MAONI YA MHARIRI: Simbu ameonyesha jitihada Michezo ya Olimpiki

Muktasari:

Katika mbio hizo, Eliud Kipchoge wa Kenya alitwaa medali ya dhahabu kwa kutumia saa 2:8.44 ikiwa ni dhahabu ya sita kwa Kenya katika msimamo wa medali kwa michezo hiyo.

Michezo ya Olimpiki ya Rio de Janeiro, Brazil ilifikia kilele juzi Jumapili kwa mbio za marathon.

Katika mbio hizo, Eliud Kipchoge wa Kenya alitwaa medali ya dhahabu kwa kutumia saa 2:8.44 ikiwa ni dhahabu ya sita kwa Kenya katika msimamo wa medali kwa michezo hiyo.

Kipchoge alifuatiwa na Feyisa Lilesa wa Ethiopia aliyetumia saa 2:09.54. Galen Hawkins wa Marekani alishika nafasi ya tatu kwa kutumia saa 2:10:05 huku Ghirmay Ghebreslasse wa Eritrea akitumia saa 2:11.04 na kushika nafasi ya nne. Alphonce Simbu wa Tanzania alitumia saa 2:11.15 kumaliza mbio hizo za kilomita 42 na kushika nafasi hiyo ya tano.

Wanariadha wengine wa Tanzania walioshiriki mbio hizo walikuwa ni Said Makula aliyeshika nafasi ya 43 wakati Fabian Joseph alishika nafasi ya 112.

Simbu alishika nafasi hiyo akiwashinda wanariadha 150. Pamoja na kwamba hakutwaa medali yoyote, nafasi aliyoifikia ni mafanikio kwake na Tanzania hasa ikizingatiwa kwamba, Taifa halijawahi kupata mafanikio hayo tangu miaka ya 1980.

Tunampongeza Simbu kwa hatua kubwa aliyoifikia, tukiamini kwamba kwa umri wake wa miaka 24, akiongeza mazoezi na maandalizi mazuri, atamfanya vizuri zaidi katika mashindano makubwa ya kimataifa yanayokuja yakitanguliwa na Michezo ya Afrika, Michezo ya Jumuiya Madola na hata mashindano

ya ubingwa wa riadha wa Dunia na Michezo ya Olimpiki ya mwaka 2020 huko Tokyo, Japan.

Simbu pamoja na mwogeleaji, Hilal Hilal ambaye naye katika eneo lake alikuwa wa kwanza, japo pointi zake za ushindi hazikutosha, kwa pamoja wameonyesha ushindani na kutuondoa kwenye ile dhana ya wasindikizaji katika michezo.

Tunaamini kwamba wakiendelea na maandalizi, vijana wetu hawa wanaweza kututoa kimasomaso katika Michezo ya Afrika ambayo itaandaliwa na ama Accra (Ghana), Lusaka (Angola) au Nairobi (Kenya), Michezo ya Madola itakayofanyika Australia mwaka 2018 kabla ya Olimpiki Tokyo.

Tanzania inapaswa kubadilika linapokuja suala la michezo hasa hii ambayo ni mikubwa na yenye kuvuta hisia za karibu kila taifa katika uso wa Dunia hii. Jana, katika maoni yetu tulihoji tulichojifunza katika Olimpiki ya Rio de Janeiro, tukiamini kwamba kumalizika kwake ni mwanzo wa maandalizi ya

olimpiki inayofuata.

Kila mchezo umewekewa vigezo vya kufuzu. Hatuna budi kuanzia sasa kujikita katika vigezo hivyo ili kupata siyo tu wanamichezo wenye weledi wa kupambana na wenzao wa mataifa mengine, bali kuondokana na dhana ya kubebwa na kuishia kujaza nafasi.

Umakini wa wenzetu Kenya unafaa kuigwa.

Kwao, waliopata nafasi wanashindanishwa tena na anayefanya vyema, ndiye anayepata tiketi ya kushiriki katika mashindano makubwa.

Baraza la Michezo la Taifa (BMT), Kurugenzi ya Michezo, Msajili wa Vyama vya Michezo na Klabu na vyama vyenyewe viunganishe nguvu kuanzia sasa kuhakikisha kwamba tunatoa ushindani utakaolijengea heshima Taifa letu.

Waziri mwenye dhamana ya michezo, asimamie hili kikamilifu kwani tunaamini kwamba likifanywa kwa weledi, litafanya kubwa ya kuitangaza nchi hii.

Tunaamini tunaweza, tunachohitaji ni msukumo wa kufikia malengo yetu. Tunauona mwelekeo mzuri wa kikosi cha vijana wa timu ya Taifa ya soka ‘Serengeti Boys’, tunataka pia katika michezo mingine.