Licha ya msamaha wa Rais, bado magereza yanaelemewa nchini

Baadhi ya wafungwa walioachiwa huru kwa msamaha wa Rais John Magufuli, Chananja Luchagula mwenye umri wa miaka 77 (kushoto) na Benjamin Wandwi mwenye umri wa miaka 67 wakitoka katika Gereza kuu la Butimba jijini Mwanza jana. Picha na Michael Jamson

Muktasari:

  • Ushirikiano huu unahitajika kati ya Jeshi la Polisi linahusika na upelelezi wa makosa ya jinai, ofisi ya Mwendesha Mashtaka wa Serikali (DPP), mahakama na taasisi nyingine kama ya kuzuia na kupambana na rushwa (Takukuru) kuharakisha hukumu za mahabusu ambao ni wengi kuliko walio-hukumiwa.

Licha ya Rais kutoa msamaha kwa wafungwa zaidi ya 8,000 kwenye maadhimisho ya uhuru wa Tangan-yika, takwimu zinaonyesha ushirikiano na juhudi zaidi zinahitajika kati ya taasisi za haki kupunguza msongamano magerezani.

Ushirikiano huu unahitajika kati ya Jeshi la Polisi linahusika na upelelezi wa makosa ya jinai, ofisi ya Mwendesha Mashtaka wa Serikali (DPP), mahakama na taasisi nyingine kama ya kuzuia na kupambana na rushwa (Takukuru) kuharakisha hukumu za mahabusu ambao ni wengi kuliko walio-hukumiwa.

Uhuru wa taasisi hizi ni muhimu pia kwani watafiti wanasema hukumu za watu wanaokabiliwa na tuhuma za wizi, biashara ya dawa za kulevya au mauaji hutegemea hadhi yao kwenye jamii. Matai-fa mbalimbali huwahukumu tofauti waha-rifu wa makosa ya jinai.Hata vifungo vyao, hutofautiana vile-vile. Wapo wanaohukumiwa muda mrefu jela wakati wengine wakipewa adhabu ndogo inayoruhusiwa kisheria. Kosa hilo hilo, ukilifanya Afrika; mathalan Tanzania hukumu yake itakuwa tofauti ukilitenda nchini China au Marekani, kwa mfano.Kutokana na uzoefu wa mataifa mbalim-bali, Taasisi ya Utafiti wa sera za Makosa ya Jinai (ICPR) kwenye ripoti yake ya Hali ya Magereza Duniani (WPB), inasema mfumo wa magereza na jinsi wafungwa wanavyohudumiwa hutoa picha ya jinsi Serikali inavyowajali wananchi wake hasa wa kipato cha chini. Kuonyesha namna wafungwa wasivyope-wa kipaumbele hata na Serikali zao, Rais wa kwanza wa afrika Kusini, Nelson Man-dela aliwahi kusema hakuna anayelijua taifa kama hajafungwa. Nchi hazitakiwa kutukuzwa kwa jinsi zinavyowahudumia viongozi wake isipokuwa wananchi wa hali ya chini. Namna wafungwa wanavyohudumiwa humaanisha jinsi Serikali inavyowajali wananchi wake. Kuonyesha msisitizo, Mandela alisema: “Ninaamini, namna nzuri ya kulielewa taifa ni kufahamu watu wa aina gani inaamua wafungwe na kwa sababu zipi.”

Kwenye sherehe za maadhimisho ya miaka 56 ya uhuru wa Tanganyika, Rais John Magufuli aliyatumia mamlaka aliyokasimiwa chini ya Ibara ya 45 (1) ya Katiba ya nchini kuwapa msamaha wafungwa 8,157.

Kati ya wafungwa hao, 1,828 walioachiwa huru na 6,329 walipunguziwa adhabu. Kwenye orodha hiyo, walikuwamo 61 kati ya 522 wanaosubiri kutekelezwa kwa adhabu hiyo. Ni wawili tu, Nguza Viking maarufu kama Babu Seya na mwanaye, Johnson Nguza anayejulikana zaidi kama Papii Kocha kati ya wafungwa 666 waliohukumiwa kifungo cha maisha, waliachiwa huru.

