Lushoto wadhihirisha tiba ya kilimo ni teknolojia

Halima Shaban akipalilia shamba lake la kabichi wilayani Lushoto, Mkoa wa Tanga. Picha na Harieth Makwetta

Muktasari:

Walikuwa wanazalisha kidogo na madalali walikuwa wakiwapangia bei hivyo kupata hasara, lakini sasa wana mbinu za kilimo, masoko, wanapata faida inayowainua kimaisha

Familia nyingi za wakulima zimekuwa zikiishi katika hali ya umasikini kutokana na kilimo kutokuwa na tija inayowawezesha kupata kipato kizuri cha kuendesha maisha yao.

Wengi wao wameishia kufanya kilimo cha kuzalisha kwa ajili ya chakula pekee na kuachana na mazao ya biashara kwa kuwa yamekuwa hayastawi vile watakavyo au bei ya soko kuwa ya chini.

Mkulima wa nyanya katika kijiji cha Handeni wilayani Lushoto Mkoa wa Tanga, Halima Shaban ni kati ya wanawake walioonja adha ya kilimo kilichotumia muda mwingi, huku mavuno yakiwa kidogo hali iliyozidi kudidimiza kipato cha familia na kushindwa kusomesha watoto.

Kwa miaka mitano aliyokuwa mkulima, akiwa hajajiunga na chama chochote, alijikita kubadili mfumo wa uandaaji mazao yake bila mafanikio.

“Soko halikuwa rafiki. Tuliuza nyanya mpaka Sh500 kwa kapu. Hii ilitokana na kilimo duni hivyo tukawa tunaishi maisha ya tabu katika nyumba duni na hata watoto walisoma kwa taabu,” anasema.

Halima anayeshughulika pia na ulimaji wa mbogamboga ikiwamo kabichi na matunda aina ya peasi, anaelezea mafanikio aliyonayo baada ya kujiunga kwenye vikundi.

Halima anasema yeye na mumewe Hatibu Bakari wamenufaika kwa kilimo na msaada wa fedha kutoka Shirika la Kimataifa la Oxfam na wanajihusisha na kilimo.

Halima anasema elimu waliyoipata kutoka Oxfam na kuwezeshwa, imewawezesha kupata mazao mengi kwa kulima eneo dogo.

Mwanakikundi mwingine, Mariam Mustafa haamini iwapo kilimo cha mbogamboga alichokianzisha nyumbani kwake kingeweza kuwa na manufaa kwa familia kama ilivyo sasa.

Anasema awali baada ya kulima mbogamboga, alikuwa akisubiri wanunuzi nyumbani jambo ambalo lilikuwa linawafanya madalali kumpangia bei ya kuuzia.

Lakini kwa sasa anasema baada ya kupata mafunzo, ana mbinu mpya za kuvuna na kuyaweka mavuno katika hali nzuri ya kuyasafirisha hadi sokoni ambako huyauza kwa bei nzuri.

Isitoshe, amekuwa mwerevu wa kufahamu bei ya soko hivyo madalali hawawezi kumdanganya tena awauzie kwa bei ya hasara.

Leo hii Mariam ni mwanachama wa Chama cha Wakulima wa Mbogamboga Lushoto na Korogwe (Lucoveg) tangu mwaka 2012 na wameweza kupiga hatua kubwa ya maendeleo na sauti ya pamoja iliyosaidia kukuza bei ya mazao yao.

Mkulima kutoka Mkusi, Happiness Omari anasema amekuwa akijishughulisha na ulimaji wa mbogamboga kama kabichi, nyanya, hoho, njegere na karoti na kwa sasa kipato chake kimezidi kuimarika na kuboresha zaidi maisha yake.

Anasema kabla ya ujio wa Oxfam alikuwa hana kipato kizuri kama ilivyo kwa sasa kwani ana uwezo wa kusomesha watoto wake, kuishi maisha ya kisasa kwa kuwa ana uhakika wa kupata Sh1.5 milioni za mkupuo kila baada ya miezi mitatu hadi minne kama hali ya hewa haikuwa mbaya.

Rajab Dassa, mwenyekiti Mtandao wa Lukoveg anasema mtandao ulianza mwaka 2012 na sasa una vikundi 30 ambavyo vina wanachama 3,500 wanaoshughulika na kilimo cha mbogamboga.

Anasema kwa sasa wanatarajia mazao yawe yanauzwa hadi nje ya nchi, lakini changamoto wanayokabiliana nayo ni ya kuweza kuzalisha kwa kiwango kinachotakiwa.

“Kwa soko la nje lililopatikana, wakulima wana changamoto mpya kwa kuwa wanatakiwa wazalishe angalau tani 20 kwa kila wiki,” anasema na kuongeza kuwa kwa sasa wanazalisha zaidi ya tani 10.

Mkurugenzi wa kampuni ya Homeveg, Mussa Mvungi, anasema wameamua kuweka kambi mkoani Tanga kwa ajili ya kuwajengea uwezo wakulima hao kwa kuwa eneo hilo lipo katika hali nzuri ya hewa ya uzalishaji wa mbogamboga.

Anasema kampuni hiyo inasimamia uuzaji wa mbogamboga na matunda katika soko la nchi za Umoja wa Ulaya (EU).

Mazao wanayotarajia kwenda kuyauza huko ni maharage na njegere kwa kuwa yana soko kubwa kutokana na kuwa na virutubisho vingi kwa afya ya mwanadamu.

Usimamizi

“Tunasimamia kuanzia utaratibu wa awali wa kuandaa mashamba kwa viwango vinavyotakiwa, ambapo wakulima wanaofikia viwango wanapata cheti. Sisi tuko moja kwa moja mashambani ili kuhakikisha wakulima wanafikia viwango vinavyotakiwa, kwa hiyo sisi ni sehemu ya mazao yanayozalishwa,” anasema.

Anasema ili wakulima wanufaike na uzalishaji huo, suala muhimu ni kupunguza gharama za pembejeo na zile za viwanja vya ndege wakati wa usafirishaji.

Mara nyingi wamejikuta wakilazimika kutumia ndege za abiria kama KLM, hivyo kutokuwa na uhakika wa nafasi kwenda katika nchi zenye soko kubwa za Uholanzi, Ubelgiji na Uingereza.

Wakulima hawa wa Lushoto walikuwa wakiendesha kilimo ambacho hakina tija baada ya kupatiwa mafunzo, kuwezeshwa na kutafutiwa masoko wamepata faida na wanaona umuhimu wa kujiajiri kupitia kilimo.

Hili ni fundisho kwa wanasiasa, watunga sera na Serikali kuangalia ni namna gani wataweza kutumia mtindo huu ili kuwawezesha wakulima wengine nchini nao wafaidike kama wenzao wa Lushoto.