Hatua hii itaimarisha huduma za afya

Muktasari:

Waziri wa Afya, Ummy Mwalimu alikaririwa akisema Serikali imekubaliana na wamiliki wa hospitali binafsi kuwa gharama hizo mpya zitatumika kwa mwaka mmoja kabla ya kuzifanyia tathmini.

Jana, gazeti The Citizen lilikuwa na habari inayohusu uamuzi wa Mfuko wa Taifa wa Bima ya Afya (NHIF) kupunguza gharama za matibabu kwa zaidi ya asilimia 60 ikiwa ni mpango wa Serikali kuhakikisha kila mwananchi anapata huduma za afya kwa kiwango sawa na ubora uleule.

Waziri wa Afya, Ummy Mwalimu alikaririwa akisema Serikali imekubaliana na wamiliki wa hospitali binafsi kuwa gharama hizo mpya zitatumika kwa mwaka mmoja kabla ya kuzifanyia tathmini.

Waziri Mwalimu alisema bima ya afya ilikuwa ikitolewa kwa kiwango kidogo cha asilimia 27 tu na NHIF ilikuwa inachangia asilimia 7.2 na kiasi kinachobaki kikitoka Mfuko wa Afya ya Jamii (CHF).

Kwa maana hiyo, bei mpya za NHIF zitapunguza gharama za matibabu, akitoa mfano wa gharama za upasuaji ambazo awali zilikuwa Sh600,000 katika hospitali binafsi, lakini sasa zitakuwa Sh150,000. Kadhalika kwa kutumia kadi ya NHIF, mgonjwa atalipa Sh15,000 tu kumuona daktari bingwa badala ya Sh30,000 za awali. Akitaka kumuona daktari wa kawaida, atalipia Sh7,000 badala ya Sh10,000.

Tunaipongeza Serikali kwa uamuzi huu ambao tuna imani kwamba utakuwa na tija kubwa kwa afya za wananchi, hasa ikizingatiwa kwamba afya ndiyo msingi wa maendeleo ya mwananchi na Serikali kwa ujumla.

Uamuzi huo unamaanisha kwamba mfuko huo sasa utakuwa na uwezo wa kupanua huduma zake ikiwa na maana ya kutoa huduma kwa wananchi na kufanya malipo kwa uhakika zaidi, hasa ikizingatiwa kwamba kwa muda mrefu umekuwa ukitegemea wahisani kama taasisi ya misaada ya Marekani, Usaids na afya ya hiari, Pathfinder.

Huduma sawa za afya imekuwa kero ya muda mrefu kwa kuwa wenye fedha wamekuwa wakipata tiba sahihi na zenye kiwango bora, huku wasionacho wakijikuta wakisumbuka kupata huduma hiyo na pengine kupoteza maisha.

Kwa hatua hiyo, tunaamini kwamba sasa kila mwananchi atapata matibabu bora na mfuko wake utamlinda kwa muda mrefu. Kwa mfano, mgonjwa aliyefanyiwa upasuaji kwa Sh100,000 halafu akaendelea kulazwa hospitali kwa muda mrefu, ni dhahiri amana yake inaweza kwisha katika mfuko. Lakini kwa hatua hii ya kupungua kwa gharama, sasa anaweza kuhudumiwa kwa muda mrefu zaidi.

Wito wetu ni hospitali zote kuendelea kutoa huduma kwa ubora uleule uliokuwa ukitolewa awali kwani suala la afya ni nyeti na linalomgusa kila mwananchi.

Lakini pia Serikali haina budi kuunda chombo cha kudhibiti huduma za afya ili kuhakikisha kwamba zinatolewa kwa uhakika na pia kupunguza uwezekano wa watoa huduma kupandisha bei kadri wanavyotaka.

Chombo hicho kifuatilie kwa karibu utoaji wa huduma na gharama za matibabu kwenye hospitali za Serikali na za umma ili kusiwepo hila kama za kupandisha bei bila kuboresha ubora za tiba.

Pia, kwa mujibu wa mtandao wa NHIF, wananchi watakaonufaika na punguzo hilo ni wale milioni 9.9 wanachama wa NHIF na CHF, sawa na asilimia 23 ya Watanzania wote.

Idadi hiyo ni ndogo katika taifa lenye watu zaidi ya milioni 48. Tunawahimiza wananchi kujiunga na mfumo huo rasmi wa matibabu kwa kuwa ndiyo suluhisho bora na nafuu zaidi kwa afya zao.