Tanzania

Kama walivyo jirani zake, Tanzania ina idadi kubwa ya mahabusu waliomo magerezani hivyo kuyafanya yafurike kuliko uwezo wake. Ndani ya miaka miwili, zaidi ya watuhumiwa 8,000 wameongezeka; ama walishahukumiwa au wanasubiri kukamilika kwa ushahidi wa tuhuma zinazowakabili.

Msamaha alioutoa Rais, kwa kiasi umepunguza msongamano uliopo kwenye magereza yote nchini ambao kabla ya uamuzi huo, Dk Magufuli alisema kulikuwa na jumla ya wafungwa 39,000 ambao wamepungua mpaka 37,000.

Pamoja na msamaha huo, Tanzania inaendelea kuwa miongoni mwa mataifa yenye idadi kubwa kuliko uwezo wa magereza yake kutunza wafungwa na mahabusu duniani.

Taarifa za WPB mwaka 2015, zinaonyesha kulikuwa na wafungwa 31,382 ambao ni sawa na asilimia 115.7 ya uwezo wa magereza yote nchini kuhifadhi wafungwa.

Kwa wakati huo, WPB ilisema uwezo wa Tanzania ni kuhifadhi wafungwa 29,552. Hata hivyo, juhudi kubwa zinafanywa kuboresha mazingira ya watuhumiwa na wafungwa waliopo magerezani. Wafungwa hao wanahifadhiwa kwenye magereza 126 yaliyokuwapo mwaka 2015.

Kati ya wafungwa waliokuwapo mwaka 2015, asilimia 53.1 walikuwa mahabusu. Kwa mfumo wa kisheria nchini, mahabusu hupoteza miaka kadhaa gerezani kabla ya tuhuma zao hazijahukumiwa.

Alipokuwa akitangaza msamaha kwa wafungwa 8,157; Rais alimtaja Mganga Matonywa, mzee mwenye miaka 85 ambaye amekuwa kifungoni kwa miaka 37 tangu alipohukumiwa. Wakati anapewa adhabu hiyo, tayari alishasota lumande kwa miaka saba ya kusikilizwa kwa kesi yake hivyo kufanya jumla ya miaka 44 aliyoishi jela.

Mkurugenzi wa Kituo cha Haki za Binadamu (LHRC), Dk Hellen Kijo-Bisimba anasema ipo haja ya kuangalia namna ya kutekeleza hazi za watuhumiwa wa makosa mbalimbali kulingana na walichokifanya.

“Magereza yetu yamejaa zaidi mahabusu. Hata baadhi ya waliohukumiwa wanatumikia vifungo virefu. Hawa wangeweza kupewa adhabu mbadala na kupunguza msongamano uliopo,” alisema Dk Kijo-Bisimba.

Alipokuwa akiwasilisha hotuba ya bajeti ya mwaka huu, Waziri wa Mambo ya Ndani, Dk Mwigulu Nchemba alisema yapo malalamiko ya wananchi kubambikiwa kesi na katika kipindi cha Julai, 2016 hadi Machi, 2017 Jeshi la Polisi lilipokea malalamiko 206 ambayo yameongezeka kutoka 138 ikilinganishwa na kipindi kama hicho mwaka 2015/16 yalipokuwa 68. Hatua zilichukuliwa kwa jeshi hilo kuwafukuza kazi askari 14 na maofisa wawili pamoja na kuwashusha vyeo askari wanne huku wengine sita wakipewa adhabu nyingine.

Kuhusu adhabu mbadala, alisema Jeshi la Magereza linayo programu ya adhabu licha ya kifungo cha gerezani ambayo kato ya Julai 2016 hadi Machi, wafungwa 1,995 wamenufaika. Miongoni mwao; 456 wametumikia adhabu ya probesheni na 1,539 adhabu ya huduma kwa jamii.

Aidha, wafungwa 794 wamemaliza adhabu zao na kuachiwa huru hivyo kupunguza gharama za uendeshaji. Kwa sasa, idara hiyo ina uwezo wa kuwatoa gerezani na kuwasimamia wafungwa 6,000 wenye sifa za kutumikia vifungo vya nje kwa mwaka ambao wakiendelea kuwepo wanaigharimu Serikali Sh3.285 bilioni za chakula na huduma.

