Leo Rwanda, kesho Kagame atafaulu Afrika nzima?

Muktasari:

  • Ameshaweka wazi kwamba anataka kulifanya Bara hilo kuwa “kubwa“. Hilo ndilo jambo muhimu kwake. Alitangaza hayo katika hotuba yake kwenye ufunguzi wa mkutano wa kilele wa AU.

Paul Kagame ni rais wa moja kati ya nchi ndogo sana katika Bara la Afrika, lakini yeye sasa amekamata uenyekiti wa Umoja wa Afrika, AU, baada ya mkutano wa kilele wa Umoja huo mjini Addis Ababa, Ethiopia, mwezi Januari.

Ameshaweka wazi kwamba anataka kulifanya Bara hilo kuwa “kubwa“. Hilo ndilo jambo muhimu kwake. Alitangaza hayo katika hotuba yake kwenye ufunguzi wa mkutano wa kilele wa AU.

“Hakuna nchi au kanda ambayo yenyewe tu inajitosheleza, lazima mambo yetu yaende, na lazima tushikamane,” alisema kiongozi huyo.

Mwaka uliopita Kagame alishirikiana na Rais wa AU aliyemwachia wadhifa huo, Alpha Conte, Rais wa Guinea. Waliingiza ‘hewa’ mpya katika AU iliyokuwa imelemaa. Kama kiongozi wa kamati ya kuifanyia marekebisho AU, alikuwa na usemi mkubwa mwaka 2013 katika kupitishwa mpango wa AU wa miaka 50 uliopewa jina la Ajenda 2063. Jambo muhimu katika mpango ni kuiunganisha Afrika.

Mpango huo unataka Waafrika wote wasilazimike kuwa na viza wanaposafiri baina ya nchi moja ya Afrika kwenda nyingine au pale wanapoivuka mipaka ya nchi zao; unataka kuweko pasipoti ya aina moja kwa nchi zote za Afrika.

Yaani, unataka kuondosha mtindo wa kutakiwa vibali vya kufanyia kazi kwa Waafrika pale wanapokuweko katika nchi yeyote ya Kiafrika; na bidhaa zipite bila ya ushuru miongoni mwa nchi za Kiafrika.

Katika mkutano huo wa kilele wa 30 wa AU, Kagame ametaka pia kuweko soko la usafiri la pamoja la Afrika nzima; kuweko anga ya pamoja na usafiri wa pamoja wa mizigo, huku mipaka baina ya nchi za Kiafrika ikitoweka.

“Tumo tayari kuamua kuwa na eneo huru la biashara ya pamoja - jambo hilo lazima lifanyike mwaka huu,” alisema Rais huyo wa Rwanda. “Watu wanastahili kuwa na mustakabali wenye kung’ara,” aliongeza.

Waafrika wengi wanamsifu na kumshangilia kiongozi huyo. Wanamuona kuwa ni mwanamageuzi aliyefanikiwa kuituliza Rwanda, nchi ambayo mwaka 1994 ilishuhudia mauaji ya kimbari ambapo watu milioni moja waliuawa, pia kuwezesha nchi hiyo ipige maendeleo, kutokuwa na ufisadi na rushwa na kuvutia uwekezaji.

Waafrika wengi wanatarajia kwamba Kagame ataweza pia kuisukuma mbele Afrika nzima. Katika hotuba yake alitoa wito moja kwa moja kwa vijana wa Kiafrika wanaopoteza maisha yao wakitafuta bahati kwa kukimbilia Ulaya.

“Hatuwezi kuijenga Afrika bila ya nyinyi,” alisema. Kwa vijana wengi wa Kiafrika, AU ni klabu ya wazee isiyokuwa ya kidemokrasia. Japokuwa pia udemokrasia unaodaiwa na Kagame mwenyewe katika nchi yake una alama nyingi za kuuliza.

Hata hivyo, yaonyesha yeye ana nia ya kweli ya kutaka mambo yaende mbele, na vijana wanaweza kuweka matarajio kwake.

AU iko katika mzozo. Umoja huo uliundwa mwaka 2011 kutokana na fikra ya Rais wa Libya wa wakati huo, Muammar Gaddafi, na kugharimiwa kutokana na fedha za nchi hiyo ya Afrika Kaskazini zilizotokana na petroli.

Lakini AU, baada ya kuuawa Gaddafi na kuangushwa utawala wake, ilikosa amani na maono. Mwaka 2015 karibu robo tatu ya bajeti ya AU ilitolewa na wafadhili wa kimataifa, kama vile Marekani na Umoja wa Ulaya.

