Sunday, January 14, 2018

Lowassa kufanya mazungumzo na Rais ni jambo lenye afya

 

By Luqman Maloto

Waziri Mkuu wa zamani, Edward Lowassa alikutana na Rais John Magufuli kwa mazungumzo, Ikulu, Dar es Salaam, Januari 9, mwaka huu. Taswira baada ya tukio la Lowassa kukutana na Rais Magufuli, imekuwa hasi upande wa Chadema na chanya upande wa CCM.

Chadema wamejitenga na Lowassa kutokana na kummwagia pongezi Rais Magufuli, kwa utoaji elimu bure, ujenzi wa reli ya kisasa na mradi wa umeme wa Stiegler’s Gorge.

Mwenyekiti wa Chadema, Freeman Mbowe alisema maneno ya Lowassa si msimamo wa chama. na pongezi hazifanani na hali halisi kwa kuwa hivi sasa uhuru wa vyombo vya habari unaminywa, watu wanapotea bila kujulikana wanaenda wapi, mbunge wa Singida Mashariki, Tundu Lissu amepigwa risasi na majibu ya upelelezi hayajatolewa.

Maneno ya Mbowe yanashabihiana moja kwa moja na yale ya mbunge wa Arusha Mjini, Godbless Lema, vilevile salamu za Lissu akiwa kwenye matibabu nchini Ubelgiji. Ukiziweka hoja zao kwenye kapu moja, unaona kwamba lawama zao kwa Serikali ni kuhusu eneo la utawala bora.

Wote watatu walijielekeza kwenye eneo mahsusi ambalo Lowassa hajayapongeza. Swali ni je, elimu bure kwa wanafunzi kuanzia chekechea mpaka kidato cha kwanza, Reli ya ,kisasa na umeme wa Stiegler’s Gorge yanalalamikiwa na Chadema?

Matarajio yalikuwa yapi?

Hapa ndipo kwenye kujadili. Je, ilitarajiwa Lowassa afike Ikulu kisha asimpongeze Rais Magufuli japo katika maeneo machache? Je, matarajio yalikuwa kwamba Lowassa angemwambia Rais Magufuli ana kwa ana kuwa haongozi nchi vizuri, anadidimiza uchumi na anakiuka misingi ya utawala bora? Mtaani wanasema kumpa za uso!

Lowassa, ambaye anafahamika kwa siasa zake za kistaarabu zisizo za jino kwa jino na mwenye kuamini katika mikakati ya kisayansi ili kufanikisha malengo, alitarajiwa kweli ampe za uso Rais Magufuli? Zingatia, Lowassa alikuwa waziri mkuu, anafahamu kiundani mamlaka na nguvu za Rais katika nchi.

Matarajio zaidi ya kile ambacho Lowassa angekizungumza Ikulu mbele ya Rais Magufuli, yanapaswa kuanzia kwenye swali, je, alikwenda kwa kualikwa au aliomba? Jawabu alilitoa Rais Magufuli kuwa Lowassa alimuomba muda mrefu ili wakutane kwa ajili ya mazungumzo. Hivyo Lowassa aliomba.

Tukifika hapo tunakubaliana kuwa Lowassa alikuwa na agenda ya msingi ya kukutana na Rais Magufuli. Kwa maana hiyo Lowassa lipo jambo ambalo alilikusudia au analikusudia kulifanikisha kupitia Rais Magufuli. Na Lowassa anatambua kuwa lugha nzuri ni kilainishi cha mazungumzo.

Lowassa anafahamu ukweli kwamba ukitaka binadamu akuelewe unapomkosoa au unapomweleza kuwa mambo kadhaa anayoyafanya hayapo sawa, ni vizuri pia ukampa orodha ya yale ambayo unayakubali kutoka kwake. Angalau kwa kufanya hivyo unaweza kumshawishi kuyaona makosa yake.

Unahitaji mtu apokee ushauri wako lakini wakati huohuo unamficha japo jambo moja ambalo amewahi kulifanya vizuri na likakuvutia. Mwisho ataona unamchukia. Kwamba huna jema umewahi kuliona kutoka kwake. Kwa maana hiyo hata ushauri wako atauona haupo sawa, isipokuwa tu wenye chuki.

Mwanafalsafa wa Marekani, Daniel Dennett ambaye ni mtafiti na mtaalamu wa sayansi ya fikra, ameliweka hili vizuri katika kitabu chake cha “Intuition Pumps and Other Tools for Thinking” anapoelekeza kuhusu kutoa ushauri wa kiungwana.

“Mkosoaji lazima aeleze ukosoaji wake kwa kuonyesha kila kitu kwa mifano iliyo uwazi, ukweli na haki kiasi kwamba mpaka anayekosolewa ashukuru na kuahidi kufanyia kazi upungufu,” anasema katika kitabu hicho.

Pili; unapokosoa ili unayemkosoa asione unamshambulia, lazima wakati wa kukosoa ueleze baadhi ya mambo mazuri ambayo unayemkosoa anayo na unayaunga mkono. Kwa kufanya hivyo, utampa nafasi akuone wewe humshambulii bali unamsahihisha ili afanye vizuri zaidi.

Bila shaka Lowassa alijua kuwa kwenda Ikulu na orodha ya mambo hasi kuhusu Rais Magufuli na Serikali kisha kutarajia yapokelewe na kufanyiwa kazi, ilikuwa sawa na kupoteza muda. Hivyo kumsifia ilikuwa na maana mbili. Kwanza ni uungwana, pili ni mkakati.

