Lishe shuleni inavyokuza ufaulu mkoani Njombe

Baadhi ya wanafunzi mkoani Njombe wakipata chakula cha mchana shuleni. Mkoa huu umefanikiwa kwa kiwango kikubwa kuhamasisha wazazi kuchangia lishe kwa watoto wao wakiwa shuleni. Na Mpiga Picha Wetu 

Muktasari:

NUKUU

“Ilibidi tuanze kutoa elimu kwa wazazi wote na walezi waone ya kuwa jukumu la kuhakikisha watoto wanapewa chakula shuleni linawahusu. Walilipokea kwa mikono miwili na tumefanikiwa kwa asilimia 100,’’

Stephen Bange (Ofisa elimu taaluma)

Je, unataka kupandisha ufaulu na kupunguza utoro shuleni mkoani kwako? Jaribu siri hii kutoka Mkoa wa Njombe.

Ofisa elimu taaluma wa mkoa huo,  Steven Bange, anasema siri iko katika kutambua umuhimu wa chakula kwa wanafunzi wakati wa masomo.

 Kwa ajili hiyo shule zote za Mkoa wa Njombe zinatoa huduma ya chakula.

“Ilikuwa unaweza kukuta mwanafunzi anasinzia darasani, ukimuuliza nini tatizo, anakuambia njaa! Kiuhalisia si rahisi kwa mtoto huyo kumuelewa mwalimu hata kidogo,” anasema na kuongeza:

“Tuligundua kwamba kumbe si rahisi kwa mtoto kushinda shule kwa saa nane bila chakula. Muda huu unatosha kudhoofisha afya yake na matokeo ni kushindwa kumudu masomo, kwa hiyo, dawa ilikuwa ni shule zote kuingia kwenye mpango wa lishe”.

Kwa upande wake, Mwalimu Mkuu wa Shule ya Msingi Image, Shadrack Sodike, pamoja na kuunga mkono mpango wa chakula shuleni, anasema pia mpango huo unapaswa kuwa endelevu kwani licha ya kusaidia uelewa kwa wanafunzi, umepunguza utoro.

Kwa mujibu wa Bange, tangu Mkoa wa Njombe uanze kutoa chakula, ufaulu shuleni umeongezeka kutoka asilimia 59 mwaka 2013 hadi kufikia asilimia 80 mwaka 2017, baada ya shule zote 480 za msingi na 16 za sekondari kuanzisha huduma hiyo ya chakula.

Anasema kwa maana hiyo wanafunzi 240,987 wa shule za awali, msingi na sekondari tayari wanapata huduma ya chakula shuleni.

Njombe wanatekeleza mpango huo huku takwimu zikionyesha unakabiliwa na tatizo la udumavu na kushika nafasi ya pili kitaifa kwa kuwa na asilimia 49.4.

Wataalamu wa afya, likiwamo Jukwaa la Lishe nchini (Panita) linataja njaa kuwa kati ya sababu zinazoweza kukwamisha ufaulu kwa wanafunzi.

Mtoto anapokwenda shule na kushinda huko bila kupata chakula chochote, hupoteza uwezo wa kufikiri na hivyo kutoelewa darasani hata kama mwalimu atajitahidi  kufundisha.

Twaweza, taasisi ifanyayo tafiti nyingi za mambo ya kijamii inasema katika moja ya tafiti zake kwamba kuna uhusiano mkubwa kati ya matokeo ya watoto kujifunza na udumavu unaotokana na utapiamlo.

Utapiamlo ni matokeo ya mtoto kutokupata chakula cha kutosha na kisicho na virutubisho muhimu mwilini.

Mtaalamu wa lishe na mratibu wa miradi wa Panita, Jane Msagati, anasema uwezo wa kujifunza wa mtoto mwenye utapiamlo ni mdogo kulinganisha na mtoto mwenye afya njema.

Mkoa wa Njombe unatekeleza mpango wa chakula shuleni wakati pia zaidi ya wanafunzi 55,000 kutoka shule 48 za msingi katika Halmashauri ya Jiji la Arusha, wakitarajia kunufaika na mpango wa chakula shuleni unaolenga  kuinua kiwango cha ufaulu.

Njombe walianzaje?

Kimsingi, utoaji wa chakula ulianza mwaka 2012, japo kwa wakati huo shule chache zilikuwa zinafanya hivyo.

Bange anasema matokeo ya wanafunzi yalikuwa yanaonyesha kuwa pamoja na jitihada za walimu kufundisha, ufaulu katika shule zilizokuwa zinatoa huduma ya chakula ulikuwa mzuri zaidi.

Anasema ilibidi kukaa chini na kuona namna wanavyoweza kutekeleza azimio la kuhakikisha kila mwanafunzi wa shule ya msingi na sekondari  anapata chakula.

