KUELEKEA MWAKA MMOJA WA MAGUFULI : Lowassa aionya NEC, Magufuli atambia barabara

Rais John Magufuli.

Muktasari:

  • Dk Magufuli alisema hayo jana kwenye mkutano wa kampeni uliofanyika Jimbo la Ukonga, Dar es Salaam, muda mfupi kabla ya kwenda kushuhudia utiaji saini wa mkataba wa ujenzi wa barabara za juu eneo la Tazara, wakati Lowassa alitoa kauli hiyo akiwa mjini Magu.

Dar es Salaam/Magu. Mgombea urais kwa tiketi ya CCM, Dk John Magufuli amesifu kazi ya ujenzi wa barabara katika miaka 10 iliyopita, huku mgombea wa Chadema, Edward Lowassa akiituhumu Tume ya Taifa ya Uchaguzi (NEC) kuwa imempotosha Rais Jakaya Kikwete.

Dk Magufuli alisema hayo jana kwenye mkutano wa kampeni uliofanyika Jimbo la Ukonga, Dar es Salaam, muda mfupi kabla ya kwenda kushuhudia utiaji saini wa mkataba wa ujenzi wa barabara za juu eneo la Tazara, wakati Lowassa alitoa kauli hiyo akiwa mjini Magu.

Akizungumzia utendaji wake kwenye mkutano huo, Dk Magufuli alisema katika kipindi cha Serikali ya Awamu ya Nne pekee, Wizara ya Ujenzi aliyokuwa akiiongoza, imefanikiwa kujenga kwa kiwango cha lami barabara za urefu wa kilomita 17,762 na akaahidi kuendelea na kasi ya ujenzi atakapopata fursa ya kuchaguliwa kuwa Rais.

“Kuwepo kwa barabara za lami ndiyo ujenzi wa uchumi imara,” alisema Dk Magufuli. “Leo mnasikia huko Mara kuna watu waliamua kudeki barabara ili mgombea wa chama fulani aweze kupita. Kwanza nawapongeza sana wale vijana kwa kazi ile ya kudeki barabara kwa sababu zingekuwa za changarawe wasingeweza kufanya usafi wa kiwango kile.”

Pia, aliwataka wananchi wasidanganyike na kauli za baadhi ya wagombea kuwa watamaliza tatizo la foleni jijini Dar es Salaam kwa muda wa siku 100, akisema hizo ni sawa na ndoto za mchana.

“Hakuna mwenye miujiza ya kuiondoa foleni kwa siku 100, anayedai ataweza anawadanganya. Ujenzi wa barabara za juu siyo jambo la siku moja, ni suala lenye taratibu na mipango yake na tayari Serikali imeshaianza.

“Leo ninapotoka hapa nakwenda kuweka saini makubaliano ya kuanza kwa ujenzi wa flyovers za Tazara na pale Ubungo, tayari tumepata fedha kutoka kwa wahisani. Tunasubiri kuanza ujenzi wa barabara yenye ghorofa tatu, ya juu, kati na ya chini.”

Dk Magufuli alishambulia makada waliowahi kushika nyadhifa kubwa serikalini ambao wanaiponda Serikali kuwa haijafanya chochote, akisema wengine hawakustahili nafasi hizo.

Pia, alisema vyama vya CCM na Chadema vyote vina mafisadi, lakini akasema waliokuwa chama hicho tawala wameanza kukimbia baada ya yeye kuteuliwa kuwa mgombea urais. “Mafisadi hawapo Chadema pekee, wapo pia CCM na ndiyo hao mnawasikia kila kukicha wanakimbia na mtawasikia na kuwaona wakiendelea kukimbia. Nawahakikishia wataendelea kukimbia maana wananijua mimi sina mchezo. Hapa ni kazi tu,” alisema.

Lowassa aishangaa NEC

Mjini Magu, Lowassa amekuwa mmoja wa watu waliostushwa na idadi ya wapigakura iliyotamkwa na Rais Kikwete na akaitupia lawama NEC kuwa ndiyo iliyompotosha mkuu huyo wa nchi.

Rais Kikwete, aliyekuwa akizungumza kwenye hafla ya kuadhimisha miaka 16 ya kifo cha Baba wa Taifa Mwalimu Julius Nyerere juzi mjini Dodoma, alitaja idadi ya wapigakura walioandikishwa na NEC kuwa milioni 28 wakati idadi iliyotangazwa na tume hiyo ni milioni 22.75.

Jana, Lowassa aliyekuwa akihutubia kwenye mkutano wa kampeni uliofanyika Uwanja wa Sabasaba mjini Magu, alisema kuna kazi kubwa kwa NEC kuhakikisha uchaguzi unafanyika kwa amani.

“Tume ina kazi kubwa sana, wasipoangalia watavuruga uchaguzi na ukivurugwa ni mwanzo wa matatizo katika nchi,” alisema waziri huyo mkuu wa zamani.

“Sielewi inakuwaje Rais anapewa takwimu halafu baada ya saa mbili zinakanushwa? Ni nani anampa Rais takwimu hizi? Tulisema tume ni huru, sasa kwa hali hii ni huru?”

Muda mfupi baada ya hotuba ya Rais, Ikulu ilitoa taarifa ikisema uhakika wa idadi hiyo ni 22,751,292 kwa Bara na 503,193 Zanzibar.

Lowassa, ambaye jana alifanya mikutano mitatu katika majimbo ya Magu, Misungwi, Sumve na Sengerema, aliitaka NEC isifanye mambo yatakayoharibu uchaguzi.

Mgombea huyo, ambaye pia hujinadi kwa kufanikisha mradi wa maji ya Ziwa Victoria, aliahidi kuwaletea wakazi wa Magu maji ya ziwa hilo ili kuwaondolea usumbufu. Alisema yeye ni mtaalamu wa masuala ya maji na wakimpa kura, atakamilisha ahadi yake kwenye mji huo.

Mkazi wa Magu, John Chacha alisema wanakabiliwa na uhaba mkubwa wa maji na kwamba wananunua dumu moja kwa Sh800.

Alisema tatizo jingine ni maeneo ya kilimo kuchukuliwa na Serikali na kugeuzwa kuwa hifadhi na kusababisha wananchi kukosa maeneo ya kilimo.

Mkazi mwingine, Filipo Lucas alitaka kuimarishwa kwa huduma za afya pamoja na elimu.

Hata hivyo, alilalamikia kitendo cha walimu kuagiza wanafunzi kupeleka mahindi shuleni pamoja na mlolongo wa michango shuleni, ambayo alisema inakwaza maendeleo ya elimu.

Kabla ya kumkaribisha Lowassa, Mwenyekiti wa Chadema, Freeman Mbowe aliendelea kupinga kauli ya Rais Kikwete ya kuwataka wananchi kurudi nyumbani baada ya kupiga kura.

“Mimi nasema, tuko tayari kupigwa, lakini hatuondoki mpaka matokeo yatoke. Hatutaki kura za maruhani,” alisema Mbowe huku akiwataka polisi kutenda haki kwa kuwa hawana mpango wa kufanya fujo zaidi ya kulinda kura.

Kingunge Ngombale Mwiru alimsifu Balozi Juma Mwapachu kwa hatua yake ya kuihama CCM na kusema kuwa amefanya uamuzi sahihi.