simba, Mganda Jackson Mayanja alipanda ndege kwenda Uganda akisema ana matatizo ya kifamilia.

Licha ya kocha huyo kutoa sababu hizo, bado mashabiki wa klabu hiyo haiwaingii akilini na kuona kama viongozi wameamua tu kumtimua kocha huyo maarufu kama Mia Mia.

Tetesi za Mayanja kuondoka Simba zilianza kabla ya msimu huu wa Ligi Kuu kuanza huku kocha wa Mbao, Etienne Ndayiragije akitajwa kuwa msaidizi wa Omog, lakini akakataa hilo. Akambeba Mayanja lakini leo kaletewa Masudi Djuma.

Naye utajiuliza, kama Mayanja hakutimuliwa, Djuma wameongea naye saa ngapi, hivi apigiwe simu aje tu kipindi kifupi? Haiingii akilini.

“Kama nilivyosema hapo awali naondoka kutokana matatizo ya kifamilia, yalianza muda mrefu lakini sasa yamefikia pabaya. Sitaweza kufanya kazi vizuri, Simba inahitaji kocha anayekuwepo muda wote, kocha ambaye anaweza kujitoa na kujituma muda wote, kwa sasa sitakuwa na uwezo huo,” anasema Mayanja

Chanzo cha kuondoka kwake

Licha ya kwamba sababu ya kifaimilia ndio imetajwa kumuondoa kikosini kocha huyo lakini habari zinapasha kuwa alikuwa hana maelewano mazuri na wachezaji wengi katika kikosi hicho cha Wekundu wa Msimbazi.

Inadaiwa kuwa Mayanja ni kocha mkali asiyependa kuyumbishwa na wala huwa hana masihara hasa katika masuala ya nidhamu jambo ambalo mara nyingi lilimuingiza katika mifarakano ya mara kwa mara na wachezaji wa klabu hiyo. Si tumezoea uzembeuzembe! Indaiwa kocha huyo ni mtu mwenye mazoezi magumu, mkali na mwenye msimamo jambo ambalo wachezaji wengi ndani ya klabu hiyo walikuwa hawalifurahii. Mayanja hapendi wachezaji wavivu wa mazoezi na wasio na nidhamu na hakusita kuwapa adhabu wachezaji wengi waliokwenda kinyume na utaratibu wake.

Aliwahi kumpa adhabu beki Abdi Banda ambaye aligoma kuingia uwanjani kuchukua nafasi ya Mohamedy Hussein ’Tshabalala’ akidai bado Tshabalala alicheza vizuri na alimuondoa mchezaji huyo katika mipango yake na kuibua mgawanyiko ndani ya timu hiyo wengine wakipinga na wengine wakikubaliana na uamuzi wa kocha huyo.

Pia Mayanja amekanusha maneno yaliyokuwa yakizushwa kuwa alikuwa akimuongoza kocha mkuu Joseph Omog katika uamuzi kadhaa. Beki wa zamani wa Simba, Boniface Pawasa anasema licha ya sababu ya kifamilia kutajwa kumuondoa Mayanja ndani ya timu hiyo lakini anachojua sababu kubwa iliyomuondoa ni kutokuwa na maelewano mazuri na wachezaji.

“Nilikaa na baadhi ya watu wa karibu na timu na walisena Mayanja hakuwa na maelewano mazuri na wachezaji na hiyo ni moja ya sababu iliyofanya kuondolewa. Sawa kocha lazima uwe na misimamo lakini si wakati wote.