Anasema hawakuona haya kuwahusisha wadau wengine wakiwamo wanasiasa katika kutekeleza mpango wao.

Hata hivyo, anasema mpango huo ulisuasua baada ya kuja kwa mkakati wa elimu bure uliosababisha wazazi na walezi kuona kwamba hawahusiki katika kuhakikisha watoto wao wanapata chakula shuleni.

“Ilibidi tuanze kutoa elimu kwa wazazi wote na walezi waone ya kuwa jukumu la kuhakikisha watoto wanapewa chakula shuleni linawahusu. Walilipokea kwa mikono miwili na tumefanikiwa kwa asilimia 100,” anasema.

 Ofisa Mtendaji wa Kijiji cha Nyombo, Ohidelis Gwivaha, anasema kijiji chao hakina wasiwasi kuhusu suala la watoto kupewa chakula.

“Unajua tuligundua hata kijiji chetu kina watoto wenye utapiamlo, sasa tulipoambiwa tuchangie wakati huo huo tukielezwa madhara ya njaa kwa watoto, hatukusita kabisa kufanya hivyo,” anasema.

Gwivaha anasema kazi ya serikali ya kijiji hicho ni kuhakikisha wazazi na walezi wote wanatoa chakula na hilo limefanikiwa.

  Anasema pia  wana mpango mahsusi kijijini hapo wa kutoa lishe maalumu kwa watoto wenye tatizo la utapiamlo na maambukizi ya virusi vya ukimwi (VVU).

“Haya yote tunayafanya baada ya kupata elimu ya uhakika ya masuala ya lishe kwa watoto. Hatupendi kuona watoto wetu wanapata utapiamlo, kwa sababu ya uzembe wetu wakati tunao uwezo wa kuhakikisha wanakula,” anasema.

Mkazi wa kijiji cha Ilimiwaha, Thabitha Ndendya, anasema hawalazimishwi kuchangia chakula shuleni baada ya kuelewa umuhimu wake.

“Walivyokuwa wamesema elimu bure tulijua hadi chakula watoto wetu watakula bure, ila sasa tumeelewa tunajitahidi bila kusukumwa,” anasema.

Hali tofauti Ludewa

   Kwa Wilaya ya Ludewa, hasa maeneo ya mwambao wa Ziwa Nyasa, utoaji wa chakula shule upo tofauti.

Bange anasema wamebuni mbinu ya wazazi wa mtaa mmoja kupeana zamu ya kupika na kuwapelekea chakula shuleni watoto wao, kwa kuwa si rahisi kukusanya muhogo na kuhifadhi shule.

   “Kule wanatumia muhogo, huwezi kuukusanya muhogo kwa wananchi na kuuhifadhi shule,” anasema.

Mwalimu Mkuu wa Shule ya Msingi Makula, Clemence Wihombe anasema shule yake haina wasiwasi katika kutekeleza mpango huo.

   Anasema walimu wamejipanga kuhakikisha kuwa kila mwanafunzi anapata chakula jambo lililosaidia kuinua kiwango cha ufaulu kwenye shule hiyo.

Zaidi ya ufaulu, Bange anasema pia ya kuwa Njombe ni kati ya mikoa iliyofanikiwa kupambana na changamoto ya utoro kwa sababu ya utoaji wa chakula.

Mikakati  wa kupambana na uhaba wa walimu

Kwa mujibu wa Bange, chakula ni upande mmoja tu wa jitihada za mkoa huo kukuza elimu na kiwango cha ufaulu.

Anasema katika kupambana na uhaba wa walimu, wametafuta dawa ya kumaliza tatizo hilo kwa kuwatumia walimu wanaosubiri ajira.

Takwimu zinaonyesha mkoa huo unakabiliwa na upungufu wa walimu 670 wa elimu ya awali, 1991 wa shule za msingi na 446 wa masomo ya sayansi katika shule za sekondari.

Anasema kutokana na uhaba huo wa walimu ilifika hatua baadhi ya shule zilibakiwa na walimu wawili, jambo lililotishia maendeleo ya elimu kwenye mkoa huo.

“Kukiwa na walimu wawili maana yake hawapaswi kuugua, mmoja akiugua kwa mwezi tu ni tatizo kubwa, maana yake watoto hawatafundishwa. Jambo hilo lilifanya tukae kutafakari njia za kupambana nalo,” anaeleza.

Anasema kimsingi mtaani wapo walimu wengi waliomaliza masomo yao lakini hawana kazi.

“Tulipogundua hawa wanaweza kutusaidia, ilibidi tuziagize kamati za shule zenye uhaba kuandaa utaratibu wa kuhakikisha walimu hawa wanapewa kazi ya kufundisha kwa ujira mdogo wakati wanasubiri ajira,” anaeleza.