Lema atafakari, abadilishe mbinu za kutetea haki yake

Mkurugenzi wa Matenity Afrika, Dk Endrew James akipiga magoti kumbembeleza Mbunge wa Arusha Mjini, Godbless Lema (kushoto) aliyekuwa akimlalamikia Mkuu wa Mkoa wa Arusha, Mrisho Gambo wakati wa hafla ya uzinduzi wa mradi  wa ujenzi wa Hospitali ya Mama na Mtoto, mkoani humo wiki iliyopita. Picha na Maktaba

Muktasari:

  • 9bil: Kiasi cha fedha kitakachotumika kujenga hospitali na mama na mtoto.
  • 2010: Mwaka ambao Lema alichaguliwa kwa mara ya kwanza kuwa mbunge.   annual TZ education budget could to lose for donor non-compliance.

Sipendi kuandika kuhusu watu lakini wakati mwingine inabidi, kama leo kwa mfano baada ya lile tukio la aibu la Arusha.

Tunaambiwa kuwa watu wenye akili ndogo wanajadili watu, wenye akili ya kati wanajadili matukio na wenye akili kubwa wanajadili masuala.  Lakini wakati mwingine ni bora kuwa katika kundi la wenye akili ndogo tuwaseme watu ili wengine wajifunze.

Nazungumzia mkasa kati ya Mkuu wa Mkoa wa Arusha, Mrisho Gambo na Mbunge wa Arusha Mjini, Godbless Lema. Mkasa wenyewe ni vurugu zilizoibuka baina ya wawili hao katika hafla ya uwekaji wa jiwe la msingi katika hospitali ya mama na mtoto inayojengwa eneo ya Buruka nje kidogo ya Jiji la Arusha.

Dalili ya vurugu ilianza baada ya Gambo kudaiwa kutaka ratiba iliyokuwa imepangwa na waandaaji wa hafla hiyo ikimjumuisha Lema kama mzungumzaji, ibadilishwe; jambo ambalo halikumfurahisha mbunge huyo.

Inasemekana Gambo awali alifikia hata kutoa sharti kuwa ili yeye awepo, Lema asiwepo eneo hilo. Pia kwa mujibu wa Lema, Gambo alilazimika kuja baada ya kuwapigia wakubwa wake, ambao inaonekana nao walimsema.

Hata hivyo, kizaazaa  chenyewe kilichoaibisha nchi nzima mbele ya wafadhili wa Shirika la Kuhudumia Afya ya Mama na Mtoto  - Maternity Africa, kiliibuka baada ya  Gambo, aliyekaribishwa  jukwaani na Mkuu wa Wilaya ya Arumeru Alexanda Mnyeti,  kuanza kuzungumza.

Inaonekana mkuu huyo wa mkoa katika hotuba yake alielezea historia ya mradi aliyoamua kuihariri, ikifuta ukweli juu ya mchango wa Lema na Taasisi ya Maendeleo Arusha (ArDF)   katika kufanikisha mradi huo utakaogharimu kiasi cha Sh9 bilioni, hususan katika kufanikisha upatikanaji wa eneo la kujenga mradi wa hospitali hiyo.

Lema alikerwa na hotuba hiyo na kushindwa kujizuia  na  kusimama na kupinga hotuba hiyo akisema imejaa upotoshwaji na siasa ndani yake.

Kwa mujibu wa vyanzo mbalimbali, Lema alisema ndiye alitafuta eneo hilo la ujenzi wa hospitali hiyo kutoka kampuni ya Mawala Advocate na siyo kweli kwamba eneo hilo limetokana na maono aliyokuwa nayo Marehemu Advocate Nyaga Mawala ya muda mrefu. Wananchi nao wakaanza kumuunga mkono Lema na kumzomea Mkuu wa Mkoa.

Inaonekana wawili hawa wamekuwa na historia ya mapambano kwa muda mrefu.Huu ni mwendelezo wa vita hii, lakini safari hii busara imeshindwa kuwaongoza kuwa hapakuwa mahali wala muda sahihi wa kufanya utoto na siasa kwani heshima ya nchi ilikuwa rehani.