Katika mkutano wa kilele uliofanywa Rwanda mwaka 2016 iliamuliwa kufanya marekebisho juu ya namna ya kuzigharimia shughuli za AU. Ilitakiwa kwamba asilimia 0.2 ya kodi ya mapato ya bidhaa zinazoingia Afrika iende AU. Lakini ni nchi za Kiafrika 14 tu kati ya 55 zilizotekeleza jambo hilo.

AU kutegemea wafadhili ni jambo la hatari. Kuna tuhuma kwamba jengo la AU lililoko Addis Ababa na ambalo lilijengwa na Wachina na kufunguliwa mwaka 2012 lilipachikwa vifaa vya kusikilizia mazungumzo ya watu.

Iligunduliwa kwamba vifaa hivyo vilikuwa vinanasa sauti vikiwa chini ya meza za ofisi katika jengo hilo. Wachina wamezielezea tuhuma hizo kuwa ni “upuuzi mtupu“.

Hata hivyo, tuhuma juu ya mkasa huo inaonyesha vipi ilivyo muhimu kwa Afrika kutegemea nguvu zake zenyewe.

Unaweza kusema kwamba Afrika inaungua kutokana na matatizo yake mengi ya kijamaa, kiuchumi, achilia mbali yale ya kisiasa.

Kila mwaka zaidi ya vijana milioni kumi wanaingia katika soko la kutafuta ajira, asilimia kubwa yao wanamalizikia patupu, na hivyo kulifanya Bara hilo lizidi kukosa usalama: Miji mikubwa, kutoka Cairo hadi Kinshasa inapasuka, hamna mtu anayewekeza katika miundombinu ya maana kwa ajili ya wananchi.

Maeneo makubwa ya ardhi yanakaliwa na watu waliopoteza matarajio juu ya hali zao za kijamaa kuwa bora, huku watu wakikosa hifadhi ya kukabiliana na uharibifu mkubwa wa mazingira unaofanywa mbele ya macho yao.

Wakati wako watu wachache fulani pembeni wananeemeka na kunenepa kupita kiasi kutokana na utajiri wa kuiba, nchi nyingine zinaangukia zaidi kwenye mizozo mikubwa. Matokeo ni mawimbi makubwa ya wakimbizi wanaotangatanga huku na kule.

Mara nyingi sisi Waafrika tunapozongwa na migogoro ambayo kwa sehemu kubwa tunaisababisha wenyewe, hutoa miito na kusema: “Matatizo ya Kiafrika yapatiwe ufumbuzi wa Kiafrika”.

Ndio na ni vizuri, lakini huo tunaoita ufumbuzi ya Kiafrika huwa ni chanzo kingine cha matatizo mapya ya Kiafrika. AU ambayo mwanzo wa karne hii iliundwa kama jumuiya kubwa ya kimataifa ya ushirika wa mataifa mbalimbali, pembeni mwa Umoja wa Mataifa, ilitakiwa iyatanzue matatizo ya Afrika.

Hilo halijawezekana na yote imetokana na ukosefu wa uwezo wa kuongoza, ukosefu wa nia safi, ukosefu wa umoja, na bila shaka yeyote ukosefu wa fedha.

Je, sasa Paul Kagame ataweza kuibadilisha hali hii? Huenda. Anatoa matumaini, licha ya mtindo wake wa utawala wa kibabe katika nchi yake. Ameiongoza Rwanda kuwa nchi ya kisasa, dirisha la kuonyesha kwamba Waafrika wanaweza kuendesha vizuri mambo yao, tena kwa mipango.

Amedhihirisha ana nguvu za kuongoza kuelekea kwenye njia iliyo bora na pia ana nia. Yeye anategemea umoja miongoni mwa viongozi wenzake wa Kiafrika na pia fedha kutoka hazina za nchi zao. AU haiwezi kuendeshwa kwa sadaka za nchi za nje. Katika dunia ya sasa ni nadra kutolewa sadaka, bali kinachotawala ni maslahi. Yule anayefadhili anataka aimbiwe nyimbo zake anazozipenda tu.

Kagame atahitaji afanye kazi bega kwa bega na marais wengine wa Afrika, angalau kuifanya AU ifanye kazi vizuri zaidi kuliko hapo kabla. Iko tamaa, kwani hata marais wenzake wanathamini maendeleo makubwa ambayo Rwanda imeyafanya.

AU itakayofanya kazi vizuri haitobadilisha maisha ya Waafrika wengi, lakini jambo moja ni wazi: Itaonesha kwamba Afrika inaweza kutanzua matatizo yake kwa mikono yake yenyewe. Sura hiyo nzuri itawafanya watu wa mataifa mengine nje ya Afrika mwishowe watambue haja ya kumimina fedha zao na kuziweka Afrika.

Afrika inahitaji uwekezaji huo, tena kwa haraka iwezekanavyo. Pindi Kagame anafaulu katika hilo, basi atakuwa amelifikia lengo lake.