MAONI YA MHARIRI: NEC imetimiza wajibu, vimebaki vyama

Mkurugenzi wa Uchaguzi wa Tume ya Taifa ya Uchaguzi(NEC), Ramadhan Kailima 

Juzi, Tume ya Taifa ya Uchaguzi (NEC), ilitangaza kuwarejesha wagombea tisa wa udiwani ambao walienguliwa katika uchaguzi mdogo uliopangwa kufanyika Novemba 26.

Taarifa iliyotolewa na NEC imesema kati ya rufaa 15 zilizowasilishwa, tisa zilikuwa za wagombea ambao hawakuridhishwa na uamuzi wa wasimamizi wa uchaguzi waliowaengua kutoka katika orodha ya wagombea wa udiwani katika kata mbalimbali.

Hatua hii ni ya kupongezwa kwani tunaamini kwamba itakuwa imefunga mjadala na malumbano ya kisiasa yaliyokuwa yameanza kujitokeza kabla ya uamuzi huo.

Lakini mbali ya uamuzi huo kufunga mjadala huo, tunaamini kwamba haukufanywa kwa shinikizo la kisiasa, bali kwa kuzingatia haki na sheria na taratibu zilizowekwa.

Ndiyo maana Tume katika taarifa yake imesema kuanzia Novemba 3 hadi 4, kwa mujibu wa Kanuni ya 29 ya Kanuni za Uchaguzi wa Serikali za Mitaa (Uchaguzi wa Madiwani) za mwaka 2015, ilipokea, ilijadili na kufanya uamuzi wa rufaa hizo.

Baada ya kuzipitia rufaa hizo tisa, NEC imesema imezikubali na kuwarejesha kugombea udiwani katika kata husika kuanzia Novemba 4 na kwa maana hiyo, wagombea hao sasa watashiriki kikamilifu katika uchaguzi huo na wananchi ndiyo watakaoamua nani wa kutoka chama gani atakayewaongoza katika kata zao.

Kadhalika, NEC imeeleza kwamba rufaa sita kati ya hizo 15, ziliwasilishwa na wagombea ambao hawakuwa wameridhishwa na uamuzi wa wasimamizi wa uchaguzi wa kuwaruhusu wagombea wenzao kuendelea kugombea udiwani katika halmashauri mbalimbali na kwamba imezikataa na kukubaliana na uamuzi wa wasimamizi wa uchaguzi, hivyo waendelee kuwa wagombea.

NEC imesema taarifa rasmi za uamuzi zimetumwa kwa wasimamizi wa uchaguzi ili wawapatie wahusika. Tunaamini kwamba wasimamizi wa uchaguzi watakuwa wameshapokea na kuwapatia wahusika taarifa hizo tayari kwa kujiandaa kushiriki katika uchaguzi huo.

Ni imani yetu kwamba uchaguzi huo ambao utahusisha kata 43 nchini utakuwa huru na wa haki na kuifanya Tanzania kuendelea kuwa mfano wa kuigwa linapokuja suala la demokrasia.

Tunaamini kwamba vyama 13 ambavyo vimesimamisha wagombea katika uchaguzi huo vya ACT – Wazalendo, Ada – Tadea, ADC, CCM, Chadema, Chauma, CUF, DP, NCCR-Mageuzi, NRA, Sau, TLP na UDP, vitaendelea na kampeni za kistaarabu zinazozingatia maadili na kubwa, mwelekeo wa kuipeleka Tanzania katika hatua kubwa zaidi ya maendeleo.

Kwa kufanya hivyo, vyama hivyo vitakuwa vinajenga msingi madhubuti kwa ajili ya chaguzi nyingine ndogo, ule wa Serikali za Mitaa wa mwaka 2019 na Uchaguzi Mkuu wa 2020 ambao utahusisha nafasi za Rais, wabunge na madiwani.

Kwa sababu hiyo, tunaviasa vyama vyote vya siasa kujipanga na kuyachukulia yote yaliyojitokeza katika mchakato wa uchaguzi huu wa Novemba 26 kama darasa kwa ajili ya chaguzi hizo zijazo.

Vijipange vyema kisheria, kikanuni na kiutaratibu katika suala zima la kuwapata na kuwapitisha wagombea ili kuepuka uwezekano wa mapingamizi ambayo yanaweza kuvinyima fursa ya kupata uwakilishi. Pia, viutumie uchaguzi huu wa marudio kama fursa ya kujijenga na kujiekea mizizi ya kufanya vyema katika chaguzi kubwa zaidi zijazo.

Tume imeshatimiza wajibu wake, kazi imebaki kwa vyama husika kujipanga.