Mtandao mmoja umeandika kuwa wafadhili kutoka Ulaya waliokuwa kwenye uzinduzi huo, walijikusanya makundi na kumkumbatia Mtendaji Mkuu wa Taasisi ya Maternity Afrika, Andrew Brown, wakimpa pole kwa kile kilichotokea, huku baadhi wakilia kuonyesha ni kwa kiasi gani hawakuridhishwa na mvutano kati ya mkuu wa mkoa, mbunge na wananchi.

Matumizi mabaya ya madaraka

Alichofanya Mrisho Gambo ni matumizi mabaya ya madaraka yake ya ukuu wa mkoa kujaribu kumkandamiza kisiasa kiongozi mwenzake, tena mbunge aliyechaguliwa na wananchi. Ubabe wa Gambo unaweza kutokana na mambo mawili.

Kwanza, ni lile nililolitaja awali, wawili hawa wana ‘bifu’ na  Gambo alikuwa anataka kuvuna pointi katika mpambano wao.

Pili, huenda Gambo anafanya kazi aliyotumwa na bosi wake. Tunajua kuwa kihistoria moja ya kazi ya ma - DC na ma-RC ambayo haitajwi ni kulinda masilahi ya chama tawala, kutegemeana na eneo.

Kwa Arusha, jiji ambalo ni ngome ya Chadema, njia bora ya kulinda masilahi ya chama tawala ni kufifisha ushawishi wa wanasiasa wa upinzani, jambo ambalo Gambo anasifiwa kuwa amekuwa akilifanya kwa ufanisi.

Waliotunga uongo kuwa Gambo ametumbuliwa wanasahau kuwa kwa mtazamo wa CCM, ambayo Rais John Magufuli ni mwenyekiti wake, ile ni kazi nzuri na usishangae siku moja akimsifu hadharani.

Tayari nimemsikia Gambo akimnukuu Rais aliyeongea naye kwa simu akimwambia kuwa ana ‘full confidence’ na yeye.

Lema kaingia mtegoni 

Gambo huenda alisema uongo katika hotuba yake lakini amefanikiwa kisiasa kumchokonoa Lema hadi mbunge huyo akajikuta anashindwa kudhibiti ghadhabu zake na kuishia kufanya mambo ya aibu. Aliyekutwa na nyama ndiyo mwizi.

Ukiangalia video zilizokuwa zikirushwa mitandaoni, ni Lema ndiye aliyekuwa amehemkwa, jazba zimempanda, anafoka kama anataka kupiga mtu wakati Gambo alikuwa ametulia anazungumza kwa utaratibu akimsihi anyamaze amalize hotuba yake.

Gambo akapata pointi zaidi pale alipozuia polisi asimshughulikie Lema ambaye kwa mujibu wa video zilizosambaa alikuwa akionekana akimfanyia fujo Gambo kwa kuingilia hotuba yake.

Gambo, akiwa Mkuu wa Mkoa angeweza kuamuru Lema akamatwe, awekwe ndani lakini hakufanya hivyo na uamuzi wake wa kutotumia nguvu umemfanya aonekane mwenye busara zaidi kati ya wawili hao.

Jambo jingine lililomchafua Lema ni yule mwanamke, ambaye huenda ni mkubwa kiumri ukilinganisha na Lema, alipopiga magoti huku akilia, akimwomba atulie amuache mkuu wa mkoa azungumze anachotaka kuzungumza.

Kama Lema ni mwelewa, basi atakuwa amejua kuwa yule mama alikuwa akimpa somo la busara. Siyo kwamba yule mwanamke alikuwa haelewi kuwa Gambo ni mvurugaji, lakini hakuona sababu ya Lema kufanya fujo zote zile na kuharibu mkutano na sifa ya nchi. Lema angeweza kutulia na kupambana na Gambo baadaye.

Katika dunia ya leo ambayo kuna vyombo vya habari vingi vikuu na vya kijamii Lema angeweza kumuacha Gambo afanye majigambo yake na kisha naye azungumze na vyombo vya habari na hata kusambaza waraka mitandaoni ili wapigakura na wananchi waelewe mchango wake katika mradi huo na kurekebisha uongo wa Gambo.

Mwandishi ni mchambuzi wa masuala ya siasa na jamii, anapatikana kwa barua pepe: [email protected] na [email protected]