“Kiasi hicho kingeweza kuokolewa endapo wafungwa hao wangetumikia vifungo vyao nje ya magereza kwa kutumikia adhabu mbadala. Kwa kuzingatia umuhimu huo, Serikali imetenga Sh1.045 bilioni ili kuongeza idadi ya wanaotumikia vifungo nje wafike 4,000,” alisisitiza Dk Mwigulu.

Kufikishwa gerezani kwa wavunjaji wa sheria mbalimbali licha ya kuongeza msongamano, utafiti unaonyesha kunayafanya yawe hatari kwa maisha ya binadamu kwani huweka rehani ustawi wa wafungwa na askari wanaowahudumia.

Licha ya gharama kubwa zinazotumika kuwahudumia wafungwa hao, taifa linapoteza nguvukazi muhimu ambayo ingeweza kuitumia kwa uzalishaji mali au huduma zinazohitajika hivyo kukuza uchumi.

Takwimu zilizopo zinaonyesha, kwa sasa, duniani kote kuna zaidi ya wafungwa milioni 10 huku Marekani ikiongoza kwa wingi ambayo kati ya mwaka 1980 mpaka 2008 idadi iliongezeka kutoka 500,000 hadi milioni 2.3.

Hali ilikuwa hivyo Brazil pia ambako idadi hiyo iliongezeka kutoka 30,000 waliokuwapo mwaka 1973 mpaka 600,000 mwaka huu. Uingereza, waliongezeka kutoka 40,000 waliokuwapo mwaka 1975 mpaka 87,000 mwaka 2012.

Afrika Mashariki

Pamoja na udogo wake, Rwanda imejenga magereza yenye uwezo mkubwa zaidi Afrika Mashariki. Ikiwa na jumla ya watu milioni 12.5 kwa makadirio ya Umoja wa Mataifa mwaka 2015, ilikuwa na wafungwa 54,279 ambao ni sawa na asilimia 95.6 ya uwezo wa magereza 14 iliyonayo.

Magereza hayo yanaweza kuhifadhi wafungwa 56,782. Kati ya wafungwa waliopo nchini humo, asilimia 6.8 kati yao walikuwa mahabusu ambao kesi zao zinaendelea kusikilizwa.

Mpaka Oktoba, Uganda ilikuwa na wafungwa 54,059 kwenye magereza 249 yaliyomo nchini humo. Idadi ya wafungwa waliomo nchini humo ni sawa na asilimia 293.2 ya uwezo wake wa kuwahudumia wananchi wahalifu 16,612. Kati ya wafungwa hao waliopo gerezani, asilimia 54.2 ni mahabusu.

Taifa changa zaidi Afrika, Sudan Kusini lina magereza madogo 80 yaliyokuwa na wafungwa 6,504. Inaelezwa kwamba Gereza la Juba ambalo mpaka mwaka 2015 lilikuwa bado linajengwa ndilo kubwa linaloweza kuhifadhi wafungwa 400 lakini mpaka Septemba mwaka huo lilikuwa nao na 1,317.

Miongoni mwa wafungwa hao, asilimia 28.9 walikuwa mahabusu. Mwaka huo, Sudan Kusini ilikuwa na jumla ya watu milioni 12.45.

Mpaka Agosti mwaka jana, Kenya ilikuwa na wafungwa 53,841 kwenye magereza 108 iliyonayo. Idadi hiyo ni sawa na asilimia 201.7 ya uwezo wa kuhifadhi watuhumiwa hao. Kenya inaweza kuhudumia wafungwa 26,687.

Kati ya wafungwa hao, asilimia 43.1 ni mahabusu wanaosubiri hukumu ya tuhuma zinazowakabili.

Mpaka mwishoni mwa mwaka jana, Burundi ilikuwa na wafungwa 10,049 lakini zaidi ya nusu, asilimia 50.4 wakiwa ni mahabusu. Licha ya kuwa na idadi ndogo zaidi ya watu, milioni 11.74, ikilinganishwa na wanachama wengine wa Jumuiya ya Afrika Mashariki (EAC), idadi hiyo ilikuwa sawa na asilimia 239.6 ya uwezo wa magereza yake 11 yanayomudu wafungwa 4,194 pekee.