Sasa basi, ama kwa uungwana au mkakati, ni wazi Lowassa alifanikiwa kumteka Magufuli ambaye naye alimmwagia sifa kuwa hakuwahi kumtukana hata mara moja. Ni mara ya kwanza Rais Magufuli kukiri kuwa Lowassa ni mwanasiasa muungwana. Hata kicheko alichotoa kinaweza kuashiria hilo. Na ukishamkubali mtu ni rahisi kupokea ushauri wake.

Kosa la Chadema

Kosa ambalo Chadema wamefanya ni kutoa matamko ya haraka kuonesha wameumizwa na kikao cha Lowassa na Rais Magufuli. Walipaswa kuvuta subira. Wakutane na Lowassa kisha wazungumze, bila shaka angewaridhisha kuhusu sababu za msingi za kumsifu Raia ili kufanikisha agenda yake.

Kitendo cha Chadema kuibuka haraka na kukosoa sifa za Lowassa kwa Magufuli ni kosa la kiufundi. Kwa lugha ya michezo huita kuuza mechi. Chadema wamejipambanua kuwa tayari wameshagawanyika. Siku zote adui hujiona mshindi au hupata faraja anapobaini nyumbani kwa hasimu hapako shwari.

Kama Chadema wangevuta subira, wangekwepa kumzungumzia Lowassa. Hivi sasa kwa CCM kusingekuwa na kicheko kikubwa. Pengine sifa za Lowassa kwa Magufuli zingetafsiriwa kama mkakati wa Chadema kumlainisha Rais Magufuli. Hata hivyo imekuwa tofauti. Tayari wameshauza mechi.

Chadema walikuwa na nafasi nzuri ya kuanza kumtumia Lowassa kufanikisha malalamiko yao ya muda mrefu. Maana imeshaonekana kuwa Lowassa ni mwanasiasa mstaarabu mbele ya Rais Magufuli. Kwa hiyo, kuna mambo Lowassa akiyasema yatapokelewa kwa urahisi na kufanyiwa kazi.

Chadema waache kutazama eneo dogo la kupoteza mtaji wa kisiasa kwa sababu Lowassa amekwenda kinyume nao, badala yake walipaswa kusimama kama chama kikubwa na kutulia ili wakitoa tamko liwe lenye faida nyingi kwa chama na Watanzania wote hivi sasa na hata siku za usoni.

Nafasi ya Lowassa na Watanzania

Kikao cha Lowassa na Rais Magufuli ni vema kimulikwe katika nafasi ya Watanzania na Lowassa mwenyewe. Je, nini masilahi ya Watanzania katika mazungumzo ya Lowassa na Watanzania? Ipi faida ya Lowassa kupitia kikao chake na Rais Ikulu?

Mwaka 2015 nchi ilimpokea Rais Magufuli kuwa Rais wake mpya. Ilikuwa baada ya miaka 10 ya uongozi wa Rais wa nne, Jakaya Kikwete. Rais Magufuli aliingia kwa sura tofauti, hakutaka kuuendekeza mtindo wa Kikwete wa kuzungumza na wapinzani na kupoza joto la kisiasa pale linapokuwa kali.

Katika muda huo hali ya kisiasa imekuwa mbaya. CCM imegeuka chama cha kufanya siasa za kukomoa, wapinzani kila uchwao wanalia kuonewa na kuhujumiwa. Katika uchaguzi mdogo wa kata 43 Tanzania Bara uliofanyika Novemba 26, mwaka jana, hali ilikuwa mbaya. Fujo zilikuwa nyingi, watu walikatwa mapanga.

Wapinzani walilalamika mawakala wao kutolewa nje ya vyumba vya kupigia kura na kushikiliwa kwa saa kadhaa na polisi. Waliporuhusiwa kurudi vituoni, wanadai walikuta masanduku yameshajaa kura.

Kutokana na hali hiyo, wapinzani, hasa Chadema walijitoa kwenye uchaguzi wa kata na majimbo kadhaa. Chadema, CUF, NLD, NCCR-Mageuzi, Chaumma, ACT-Wazalendo wamegomea uchaguzi mdogo wa ubunge majimbo matatu na kata 6.

Ni nyakati ambazo kada wa Chadema, Ben Saanane, amefikisha mwaka mmoja na miezi miwili tangu atoweke, mwandishi Azory Gwanda anakaribia miezi miwili tangu atekwe, maiti zimeokotwa katika fukwe bila majibu waliokufa ni nani na kwa nini.

Lowassa alishazungumzia haki za mashehe walioko mahabusu kwa tuhuma za ugaidi na kesi zao haziishi wala kusikilizwa na tukio la Lissu kupigwa risasi na Bunge kuonekana kujitenga na matibabu yake wakati ni mbunge.

Matukio hayo, kwa mwanasiasa mwenye kuipenda Tanzania kuliko siasa lazima atake mazungumzo. Wa kuzungumza naye ni Rais Magufuli. Hivyo, Lowassa kukutana na Rais Magufuli ni jambo jema, kama tu yaliyojadiliwa ni masuala ya nchi, au shabaha yake ni kutafuta ufumbuzi.

Bila shaka nafasi ya Lowassa kwa Chadema inaweza kuonekana si njema kama ambavyo imeshajionyesha. Hata hivyo inawezekana baadaye akaeleweka zaidi kwa Chadema na Watanzania maana kufanya mazungumzo na Rais ni jambo lenye afya.

Siwazii kuwa Lowassa alikutana na Rais ili kuanza safari ya kurejea CCM. Nawaza afya ya mazungumzo na mwanzo mpya wa milango ya Ikulu kufunguka kujadili masuala ya nchi.

-->