MAONI YA MHARIRI: Kauli ya Spika bungeni haikuwa muafaka

Spika wa Bunge, Job Ndugai 

Muktasari:

Hata hivyo, wakati wa kuipitisha bajeti hiyo kuliibuka hoja iliyotolewa na Spika Job Ndugai kuwa kupiga kura za ‘hapana’ kukataa kupitisha bajeti hiyo ilikuwa ni sawa na kukataa kupata mgawo wa fedha za maendeleo.

Bajeti ya mwaka 2017/18 ilipitishwa Jumanne wiki hii baada ya siku saba za wabunge kuijadili, wakianza na bajeti za wizara mmojammoja kwa takribani miezi miwili.

Hata hivyo, wakati wa kuipitisha bajeti hiyo kuliibuka hoja iliyotolewa na Spika Job Ndugai kuwa kupiga kura za ‘hapana’ kukataa kupitisha bajeti hiyo ilikuwa ni sawa na kukataa kupata mgawo wa fedha za maendeleo.

Ndugai alitoa hoja hiyo Jumanne jioni wakati Bunge likisubiri matokeo ya kura kupitisha bajeti ya mwaka 2017/18 ambayo ni Sh31.71 trilioni.

Baada ya kumaliza kupiga kura na kutambulisha wageni, Ndugai alisema badala ya kukaa kimya kusubiri matokeo, anakaribisha miongozo na kuanza na wabunge wa Chadema, Joseph Mbilinyi (Mbeya Mjini) na Mwita Waitara (Ukonga).

Sugu alihoji mantiki ya kauli yake kuhusu kupiga kura ya kukataa bajeti. Na ndipo baada ya kusikiliza hoja zote alisema bajeti ya sasa ni shirikishi tofauti na zamani, kwa hiyo haistahili kupingwa kwa kuwa kufanya hivyo ni kukataa maendeleo.

Spika Ndugai aliwaeleza mawaziri wakati wa mijadala ya mapendekezo ya bajeti za wizara zao kuwa wasipeleke fedha za miradi kwenye majimbo ya upinzani kwa kuwa wanasusia upitishwaji wa bajeti hizo, kauli ambayo alikuwa akiirudia mara kwa mara. Alisema uamuzi wa wabunge hao unatokana na mawazo ya wananchi waliowapigia kura, hivyo wanapopiga kura wajue wanapigia kura wananchi wao.

Suala hilo liliibuka tena juzi, wakati Naibu Waziri wa Ujenzi, Edwin Ngonyani alipomwambia Mbunge wa Mikumi (Chadema), Joseph Haule kuwa minara itajengwa jimboni kwake, lakini akumbuke kuwa aliikataa bajeti ya Serikali.

Kauli hiyo ya Spika imetushangaza na bado tunashindwa kuamini kama alikuwa akimaanisha anachokisema au aliteleza.

Kama wadau wengine walivyotoa maoni yao kuhusu suala hilo, nasi tunaungana nao kupinga msimamo huo wa Spika kwa sababu badala ya kujenga unaweza kubomoa na kutugawa Watanzania.

Kauli hiyo inaweza kuligawa Taifa na kuondoa maana nzima ya demokrasia ambayo ndiyo msingi wa Katiba yetu ambayo inatambua kuwapo kwa mawazo tofauti miongoni mwa wananchi.

Kufanya wabunge wote wawe na mtazamo unaofanana, hauwezi kuwa mzuri kwa afya ya demokrasia nchini na kama tunataka kusonga mbele hatuna budi kukubali mawazo ya pande zote hata kama hayapendezi mbele ya wengine.

Ilimradi nchi ilikubali kuingia katika mfumo wa vyama vingi tangu mwaka 1992, hatuna budi kuishi katika mfumo huo badala ya kudhani kwamba bado tupo katika mfumo wa chama kimoja.

Kunapokuwa na mawazo mbadala hufanya chama tawala kutolala na hivyo hufanya kuwe na maendeleo kwa nchi. Kwa miaka yote wakati wa upitishwaji wa bajeti, kuna wabunge ambao hupiga kura ya ‘ndiyo’ na wengine hupiga kura ya ‘hapana’.

Kwa miaka yote hatujawahi kusikia wabunge wanaopigia kura ya ‘hapana’ wakiambiwa majimbo yao hayatapewa fedha za maendeleo, jambo hilo limetushangaza na hatuamini kama linaweza kuchukuliwa na kutekelezwa na mawaziri.

Tunashauri viongozi wanapotoa kauli zao wawe wanazipima kwanza, kwa sababu zinaweza kusababisha utengano badala ya kuleta umoja.

Tunajua hata kwenye halmashauri nyingi kuna madiwani wa vyama vyote na wanapopitisha bajeti zao huwa wanatofautiana, kuna wakati wabunge wa CCM hupinga bajeti za halmashauri na hiyo haimaanishi kuwa huwa hawataki fedha za maendeleo, lakini ni kutokubaliana na baadhi ya mambo yaliyo ndani ya bajeti husika.