KAKAKUONA: Lazima tujiunge CCM kumuunga mkono JPM?

Muktasari:

·Sababu kubwa aliyoitoa, kama ilivyokuwa kwa madiwani na viongozi wengine waliojiondoa upinzani, ni utendaji uliotuka wa Rais John Magufuli.

Nimeshtushwa kidogo na wimbi la viongozi wa kisiasa kuhama kutoka vyama vya upinzani na kujiunga na CCM, ili eti kumuunga mkono Rais John Magufuli.

Ninajiuliza sipati majibu, kwamba ili uonekane unamuunga mkono Rais kwa namna anavyoiongoza nchi ni lazima mtu awe ndani ya CCM.

Vivyo hivyo, ninajiuliza pia, hivi kwa wale ambao si wanachama wala wafuasi wa vyama vya siasa lakini wanamuunga mkono Rais wetu, nao wanatakiwa wahamie CCM wakati hawaamini katika itikadi hiyo?

Tumeshuhudia madiwani katika mikoa ya Arusha, Kilimanjaro na Iringa na baadaye mbunge wa Kinondoni (CUF), Maulid Mtulia kujiondoa katika chama hicho na kujiunga na CCM.

Sababu kubwa aliyoitoa, kama ilivyokuwa kwa madiwani na viongozi wengine waliojiondoa upinzani, ni utendaji uliotuka wa Rais John Magufuli.

Mtulia alienda mbali kidogo na kueleza kuwa kwa vile yeye yuko upinzani na ilani inayotekelezwa ni ya chama tawala ambacho ni CCM, inamuwia vigumu kutekeleza yale aliyoahidi.

Nimejiuliza sana kwamba hivi kazi hasa ya mbunge ni ipi? Na Je, ili kuisimamia Serikali atatumia majukwaa gani ya kisheria ili kuwawakilisha wananchi wake na kutetea maslahi yao?

Ibara ya 63(2) ya Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ya mwaka 1977, imelipa Bunge na wabunge mamlaka ya kuisimamia na kuishauri Serikali na vyombo vyake vyote katika utendaji kazi.

Lakini si hivyo tu, mbunge kwa nafasi yake ni diwani wa Halmashauri iliyopo katika jimbo lake, vyombo hivi viwili ndivyo vyenye jukumu la kusimamia maendeleo ya wananchi.

Sasa unapomuona mbunge na diwani anaacha wadhifa wake ili eti aende kumuunga mkono Rais ambaye hata mimi nisiye na chama namuunga mkono, napata wakati mgumu kidogo kuelewa.

Kwamba unaacha Bunge na Baraza la Madiwani ambavyo ni silaha muhimu ya kumsaidia Rais Magufuli kutekeleza ahadi zake kwa Watanzania, ili ukose jukwaa na bado tuamini sababu unazotueleza! Ajabu.

Ipo mifano mingi tu ya viongozi wa upinzani wanaomuunga mkono Rais Magufuli na hata wengine kupewa majukumu ndani ya Serikali wakiwa upinzani, lakini hawajashindwa kumuunga mkono Rais.

Mathalani, mkuu wa mkoa Kilimanjaro, Anna Mghwira ni mwanachama wa ACT-Wazalendo na bado ni mkuu wa mkoa na hajawahi kushindwa kumsaidia Rais Magufuli.

Mwenyekiti wa Tanzania Labour Party (TLP), Augustino Mrema ni mwenyekiti wa Taifa wa Bodi ya  Parole na ameteuliwa na Rais Magufuli, mbona hajalalamika kuwapo kwake upinzani kunamkwamisha JPM?

Wapo viongozi wa upinzani ambao kama John Cheyo wa UDP na Fahmi Dovutwa wa UPDP, wanamuunga mkono Rais Magufuli kwa baadhi ya mambo lakini bado ni viongozi wa vyama vyao.

Ni lazima tukubali kuwa kuna faida kubwa katika taifa ya kuwa na vyama vya upinzani, hasa linapokuja suala la “checks and balance”, Serikali ya CCM ni vigumu sana kujikosoa yenyewe.

Nilifarijika sana na kauli ya Rais mstaafu, Jakaya Kikwete aliyoitoa akiwa ughaibuni Agosti mwaka huu, na kuvitaka vyama vinavyotawala kutoviona vyama vya upinzani kama maadui.

Vyama tawala kama ilivyo CCM, vinatakiwa viuchukulie upinzani kama kioo cha kujitazama na si maadui kiasi kwamba tufike mahali hata tusishirikiane kwenye shughuli za kijamii. Hapana.

Wapo Watanzania wengi tu tunaomuunga mkono Rais, lakini hatuna vyama, leo mkituambia ili uonekane unamuunga mkono JPM kindakindaki lazima uwe CCM, hakika hamtutendei haki.

CCM isifikiri kwa kuua upinzani ndio itaendesha nchi vizuri, la hasha, matokeo yake itakosa wa kuiambia kama imeanguka au imesimama au iko uchi au imevaa nguo ili iweze kujisahihisha. Tuachane na usanii huu wa kisiasa.

0769600900